Mchumi apongeza VAT kwenye miamala ya benki
Written By CCMdijitali on Sunday, July 3, 2016 | July 03, 2016
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Idara ya Uchumi, Dk Haji Semboja
Source - Habari Leo
MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Idara ya Uchumi, Dk Haji Semboja amesema kodi iliyoibua mjadala katika jamii hivi sasa, ni chanzo kipya na kizuri cha mapato.
Lakini amesema serikali imechelewa kutoa ufafanuzi wa makato yake, ambao ungeondoa mkanganyiko unaotokea hivi sasa.
Kodi hizo ni zile zinazohusu Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) inayokatwa katika gharama ya huduma za mabenki, ambayo Mamlaka ya Mapato (TRA) imetaka isitozwe kwa mteja, huku Benki Kuu (BoT), ikisema mabenki yalikuwa sahihi, kutangaza kutoza kutoka kwa wateja.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Dk Semboja alishauri pande zote zinazovutana, zikutane na kuzungumza ili kuona jinsi ya kutelekeza ulipaji wa kodi hiyo, kwa sababu ni kodi muhimu kutoka chanzo kipya cha mapato.
Akifafanua kuhusu chanzo hicho kipya, Dk Semboja alisema katika nchi yoyote inayokua, lazima kuibuke vyanzo vipya vya mapato kutokana na shughuli za kijamii na kilichopaswa kufanyika kabla ya kuanza utekelezaji, ni tathmini ya athari katika kutoza kodi chanzo hicho.
“Baada ya kufanyika kwa tathmini hiyo na kwa kulinganisha na nchi nyingine, ingeonesha nani ni waathirika wa leo na baadaye na wangeweka kwenye maandishi nani anapaswa kulipa kodi hiyo kama ni mlaji au mtoa huduma,” alisema Dk Semboja.
Alishauri ni vyema kodi hiyo ikatozwa kwa kuweka makubaliano ya nani mhusika, kama ni kwa mgawanyo wa mlaji na mtoa huduma, ili kuondoka na malumbano yasiyo na tija. Nao wananchi waliotoa maoni yao iwapo wanafahamu kiasi kinachokatwa wanapofanya miamala ya kibenki, walisema hawafuatilii, ila kwenye huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi ndio wanafahamu.
“Sifuatilii makato kwenye benki, ila ninapotaka kutuma fedha kwa mtu kwa njia ya simu ya mkononi huwa nauliza kiasi ninachokatwa ili nijue,” alisema Michael Maleko mkazi wa Dar es Salaam. Ni mzigo?
Pamoja na maoni hayo ya Profesa Semboja na ya wananchi, gazeti hili pia limebaini kuwa hata madai kwamba kodi hiyo ya VAT katika mabenki na ya ushuru wa bidhaa, unaokatwa katika miamala ya fedha katika simu, si mzigo katika maisha ya Watanzania, kama inavyoelezwa na vyombo vya habari.
Tangu wakati wa kuwasilishwa kwa Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017, wakati wa mijadala bungeni na wiki hii baada ya kuanza kwa mwaka wa kwanza wa fedha wa Serikali ya Rais John Magufuli, vyombo vya habari vilishikilia baadhi ya kodi, na kudai zitaongeza mzigo katika gharama za maisha.
Miongoni mwa kodi hizo ni pamoja na VAT inayokatwa katika gharama za huduma za benki, ambayo ilitolewa mfano kuwa kama gharama ni Sh 1,000 ambayo ndiyo gharama halisi ya baadhi ya benki, asilimia 18 ndiyo itakwenda serikalini.
Takwimu
Gazeti hili katika kubaini kama kweli kodi hizo mbili ni mzigo, lilipitia takwimu za matumizi ya kipato cha Watanzania katika kugharamia maisha yao (Consumers Price Index), kuona kama gharama za huduma za mabenki na ada za miamala ya fedha katika simu, imekuwa ikichangia katika gharama za maisha ya Watanzania.
Gazeti hili lilibaini kuwa takwimu hizo zilizoko katika tovuti ya Ofisi ya Takwimu ya Taifa, zinaonesha kuwa gharama hizo ni sehemu ndogo tu ya matumizi ya Watanzania katika mahitaji yao kimaisha.
Chakula, usafiri
Ingawa gharama za benki na ada za miamala ya simu zimekuwa zikitozwa kabla hata ya Bajeti ya Serikali ya 2016/2017, takwimu hizo zinaonesha kuwa sehemu kubwa ya kipato cha Watanzania, asilimia 38.5 hutumika kugharamia chakula na vinywaji visivyo na kilevi, ambavyo havijatozwa kodi.
Huduma au bidhaa ya pili inayochukua sehemu kubwa ya kipato cha Watanzania, ambayo ikipanda ina mchango mkubwa katika kuongeza mzigo wa gharama za maisha yao ni usafiri na usafirishaji, ambao unachukua asilimia 12 ya kipato chao.
Katika kuhakikisha kuwa usafirishaji na usafiri hauendelei kuwa mzigo katika maisha ya Watanzania, Serikali ya Awamu ya Tano, katika Bajeti yake ya kwanza, ilikwepa kuongeza kodi au tozo ya aina yoyote katika mafuta.
Hata wabunge walipotaka kila lita moja ya mafuta ya petroli ikatwe Sh 50, kwa kuwa yameshuka bei kwa asilimia 20, ili fedha hiyo ikatunishe Mfuko wa Maji na kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya na zahanati vijijini, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, alipinga.
Katika utetezi wa kupinga kuongezwa Sh 50 katika mafuta hayo, Mpango alisema kushuka kwa bei ya mafuta, kumeleta ahueni kwa wananchi wengi, hivyo serikali imeamua kutoongeza tozo kwenye mafuta, ili wananchi waendelee kunufaika na unafuu huo wa bei ya mafuta.
“Ni dhahiri kuwa ongezeko la tozo katika mafuta ya petroli na dizeli litasababisha kupanda kwa bei ya mafuta nchini, jambo litakaloongeza gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa chakula na bidhaa kama vifaa vya ujenzi na huduma nyingine,” alisema Dk Mpango, alipokuwa akitetea msimamo wa serikali kutoongeza gharama katika maisha ya wananchi.
Nyumba, maji, nishati
Takwimu hizo za Mei mwaka huu, zimeonesha kuwa huduma na au bidhaa zinazoshika nafasi ya tatu kwa kuchukua sehemu kubwa ya kipato cha Watanzania, ni gharama za nyumba kwa maana ya kodi, maji, umeme, gesi na nishati nyingine inayotumika katika makazi ya watu, ambazo kwa ujumla wake zinachukua asilimia 11.6 ya kipato cha Watanzania.
Katika huduma hizo, hakuna kodi iliyoongezwa ukiacha kodi katika kodi za pango na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa kodi za majengo, badala yake huduma kama umeme ambayo ilishuka bei kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu, serikali imetenga fedha nyingi kuisambaza kwa wananchi wengi zaidi ili wanufaike.
Mavazi, mawasiliano
Huduma na au bidhaa zingine zinazogharimu maisha ya Watanzania kwa mujibu wa takwimu hizo, ni mavazi na viatu vinavyochukua asilimia 8.3 ya kipato cha Watanzania. Pamoja na kodi katika mitumba inayotajwa kuvaliwa na watu wengi kuongezwa kodi, lakini haikuchukuliwa na vyombo vya habari kuwa mzigo kwa wananchi kama ilivyochukuliwa kwa gharama za huduma za benki na za kuhamisha miamala ya fedha kwa kutumia simu.
Huduma za mawasiliano, bila kufafanuliwa kama zinahusu pia huduma za uhamishaji wa miamala kwa njia ya simu, lakini kwa hakika hazihusishi gharama za huduma za benki, zimeshika nafasi ya tano kwa kuchukua asilimia 5.6 tu ya kipato ya Watanzania.
Sigara, vilevi vingine
Huduma zingine zinazochukua chini ya asilimia tano ya kipato cha Watanzania na asilimia yake katika mabano ni pamoja na huduma za migahawa na hoteli (asilimia 4.2) na huduma za vilevi na sigara, ambazo karibu kala bajeti, zimekuwa zikiongezwa kodi, lakini huchukua asilimia 3.7 tu ya kipato cha Watanzania.
Huduma na bidhaa zingine ambazo kutokana na kuchukua chini ya asilimia 1.5 ya kipato cha Watanzania, zimewekwa pamoja na kupewa jina la huduma na bidhaa mbalimbali, ambazo huenda ndiko ziliko gharama za mabenki, kwa ujumla wake zimetajwa kuchukua asilimia 3.1 tu ya kipato cha Watanzania.
Takwimu hizo zimeonesha kuwa huduma za afya, hugharimu asilimia 2.9 ya kipato cha Watanzania, starehe na masuala ya utamaduni asilimia 1.6 ya kipato huku gharama za elimu, ambayo kwa sasa inatolewa bure kutoka darasa la awali mpaka kidato cha nne, ikichukua asilimia 1.5 tu ya kipato cha Watanzania walio wengi. Imeandikwa na Joseph Lugendo na Ikunda Erick
Labels:
BIASHARA