NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS (TAMISEMI),SELEMAN SAID JAFFO |
SERIKALI imesisitiza kuwa haitasita kuwachukulia hatua askari Mgambo watakaobainika kujihusisha na vitendo vya unyanyasaji wa mama lishe na wafanyabiashara wengine, ikielezwa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria.
Aidha,imeshauri wafanyabiashara kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyotengwa rasmi na Halmashauri ili kuepuka misuguano na mamlaka husika.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo ametoa msimamo huo leo bungeni mjini Dodoma wakati anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Vullu (CCM), aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kuwaandalia mama lishe mazingira bora ya biashara, ili waepuke manyanyaso ya askari wa Mgambo katika majiji yote nchini.
Katika swali lake, alisema zaidi ya asilimia 30 ya wakazi wa mijini hupata chakula chao cha asubuhi, mchana na hata jioni kwa mama lishe, lakini watoa huduma hao muhimu hujikuta wakinyanyaswa kila kukicha.
Jafo alisema, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wafanyabiashara wadogo waliopo katika sekta hiyo isiyo rasmi katika kukuza kipato na ajira.
“Kwa kuzingatia umuhimu huo, halmashauri zote zimeagizwa kuhakikisha zinatenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara ndogo, wakiwemo mama lishe karibu na maeneo walipo wateja. Akizungumzia unyanyasaji wa mgambo, alisema wanachokifanya ni kinyume cha Sheria ya Polisi Wasaidizi ya Mwaka 1969 inayowazuia kuwapiga, kuchukua au kuharibu bidhaa au mali za wananchi.
Alisisitiza kuwa, askari Mgambo, kama ilivyo kwa watumishi wengine, wanatakiwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu bila manyanyaso wala dhuluma wakati wanapowaondoa wafanyabiashara katika maeneo yasiyoruhusiwa.