NAIBU WAZIRI PINDA AELEKEZA UENDELEZAJI MIJI KUZINGATIA MIPANGO KABAMBE

Na Munir Shemweta, WANMM Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda amezielekeza Halmashauri zote nchini kuhakik...

Latest Post

BREAKING NEWS: MADIWANI WAJIFUNGIA MASAA 5 KUHUSU KUMKATAA MKURUGENZI WA JIJI BW. ATHUMANI KIHAMIA.

Written By CCMdijitali on Tuesday, June 27, 2017 | June 27, 2017


MADIWANI  WAJIFUNGIA MASAA 5 KUHUSU KUMKATAA MKURUGENZI WA JIJI BW. ATHUMANI KIHAMIA.

Madiwani hao wakiongozwa na mbunge  wa Arusha mjini Godbless Lema walijiorodhesha majina kwa idadi ya theluthi moja ya madiwani wote kwa lengo la kuitisha baraza maalum la kumkataa mkurugenzi huyo ambaye wanamtuhumu kuwa tangu alipoingia amekuwa na Kazi moja ya kuvuruga madiwani wa Chadema.

Awali desemba 2016 TAMISEMI iliunda tume ya watu 5 kufuatilia utendaji kazi wa mkurugenzi huyu lakini bado habadiliki. Madiwani  hao hivi karibuni  mnamo tarehe 23 juni 2017 walijifungia katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri kumjadili mkurugenzi huyo kwa tuhuma za   kupuuza maazimio ya vikao na kutekeleza ya kwake na washirika wake. amekuwa  akiwaweka ndani ndani madiwani kwa kutumia polisi na kulazimisha maamuzi yasiyo ya madiwani kuhusu upangishaji wa maduka ya jiji na kutowaondoa wamachinga mjini na mengineyo mengi.  Baada ya mjadala mzito yafuatayo yaliamuliwa dhidi ya mkurugenzi  huyo.

  1. Apelekwe kwenye kamati ya maadili inayoongozwa na Profesa Mosha ili asomewe  tuhuma hizo za kuendesha halmashauri kibabe.

2. Baada ya hapo baraza maalum la madiwani kuitishwa na    kumsomea tuhuma na  kumkataa siku hiyohiyo.

3. Endapo maamuzi ya kumkataa yakipuuzwa baraza la madiwani litavunjwa kuliko kuendelea kuongozwa na mkurugenzi huyu ambaye hatabiriki na haeleweki anachokitaka.

4. Kama ilivyo kwa RC Mrisho Gambo mkurugenzi  huyu amekuwa akiundiwa tume na hata kupelekwa PCCB kila Mara hasa alipokuwa Kaliua mkoani Tabora kwa kuvurugana  na madiwani na kukataa kutekeleza maazimio ya vikao ambapo alipohamishwa walifanya sherehe.

5. Baraza likivunjwa itatengenezwa migogoro Ili mabaraza mengine ya halmashauri zinazoongozwa na Chadema zivunjwe kisha maandamano yaanze nchi mzima.  

Akiongea na chanzo hiki diwani mmoja wa viti  maalum Chadema amesema kwa ufupi mitego yote ya kumnasa Mkurugenzi huyu ni kama  imeshindikana ikiwemo kumtegeshea asaini nyaraka zenye utata kwa kuwatumia wakuu wa idara au kumtengenezea ajali ya gari au kumteka au   kumchafua ikiwemo  kumteka  mwalimu Batuli Kisaya wa shule ya msingi ya Unga limited.  

"Tukifika 2020 na huyu mtu  tutaharibikiwa ni vyema mgogoro iwe mikubwa ili mheshimiwa rais amtoe vinginevyo bora kuvunja  baraza kuliko kuingia katika uchaguzi akiwepo maana hatutabaki salama damu itamwagika kwa kuwa anafahamika akipewa maagizo na serikali anatekeleza kama yalivyo   hapunguzi hata nukta ni hatari hakutakuwa na haki hata kidogo" alisema mbunge Lema. 

Rafiki wa karibu wa mmoja wa wasaidizi wa karibu  Mkurugenzi Huyo amethibitisha kuwa kwa jinsi alivyo tangu amefika hajabadilika wala kuonyesha dalili za kubadilisha misimamo yake, kwa kweli kazi ipo.


CCM Dijitali yawaletea Ujumbe wa "IDD EL Fitri 2017"



Salamu za Eid Mubarak

Written By CCMdijitali on Sunday, June 25, 2017 | June 25, 2017




Samia: Rushwa husababisha wananchi kukosa imani na serikali yao

Written By CCMdijitali on Thursday, June 22, 2017 | June 22, 2017


Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
 
Imeandikwa na Katuma Masamba - Habari Leo

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema rushwa ni miongoni mwa vitu vinavyoharibu maendeleo na kwamba kukithiri kwa vitendo hivyo katika nyanja mbalimbali kunasababisha wananchi kukosa imani na serikali yao.

Samia ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi) wakati akizungumza kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa Kimataifa wa kubadilishana uzoefu katika vita dhidi ya rushwa ambapo amesema, rushwa inatakiwa kushughulikiwa kuanzia kwenye kiini na kwamba serikali inalihakikisha hilo.

“Rushwa ni uovu ambao umeendelea kuharibu nyanja zote za maendeleo ya binadamu. Rushwa hudhoofisha utawala wa sheria, hivyo huharibu uaminifu wa umma kwa serikali,” alisema Samia.

Alisema serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli imejidhatiti katika mapambano dfhidi ya rushwa na kwamba tayari kuna mikakati mbalimbali iliyowekwa kwa ajili ya vita hiyo ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Rushwa na Mpango wa Utekelezaji wa Awamu ya Tatu (NACSAP III).

Mkutano huo unafanyika nchini kutokana na ombi la Rais John Magufuli kwa Rais wa Benki ya Dunia, Jim Yong Kim kusaidia Tanzania katika kuimarisha utawala bora. Mkutano huo unaelezwa utakuwa msaada kwa Tanzania katika vita dhidi ya rushwa. Mwisho.


Azindua viwanda vikubwa 3


Rais John Magufuli akijaribu kuendesha trekta katika kiwanda cha kutengeneza matrekta aina ya Ursus kilichopo Kibaha mkoani Pwani jana baada ya kuzindua mradi wa kutengeneza matrekta hayo. (Picha na Ikulu).



RAIS John Magufuli amezindua viwanda vikubwa vitatu na mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa mabomba makuu kutoka Mlandizi hadi Dar es Salaam, katika siku ya pili ya ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani jana.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, kwanza, Rais Magufuli alizindua kiwanda cha kutengeneza vifungashio cha Global Packaging Tanzania Ltd kilichopo katika eneo la viwanda Kibaha ambacho kina uwezo wa kutengeneza mifuko ya sandarusi 53,000 kwa siku kwa ajili ya kuhifadhia mazao.

Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Mtanzania, Joseph Wasonga kimeajiri watu 110 na kimejengwa kwa gharama ya takribani Sh bilioni nane. Aidha, Dk Magufuli alizindua mradi wa kutengeneza matrekta 2,400 aina ya Ursus ambao utagharimu Sh bilioni 55, na matrekta hayo yatasambazwa nchi nzima kwa ajili ya kuboresha sekta ya kilimo.

Mradi huo unamilikiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 na utazalisha matrekta ya aina 6 zenye nguvu ya kuanzia HP50 hadi HP 85. Pia jana, Rais Magufuli alizindua kiwanda cha chuma cha Kiluwa Steel Group kilichopo Mlandizi ambacho katika awamu hii ya kwanza kina uwezo wa kuzalisha tani 500,000 za nondo kwa mwaka na awamu ya pili kitaongeza uzalishaji hadi kufikia tani milioni 1.2 kwa mwaka.

Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing alisema kiwanda hicho kinachomilikiwa na Mtanzania Mohamed Kiluwa kwa asilimia 51, asilimia 49 zinamilikiwa na mwekezaji kutoka China ikiwa ni mwendelezo wa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya China na Tanzania.

Aidha, Shirika la Reli Tanzania (TRL) limejenga njia ya reli ya kilometa 3.5 inayounganisha kiwanda hicho na reli ya kati ikiwa ni juhudi za kurahisisha usafirishaji wa malighafi na vyuma vinavyozalishwa kiwandani hapo kwenda ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika miradi hiyo, Rais Magufuli alipongeza uwekezaji huo na akaagiza vyombo vinavyohusika kutoa vibali kwa ajili ya ujenzi wa viwanda hapa nchini viondoe urasimu ambao umekuwa ukiwakatisha tamaa wawekezaji kujenga viwanda.

Dk Magufuli alitoa mwito kwa wamiliki wa viwanda hivyo kujali maslahi na usalama wa wafanyakazi waliowaajiri, amezitaka benki nchini kujielekeza kufanya biashara na wananchi kwa kuwakopesha mitaji wafanyabiashara na wajasiriamali badala ya kutaka kufanya biashara na serikali na ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha viwanda vya chuma vinatumia malighafi za hapa nchini kutoka Mchuchuma na Liganga.

Leo Rais Magufuli atakamilisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu mkoani Pwani kwa kuzindua kiwanda cha vinywaji baridi cha Sayona Drink Ltd, kuzindua kiwanda cha kukausha matunda cha Elven Agric Company na kuzindua mradi wa barabara ya Bagamoyo – Msata.


Magufuli ‘amtumbua’ Mutalemwa Dawasa


     Imeandikwa na Shadrack Sagati

RAIS John Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam, (Dawasa), Archad Mutalemwa ‘kuachia ngazi’ kwa maelezo kuwa amekaa muda mrefu katika mamlaka hiyo.

Rais pia amemwagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji kuhakikisha anamaliza mkanganyiko uliopo kati ya Dawasa na Kampuni ya Maji Safi Dar es Salaam (Dawasco) juu ya uendeshaji wa huduma ya maji na pia amemwagiza namna ya kuangalia kuunda bodi moja ya maji; badala ya kuwa na bodi mbili zinazosimamia taasisi hizo mbili.

Mbali na hilo, alisema taasisi za serikali zisizolipia huduma ya maji zinapaswa kukatiwa huduma hiyo na kwamba wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa wilaya ambao taasisi zao nyeti zitakatiwa maji, wajihesabu kuwa wameshindwa kazi kwa sababu fedha zinatolewa kulipia huduma hiyo muhimu.

Rais Magufuli pia ameiagiza Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuhakikisha kwamba wafanye kila linalowezekana mji wa Kisarawe mkoani Pwani upatiwe maji haraka na pia wakamilishe mradi wa maji wa Lindi ambao alisema umekaa kwa muda mrefu bila kukamilika.

Dhambi za wizara
Akizindua mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu na ulazaji wa mabomba makuu kutoka Mlandizi kwenda Kibamba, Dar es Salaam, Rais Magufuli alitaja upungufu ya wizara ni kuwepo kiwanda jijini Dar es Salaam ambacho kilifunga bomba la maji bila kupitishiwa kwenye mita.

Alisema kinatumia maji mengi, lakini hawalipi bili. Pia alisema kuna kampuni moja inajenga barabara ilikuwa inatumia maji ya Dawasco bila kulipa ankara zao. “Sasa kama hao matajiri hamuwadai ankara zenu, inakuwaje wananchi hawa maskini mnakuwa na viherehere vya kwenda kuwadai bili zao,” alieleza Rais Magufuli katika hotuba yake kwa wananchi.

Pia alisema kuna wafanyakazi wa Dawasco ambao anawafahamu wanaouza maji na fedha zinaenda kwenye akaunti zao na akasisitiza kuwa anafahamu hadi akaunti zao. Alimwagiza waziri alifanyie kazi yeye mwenyewe.

“Rekebisheni dhambi zenu zilizopo, hapa Ruvu mmepata A, lakini kule kwingine mmepata C maana mambo yenu hayaendi vizuri,” alisema Rais. Amvaa bosi wa Dawasa Rais Magufuli katika hotuba yake alihoji, “Kuna wanaouliza hivi Mutalemwa utastaafu lini?

Maana nimeanza kukusikia nikiwa bado sekondari. Mzee wangu jiandae kustaafu, unaweza kuwa na mwili mzuri; lakini umri umekwenda tunataka kukutumia kwa kazi zingine za taifa hili. “Hivyo nakuomba mzee wangu jiandae kustaafu kwa haraka kabla ya mabaya hayajakupata.

Maana ukikaa sehemu kwa muda mrefu hata kama watu wanakupenda unaweza kukumbwa na mabaya. Mimi hili nimeona niliseme tu kwa uwazi,” alisema Rais Magufuli. “This is your time, umefanya kazi nzuri, waachie vijana ili tushughulike nao, tufukazane nao.

Kama umenisikia nielewe, kama hujanielewa….,” alisema Rais Magufuli. Upotevu wa maji udhibitiwe Kuhusu kupotea maji, Rais Magufuli alisema nchi inaweza kukopa fedha nyingi, lakini asilimia kubwa ya mapato hayo yanaweza kupotea kwa maji yanayopotea.

Aliwaomba watendaji wa wizara hiyo kuhakikisha hakuna maji yanayopotea. Alisema Wizara ya Maji na Umwagiliaji wamefanya kazi nzuri, licha ya kuwa kazi zao hazionekani. “Dawasa na Dawasco tembeeni vifua mbele kwani mnafanya kazi kubwa.

Nimeiona kazi nzuri na ya kufurahisha,” alisema Magufuli. Aliwahakikishia kuwa serikali iko pamoja nao na akawataka miradi ambayo haijakamilika ukiwemo wa Lindi, wajipange na ikiwezekana Dawasa wahamie wote Dawasco wakausimamie ili uweze kukamilika.
Alisema anafahamu kuna utata kati ya Dawasa na Dawasco. “Nafahamu kuna contradiction (mkanganyiko) kati ya pande hizo mbili kati ya Dawasco na Dawasa.

Dawasco wanahoji kwa nini
Dawasa wakimaliza kufanya kazi kwa nini wasijiunge pamoja na Dawasco kufanya kazi pamoja, lakini Dawasa nao wanauliza kwa nini tusibaki na miradi hii ili tuiendeshe sisi, kwa nini tunawapa Dawasco?

Hili naliacha kwa Wizara ya Maji,” alieleza Dk Magufuli. Aagiza kukata maji Rais Magufuli pia aliiagiza wizara kuhakikisha taasisi zake zinawakatia maji taasisi zote za serikali ambazo zinadaiwa kiasi hicho cha Sh bilioni 40.

Alisema wizara hiyo ifanye uhakiki wa madeni hayo na wapeleke Wizara ya Fedha na Mipango taasisi zote zinazodaiwa ili fedha hizo zikatwe huko huko. “Na nyinyi pia lipeni shilingi bilioni nane mnazodaiwa za umeme, lakini msipofanya hivyo pia nitaiagiza Wizara ya Fedha ikate huko huko,” alisema.

Aliongeza: “Tumezoea kudekezana, maana wizara ina bajeti na fedha za matumizi zinapelekwa, lakini vipaumbele vyao vinakuwa safari za nje na semina na wanacha kulipia maji.”

Kisarawe ipatiwe maji
Aliagiza wizara kuhakikisha kuwa wanafikisha huduma ya maji katika mji wa Kisarawe ili nao wafaidike na huduma ya maji kwa kuwa nao wamekuwa wanatunza vyanzo vya maji.
Aliwataka wahandisi wa wizara hiyo kusahau yaliyopita; badala yake sasa watumie elimu zao kuwahudumia wananchi. Rais Magufuli aliwaagiza wizara na taasisi zao wakapunguze makongamano na semina ili wakafanye kazi.

“Semina zenu hizi naziorodhesha… bodi zikasimamie kazi…lakini pia hakuna haja ya kuwa na bodi nyingi ya Dawasco na Dawasa, kwa nini tusiwe na bodi moja inayosimamia maji?” alihoji.

Katibu ataja miradi saba Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Emmanuel Kalobelo alisema mradi wa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu ni miongoni mwa miradi saba ya kimakakati ambayo inalenga kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na miji ya Kibaha, Mlandizi na Bagamoyo.

Alitaja miradi hiyo kuwa ni upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini, upanuzi wa mtambo wa Ruvu Juu, uchimbaji wa visima virefu vya Kimbiji na Mpera, ujenzi wa bwawa la Kidunda, upanuzi wa mtandao wa usambazaji maji katika meneo yote yanayohudumuiwa, kupunguza upotevu wa maji na uboreshaji wa mfumo wa mitandao ya majitaka.

Alisema miradi hiyo inalenga kuongeza uzalishaji wa maji kutoka ujazo wa lita milioni 300 hadi lita milioni 750 kwa siku ifikapo mwaka 2020. Balozi wa India, Sandeep Arya alisema tangu Waziri Mkuu wa India, Narenda Modi alipofanya ziara yake nchini, hatua mbili zaidi zimepangwa katika ushirikiano baina ya hizo mbili ikiwemo kusainiwa kwa mkataba mwezi uliopita kwa ajili ya upanuzi wa usambazaji wa maji katika miji ya Tabora, Nzega na Igunga.



 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link