Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba amelipongeza Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa kuwakamata watuhumiwa 20 kati ya 24 ambao wanahusishwa na matukio ya kuingiza bidhaa za magendo kutoka visiwani Zanzibar kwa njia ya majahazi katika Wilaya ya Mkinga zenye thamani ya Sh bilioni 1.2.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukamatwa kwa magendo hayo kwa awamu mbili ambapo Septemba 8 mwaka huu jahazi lililokuwa limebeba balo 170 zenye doti 17,000 za vitenge vikiwa na thamani ya zaidi ya Sh milioni 500 na Septemba 11 mwaka huu yalikamatwa magari mawili aina ya fuso yaliyokuwa yamebeba mabalo 180 huku yakiwa yamewekewa mawe (Tanga Stone) kwa juu.
Aidha, watuhumiwa hao waliomba msamaha ili jeshi la polisi liwaachie huru wakidai hawahusiki na mzigo huo na wao ni wafanyakazi tu katika magari na majahazi yaliyokutwa na mzigo huo wa magendo.
Akizungumza katika Kituo cha Polisi cha Mtandikeni wilayani Mkinga ambako watuhumiwa hao wanashikiliwa, Mheshimiwa Mgumba pia amelitaka jeshi hilo kuwakamata watuhumiwa wengine wanne ambao waliachiwa kinyume cha utaratibu na Afisa Upelelezi wilayani humo.
“Nina Imani kubwa na jeshi la polisi kama mmeweza kuwakamata hawa wote 15 hamtashindwa kuwakamata hao wanne,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi mkoani Tanga kutoshiriki au kufanya kazi yoyote ambayo si halali kwa sababu ukishiriki katika vitendo vya wizi na wewe ni mwizi.
“Niwaombe ndugu zangu mkoani Tanga, asikupe mtu yeyote kazi ambayo si halali kwa sababu ukishiriki kwenye biashara ya magendo na wewe unafanya biashara ya magendo, ukishiriki kusafirisha binadamu na wewe unahusika, nawataka mfanye kazi halali kwa maendeleo ya taifa letu.
“Kwenye hili tutaendelea kuchukua hatua na hatutamuonea wala kumpendelea mtu haki itatendeka kwa kila anayestahili mwenye kosa kwa mujibu wa uchunguzi sharia itafuata mkondo wake,” amesema RC Mgumba.