NAIBU WAZIRI PINDA AELEKEZA UENDELEZAJI MIJI KUZINGATIA MIPANGO KABAMBE

Na Munir Shemweta, WANMM Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geofrey Pinda amezielekeza Halmashauri zote nchini kuhakik...

Latest Post

BALOZI SEIF ALI IDDI AFUNGA MKUTANO WA 18 WA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR

Written By CCMdijitali on Friday, January 30, 2015 | January 30, 2015

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufunga Mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukiendelea katika ukumbi wa Majengo ya Baraza hilo uliyopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Aliyepo meza ya juu ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho akiambatana na Makatibu na walinzi wa Baraza  hilo wakitoa nje mara baada ya kufungwa kwa Mkutano wa 18 wa Baraza la 
Wawakilishi Mbweni.
Picha na – OMPR – ZNZ.

                                        Press Release:-

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakamilisha utafiti wa kuibua vivutio vipya vya Utalii vilivyopo katika maeneo ya vijiji nchini ambapo matokeo ya utafiti huo yatasambazwa kwa wanachi ili kuongeza uelewa wa fursa za sekta ya utalii zilizomo katika maeneo yao.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akiufunga Mkutano wa 18 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliokuwa ukiendelea katika ukumbi wa Majengo ya Baraza hilo yaliyopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Balozi Seif alisema utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kutoa ajira za moja kwa  moja zaidi kwa Wananchi hasa wale wa Vijijini katika kuendeleza ile azma ya Serikali ya kuimarisha Utalii kwa wote.

Alisema mwishoni mwa mwaka uliopita Sekta ya Utalii imefanikiwa kutoa fursa za ajira zisizokuwa za moja kwa moja zipatazo 60,000 na zile za moja kwa moja 22,884 ambapo takwimu zinaonyesha wazi kwamba mchango wa sekta ya utalii katika pato la Taifa umefikia asilimia 27%.

Balozi Seif alieleza kutokana na mchango mkubwa wa sekta ya utalii katika maendeleo ya Taifa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya kitaasisi na kiutendaji ili kukidhi viwango vinavyokubalika kimataifa katika utoaji wa huduma za kitalii.

Alifahamisha kwamba Serikali itazidi kuhamasisha wananchi kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango ambazo zitakuwa na uwezo wa kuingia kwenye  soko la utalii na hivyo kuifanya sekta hii kuzidi kuwanufaisha zaidi wananchi ambao ndio walengwa wakuu.

Alieleza kuwa hivi sasa wananchi waliowengi hasa wakulima wamepata fursa ya kuuza bidhaa wanazozalisha mashambani kuuza kwenye hoteli mbali mbali hali ambayo imeongeza upatikanaji wa soko la uhakika wa bidhaa zao.

Alisema kuwa ili sekta ya utalii izidi kukuwa na kuleta tija hakuna budi kwa Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na wananchi kuimarisha vivutio pamoja na mindombinu itakayowavutia watalii ikiwemo usafi na utunzaji wa mazingira, uwekezaji katika ujenzi wa hoteli zenye viwango bora.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliziagiza Taasisi zinazohusika katika kusimamia sekta hiyo kuandaa na kutekeleza mipango itakayoamsha ari ya wananchi kupenda kutembelea maeneo yenye vivutio vya utalii kwa lengo la kukuza utalii wa ndani.

Hata hivyo Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba kuimarika kwa utalii washirika wote wa sekta hiyo hawanabudi kuhakikisha kwamba mapato yatokanayo na  eneo hilo yanakusanywa kikamilifu na kuingia katika mfuko Mkuu wa Serikali.

Aliendelea kusisitiza umuhimu wa kuendelea kudumishwa kwa amani iliyopo hapa nchini ambayo ndiyo kichocheo kikubwa kinachotoa fursa kwa wageni na watalii kupenda kuvitembelea visiwa vya Zanzibar.

Akizungumzia sekta ya kilimo ambayo bado ni tegemeo kubwa la wananchi waliowengi katika kujipatia ajira, kipato,chakula na kuimarisha lishe na afya zao Balozi Seif alisema Serikali inaendelea kutoa msukumo mkubwa kusaidia sekta hiyo ili wananchi waweze kuongeza tija na uzalishaji na hivyo kuimarisha vipato vyao.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kwamba huduma za kilimo cha matrekta na zana nyengine za kilimo zinapatikana kwa uhakika na kwa bei nafuu zitakazotoa nafasi kwa  wakulima kuzimudu.

Alisema mpango huo utakwenda sambamba na ongezeko la kiwango cha upatikanaji wa mbegu bora ya mpunga, dawa ya kuulia magugu na mbolea kupitia programu ya ruzuku katika kilimo cha Mpunga.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa wakulima wote wa zao la mpunga nchini kuungana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali kwa kutumia fursa zilizopo kuhakikisha wanalima kwa wakati na kufuata kanuni za kilimo bora.

Halkadhalika Balozi Seif akawahimiza wakulima wote wa mazao mengine kuchukuwa juhudi stahiki kwa kufuata ushauri wa mabwana shamba na Mabibi shamba ili nao waweze kuongeza uzalishaji wa mazao yao.

Akigusia suala la udhalilishaji wa kijinsia ambalo linaendelea kuwa changamoto licha ya juhudi zinazochukuliwa za kudhibiti vitendo viovu lakini Balozi Seif alisema bado wapo watu miongoni mwa jamii wanaoendeleza vitendo hivyo.

Alisema ni wajibu wa kila mwana jamii kuzidisha mapambano dhidi ya waovu wanaohusika na matendo hayo kwa kuwafichua na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria  bila ya kuwaonea muhali.

Alisema waovu hao kwa kiasi kikubwa wanavunja utu na heshima za kibinaadamu na kuwasababishia madhara makubwa ya kimwili na kiakili.

“ Watu wote wenye taarifa za waovu hao ni vyema kutosita kufika mahakamani kwa kutoa ushahidi pale wanapohitajika na kuacha kabisa masuala hayo kumalizikia majumbani “. Alisema Balozi Seif.

Kuhusu  utolewaji wa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wananchi pamoja na Viongozi  hasa wale wa Kisiasa waelewe kwamba huduma hiyo hutolewa kwa mujibu wa sheria nambari 7 ya Mwaka 2005.

Alisema muhusika lazima atimize matakwa ya sheria hiyo kabla ya kupatiwa kitambulisho ambayo ni pamoja na Mzanzibari wa kuzaliwa, mwananchi kukaa katika eneo lake  si chini ya miezi 36 sambamba na kutimiza umri wa miaka 18.

Hata hivyo Balozi Seif alifafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 13 { 1 } { 2 } cha sheria hiyo imetoa haki kwa mtu kukata rufaa kwa Mkurugenzi wa Vitambulisho dhidi ya Afisi ya usajili pindipo hakuridhia na mamuzi yanayotolewa  au kwa waziri kama pia hakuridhika na uamuzi wa Mkurugenzi.

Alisema suala la utoaji wa vitambulisho vya Mzanzibari limekuwa na mjadala mkubwa kutokana na baadhi ya wanasiasa na waheshimiwa kulalamikia juu ya baadhi ya wananchi wao kutopatiwa vitambulisho hivyo kwa sababu mbali mbali.

Alielezea imani yake kwamba waheshimiwa wawakilishi, wanasiasa na wananchi hawana sababu  ya kulalamikia  suala hilo ambalo lina utaratibu mzuri uliowekwa kwa  mujibu wa sheria.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitanabahisha kwamba suala zima la upatikanaji wa vitambulisho hivyo lisihusishwe na mambo ya kisiasa kwani utaratibu wa kisheria upo. Hivyo ni vyema na wajibu wa kila mwananchi kutumia sheria hiyo katika kutafuta haki yake.

Miswada Minne ya Sheria iliwasilishwa katika Mkutano huo wa 18 wa Baraza la Wawakilishi  na kujadiliwa na wajumbe wa Baraza  hilo ambayo ni Mswada wa sheria ya kuanzisha sheria ya kupunguza na kukabiliana na maafa Zanzibar na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Mwengine ni Mswada wa sheria ya kuanzisha Taasisi ya ulinzi ya Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar, Mswada wa sheria ya kufuta sheria ya usimamizi wa mazingira kwa ajili ya maendeleo endelevu nambari 2 ya mwaka 1996 na kuweka badala yake msharti bora ya kuhifadhi, kulinda na kusimamia mazingira pamoja na mswada wa sheria ya maadili ya Viongozi wa umma na kuanzisha Tume ya maadili ya Viongozi na mambo mengine yanayohusiana na hayo.

Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 11 Machi mwaka 2015 mnamo saa 3.000  za asubuhi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
30/1/2015.

BALOZI SEIF ALIFANYA ZIARA YA GHAFLA NDANI YA BANDARI YA MALINDI



 
 Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdullah Juma Abdullah akimtembeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif baadhi ya maeneo yaliyowekwa makontena ndani ya Bandari hiyo.





Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdullah Juma Abdullah kuchukuwa hatua ya kuyapeleka TRA Makontena yote yaliyoshindwa kufuata tataribu ambayo yanaleta msongamano ndani ya Bandari hiyo.



Mrundikano mkubwa wa makontena unaoonekana katika Bandari ya Malindi ambapo baadhi ya wafanyabiashara wanashindwa kutoa makontena yao na kuleta usumbufu kwa watendaji wa Bandari hiyo.

 Balozi Seif alifanya ziara ya ghafla ndani ya Bandari hiyo ili kujionea hali halisi ya utendaji wa bandari hiyo.

Picha na – OMPR – ZNZ. 




                                         Press Release:-


Mrundikano Mkubwa wa Makontena uliopo hivi sasa katika Bandari Kuu ya Malindi Mjini Zanzibar unaonyesha dalili ya kuzitia wasi wasi baadhi ya meli kubwa  za Kimataifa zinazopanga kuleta mizigo yake katika nchi za Mwambao wa Afrika Mashariki.

Uchelewaji wa baadhi ya wafanyabiashara kuchukuwa makontena yao Bandarini hapo ndio sababu kubwa inayochangia mrundikano huo usio wa lazima endapo taratibu za sheria ya kibiashara zitachukuliwa kwa wakati.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara ya ghafla katika Bandari ya Malindi kuangalia harakati za Bandari hiyo na kujionea msongamano mkubwa wa Makontena ya wafanyabiashara ambayo hadi sasa bado hayajachukuliwa wakati muda wa kukaa eneo hilo umepita.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla Juma Abdulla alimueleza Balozi Seif kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanasita kutoa makontena yao kwa wakati wakilitumia eneo hilo kama sehemu ya kuweka bidhaa zao wakiendelea kutafuta wateja wa bidhaa hizo.

Alisema tatizo hilo licha ya Uongozi wa Bandari kutoa matangazo ya kuwataka wafanyabiashara hao wakamilishe taratibu zinazowahusu lakini bado  utekelezaji wake unakuwa wa kusua sua.

Alisema Uongozi huo umekuwa ukiwasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania          { TRA } ili kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo ambalo limekuwa mzigo mkubwa kwa watendaji wa Bandari hiyo.


“ Zipo taratibu za kisheria zilizowekwa kwa wafanyabaishara wanaochelewa kutoa mizigo yao Bandarini ambayo huipa uwezo Mamlaka ya Mapato Tanzania kupiga mnada kwa biadhaa zilizoshindwa kufuata utaratibu “. Alisema Nd. Abdulla Juma Abdulla.


“ Sisi tunazo kanuni na taratibu zinazotupa Mamlaka ya kuwatoza  Dola kumi za Kimarekani kwa wafanyabiashara wanaochelewa kutoa Makontena yao katika muda waliopangiwa “. Alifafanua Nd. Abdulla.


Mkurugenzi Mkuu huyo wa Bandari Zanzibar alimfahamisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba lipo tatizo jengine la uhaba wa vifaa vya kazi  Bandarini hapo kutokana na ongezeko la mizigo inayoteremshwa pamoja na ufinyu wa nafasi za kuweka Makontena.

Nd. Abdullah alisema ipo nafasi ndani ya eneo la Bandari ambalo linaweza kusaidia kuweka Makontena yanayoteremshwa kwenye Bandari hiyo ambalo linaweza kusaidia kupunguza ufinyu wa maeneo ya maegesho ya Makontena.

 Alisema tatizo kubwa ni taratibu za Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kutoa kibali cha kuruhusu ujenzi katika eneo hilo ambalo limo ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliomo katika Hifadhi ya urithi wa Kimataifa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni { UNESCO }.

Akitoa shukrani zake kwa kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa na watendaji wa Shirika la Bandari Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Bandari kuyapeleka  Mamlaka ya Mapato Tanzania {TRA } Makontena yote yaliyoshindwa kukamilisha taratibu zilizowekwa.

Balozi Seif alisema Serikali imekuwa ikipokea lawama  na malalamiko siku hadi siku kutokana na harakati zilizopo Bandarini ambazo matatizo mengi husababishwa na watu wasiopenda kufuata taratibu zilizowekwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizishauri Mamlaka zilazohusika na kazi hiyo kuhakikisha kwamba sheria zote za biashara zinafuatwa na endapo yapo makontena yaliyoshindwa kulipiwa ushuru hatua za kupiga mnada zichukuliwe ndani ya siku 40 ili kurejesha gharama zinazotumiwa katika kazi hiyo.

MAMA ASHA SULEIMAN IDDI AKABIDHI TANURI LA KUHIFADHIA TAKA TAKA



 Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi akimkabidhi Tanuri la kuhifadhia taka taka Mkuu wa Kituo cha Afya Cha Kitope Dr. Ameir Yunus  Makame.



Mama Asha Suleima akizungumza na baadhi ya watendaji wa Kituo cha Afya cha Kitope mara baada ya kukabidhi Tanuri la kuhifadhia taka taka zinazokusanywa ndani ya Kituo hicho.

Tanuri la kuhifadhi taka taka zinazozalishwa katika Kituo cha Afya cha Kitope lililojengwa na kugharamiwa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali ili na kuungwa Mkono na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “ B”.

Picha na – OMPR – ZNZ.


                                    Press Release:-


Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi amewakumbusha Wafanyabiashara na Wananchi kuendelea kuwa na utamaduni wa kulipa kodi kwa wakati ili fedha zinazokusanywa na Halmashauri za Wilaya zao ziweze kuongeza nguvu katika kusaidia kuiendeleza miradi yao ya maendeleo.

Alisema nguvu za baadhi ya Halmashauri hapa Nchini zinakuwa ndogo kuunga mkono miradi ya Wananchi kutokana na baadhi ya wananchi hasa wafanyabiashara kukweka kulipa kodi kitendo ambacho pia kinakosesha mapato Serikali Kuu.

Mama Asha Suleiman Iddi alitoa kumbusho hilo wakati akikabidhi tanuri la kuchomea taka taka { Placentar Pits } katika Kituo cha Afya cha Kitope Kiliomo ndani ya Jimbo la Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Ujenzi wa Tanuri hilo uliogharamiwa na Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi na kuungwa mkono wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “ B “ulifuatia ziara aliyoifanya Kituoni hapo Tarehe 3 Machi Mwaka 2013 na kuelezwa changamoto zinazokikabili Kituo hicho.

Mama Asha alisema uwepo wa Tanuri hilo ambalo ilikuwa kilio cha muda mrefu kwa wafanyakazi wa Kituo hicho umelenga kuhifadhi mabaki ya taka taka zinazozalishwa kituoni hapo ambazo kuachiwa kwake zingeweza kusababisha maambukizo ya maradhi mbali mbali.

Alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa juhudi anazoendelea kuchukuwa katika kusaidia kuunga mkono miradi inayoanzishwa na Wananchi  ndani ya Jimbo hilo.

Aliwatahadharisha Wananchi wa Jimbo hilo kujiepusha na choko choko zinazoendelea kupenyezwa na baadhi ya watu ndani ya Jimbo hilo zikielezkezwa zaidi kwa vijana kwani kuachiwa kwake zinaweza kuviza maendeleo yaliyopatikana Jimboni humo.

Akitoa shukrani Mkuu wa Kituo hicho Dr. Ameir Yunus alisema changamoto ya ukosefu wa Tanuri hilo ilikuwa ikiwapa wakati mgumu wafanyakazi wa kituo hicho katika kukabiliana na taka taka zilizokuwa zikikusanywa ndani ya Kituo hicho.

Dr. Yunus alisema changamoto ya ukosefu wa Tanuri hilo ilikuwa ikiwapa wakati mgumu wafanyakazi wa Kituo hicho katika kukabiliana na taka taka zilizokuwa zikikusanywa ndani ya Kituo hicho.

Mkuu huyo wa Kituo cha Afya cha Kitope aliwaomba akina mama waja wazito wa Jimbo hilo na vitongoji vyake kukitumia kituo hicho katika kupata huduma za afya pamoja na zile za waja wazito ili wawe na uhakika wa kujifungua salama.

Dr. Yunus alifahamisha kwamba ule wakati wa akina mama kwenda kituoni hapo na Majembe kwa ajili ya kupata huduma za uzazi umekwisha kabisa baada ya kupatikana kwa Tanuri hilo.

Tarehe 3 Machi Mwaka 2013 Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi alifanya ziara ya kukikagua Kituo cha Afya cha Kitope na kutoridhika na mazingira aliyoyakuta ya Kituo hicho.

Aliwakumbusha wafanyakazi wa Kituo hicho kuzingatia usafi wa mazingira yanayokizunguuka kituo hicho ili kuepuka maradhi yanayoweza kuwakumba wagonjwa wanaofika kituoni hapo ambapo aliahidi kuwajengea Tanuri la kuhifadhia taka taka.




Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

29/1/2015.

 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link