Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akiwajulia hali
majeruhi wa ajali ya gari, Tunu Herman na Vanny Charles waliolazwa katika Hospitali ya
Rufaa Bugando kutokana na ajali ya gari iliyotokea jana katika Wilaya ya Busega mkoa wa
Simiyu ambapo wanahabari watano wamefariki katika ajali ya gari hiyo
Waziri Nape alipowajulia hali Majeruhi Hospitali ya Bugando
Immaculate Makilika na Prisca Ulomi, Mwanza
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amewajulia hali majeruhi wa ajali iliyotokea jana katika Wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu.
Waziri Nape alisema kuwa amefarijika kuona majeruhi wanaendelea vizuri mara baada ya kupata matibabu na hata sasa angalau wanaweza kuzungumza kidogo, majeruhi hao ni Tunu Herman na Vanny Charles ambao ni wanahabari.
"Nawapongeza madaktari wa hospitali ya Bugando na watumishi wote wa afya kwa kutoa matibabu mazuri kwa majeruhi hata sasa kama tulivyowaona angalau wanajitambua, pia nashukuru uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa jitihada mbalimbali walizofanya ili kusaidia majeruhi hawa waweze kupata msaada wa haraka" alisema Waziri Nape
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel alisema kuwa anamshuru Mhe. Waziri kwa kuwatembelea majeruhi na anawapongeza madaktari kwa kufanya jitihada za makusudi za kukoa maisha yao.
Aidha, ameendelea kuipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kununua vifaa vya kisasa ambavyo vimetumika katika kufanya uchunguzi wa majeruhi hao na hivyo imesaidia kutosafirisha majeruhi hao nje ya Mkoa au nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa Bugando Dkt. Fabian Massaga alisema kuwa hali ya majeruhi inaendelea vizuri , madaktari bingwa na matabibu wanaendelea kuwapatia huduma mbalimbali ili afya zao ziendelee kuimarika
Aidha, ametoa rai kwa wadau wa sekta ya usafiri kuweka mikakati ya kupunguza ajali za barabarani kwa kuwa ajali sio magonjwa yanayoambukiza hivyo zinaepukika.
Katika Hatua nyingine, Waziri Nape alihudhuria mazishi ya mmoja wa waandishi aliyezikwa leo Husna Milanzi ambapo katika mazishi hayo aliambatana na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza pamoja na wana habari