SERIKALI KULINDA MASLAHI YA WANAHABARI
Na Immaculate Makilika na Prisca Ulomi, Mwanza
Serikali imesema imedhamiria kulinda maslahi ya waandishi wa habari nchini kwa kutatua
changamoto mbalimbali zinazowakakabili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape
Nnauye , jijini Mwanza katika Uwanja wa Nyamagana wakati aliposhiriki katika tukio la
kuaga miili ya wanahabari 5 waliofariki katika ajali ya gari iliyotokea jana Januari 11, 2022
katika Wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu wakati wakielekea kwenye ziara ya kukagua miradi
na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Robert Gabriel
Mhe. Nape amewataka waajiri wa waandishi wa habari waliopata ajali na kufariki katika ajali
hiyo kuwalipa maslahi yao kwa familia za marehemu.
"Natoa siku 7 kwa waajiri wote kuanzia leo kulipa haki za wanahabari waliofariki na taarifa
za uthibitisho wa malipo iwasilishwe kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza" alisisitiza Waziri
Nape
Aidha, Waziri alisema kuwa Serikali itapitia upya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka
2016 kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo ili kuboresha maslahi ya Wanahabari nchini.
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza tupitie mapungufu ya sheria hiyo na
kurekebisha , mimi nitahakikisha nalinda uhuru na haki zenu ziko salama mikononi mwa
Rais Samia, nami nitasimamia kwa kuwa sasa nimerudi nyumbani kusimamia sheria hii na
tutahakikisha haki zenu zinalindwa kwa vile mimi ni muasisi wa sheria hii" Alisisitiza Waziri
Nape
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Mhandisi Gabriel alisema kuwa huu
umekua msiba wa Taifa na Viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan wametuma salamu za pole kwa wafiwa
na wananchi wa Mkoa wa Mwanza.
Aidha, aliongeza kuwa Mkoa wa Mwanza umepata pigo kubwa na watahakikisha viongozi
wa Mkoa huo wanaendelea kutoa ushirikiano kwa wanahabari nchini ili kusaidia waendelee
kutekeleza majukumu yao kwa weledi.
Wanahabari watano waliofariki katika ajali hiyo ni Abel Ngapemba, Afisa habari wa Mkoa
wa Mwanza, Steven Masengi, Afisa habari Wilaya ya Ukerewe na Husna Milanzi mwandishi
wa ITV, Johari Shani mwandishi wa Uhuru digital na Anthony Chuwa mwandishi wa
kujitegemea.