Home » » Wasomi watabiri anguko la Chadema, Ukawa

Wasomi watabiri anguko la Chadema, Ukawa

Written By CCMdijitali on Tuesday, August 4, 2015 | August 04, 2015


Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo


SIKU moja baada ya Mwenyekiti wa Taifa ya Chadema, Freeman Mbowe kukiri kupumzika kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Willbrod Slaa, wasomi na wanachama wa chama hicho, wamedai kuwa huo ni mwanzo wa kupasuka kwa chama hicho na kusambaratika kwa umoja wa vyama vinne vya upinzani vinavyounda Ukawa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Aidha, wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) wameushutumu uongozi wa chama hicho, kubariki kujivua uanachama wa CUF na kujiunga na Chadema kwa Juma Duni Haji, Makamu Mwenyekiti wa CUF ambaye jana alitangazwa kuwa mgombea mwenza wa Edward Lowassa wa Chadema.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa nchini nao wamelaumu utaratibu uliotumika katika kupiga kura za kuwapitisha wagombea wa Chadema, Edward Lowassa na Juma Duni Haji, jana kuwa haukufuata taratibu za uchaguzi, badala yake wajumbe wa mkutano mkuu wamelazimishwa kupiga kura za wazi kwa hofu ya mkutano huo kumkataa Lowassa, kwani hapo awali uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema ulishaamua Dk Slaa awe mgombea urais, kabla ya ujio wa Lowassa.

Wakizungumza jana, baadhi ya makada wa Chadema walisema utaratibu wa upigaji kura, ungefanywa kwa siri ili kupata matokeo mazuri kuliko mtindo aliouanzisha wa kupiga kura kwa kuinua mikono juu.

Hata hivyo, wanachama hao walikwenda mbali zaidi na kusema suala la kupumzika kwa Dk Slaa katika kipindi hiki ni maumivu kwao na kwamba kama suala lake litaendelea kugubikwa na sintofahamu ni wazi kuwa watakihama chama hicho na hawatakiunga mkono katika uchaguzi mkuu ujao.

“Kama utaratibu wa kuheshimu mawazo ya wachache utaendelea ndani ya chama ni wazi kuwa kutatokea mpasuko mkubwa ambao haujategemewa kwa sababu bado hatujasahau kufukuzwa kwa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe na wanachama wengine sasa leo wanamfukuza Dk Slaa kwa kupinga uamuzi wao wa kuwakaribisha kina Lowassa,” alisema Muhidin Mcharo, mkazi wa Kawe.

Kwa upande wa CUF, baadhi ya wanachama wamepingana na uamuzi wa Duni kujiunga Chadema na kudai kuwa makubaliano ya Ukawa ni ya mdomoni, kwani hakuna nyaraka zozote za kisheria zinazothibitisha wameungana, hivyo hata kama Chadema itaingia Ikulu uwezekano wa kusaliti vyama vingine ni mkubwa, kwani wameshaonesha mfano kwa kuwafukuza akina Zitto.

Pia, waliwalalamikia Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Sharrif Hamad kwa kumkubalia Duni kwenda Chadema, wakisema uamuzi huo una maslahi kwa wachache.

“Sisi tunajua Chadema ni wabinafsi na ushahidi upo sasa sisi kama wanachama tutafanya maamuzi yetu ikifika Oktoba 25 mwaka huu maana vyama hivi vimeshindwa kuleta mageuzi “alisema Omari Shekinyashi, mkazi wa Buguruni, yaliko makao makuu ya chama hicho.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo alisema utaratibu wa upigaji kura, uliooneshwa jana ni wazi ni mwendelezo wa muda mrefu wa Chadema kubana demokrasia linapokuja suala la uchaguzi.

Alisema kitendo cha kuwapitisha Lowassa na Duni Haji ilikuwa ni uamuzi wa wachache, hivyo mkutano mkuu ulitumika kama mbwembwe ya kufikia malengo ya wachache ndani ya chama hicho, kwani tayari uamuzi ulishafanyika.

Aliongeza kuwa hata chama tawala, CCM kinapoteua jina la mgombea kinapeleka mapendekezo ya majina matatu kwenye mkutano mkuu na kupigiwa kura za siri, tofauti na walivyofanya Chadema.

Kuhusu kujiengua kwa Dk Slaa, Mkumbo alisema hilo lilishajulikana tangu awali baada ya Lowassa kujiunga Chadema, lakini hilo lilifichwa hadi juzi walipotumia lugha ya kidiplomasia kuwa anapumzika, lengo likiwa kuficha hali halisi ya `mtikisiko’ ndani ya chama hicho.

Mkuu wa Idara ya Siasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alisema uamuzi wa Chadema kupokea wanachama walioenguliwa CCM ni kujishushia heshima, kwani tayari walishaweka msimamo kuwa hawawezi kupokea mabaki kutoka CCM.

Alisema ni wazi uko uwezekano wa kutokea mpasuko mkubwa miongoni mwa wanachama wa chama hicho kutokana na kutoridhishwa na mfumo wa maamuzi ya vikao.

Imeandikwa na Mwandishi Wetu - HABARI LEO.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link