Home » » Sheria uhalali wa mtoto yaja

Sheria uhalali wa mtoto yaja

Written By CCMdijitali on Saturday, September 10, 2016 | September 10, 2016

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
Imeandikwa na Angela Semaya, Dodoma | Habari Leo

SERIKALI imewasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa Mwaka 2016, ambao pamoja na mambo mengine utaiwezesha maabara hiyo kufanya uchunguzi unaohusisha matumizi ya teknolojia ya vinasaba, ikiwamo uhalali wa mzazi kwa mtoto.

Aidha, sheria inayokusudiwa itaipa mamlaka maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuwa maabara ya rufaa na msemaji wa mwisho wa serikali katika shughuli za uchunguzi wa kimaabara wa kikemia, sayansi, jinai na vinasaba.

Iwapo muswada huo wa sheria utapitishwa, pia utaiwezesha maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya uchunguzi unaohusisha matumizi ya teknolojia ya vinasaba, mfano uhalali wa mzazi kwa mtoto, utambuzi wa binadamu wakati wa majanga, utambuzi wa jinsi tawala ya binadamu na watu wanaosafiri kwa makundi.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akiwasilisha muswada huo wa sheria, alisema pia utaiwezesha maabara hiyo kufanya uchunguzi wa sampuli zinazotajwa kwenye sheria mbalimbali kama vile vyakula, dawa, mazingira, maji na majitaka, afya mahali pa kazi, usalama barabarani na utumiaji wa dawa za kulevya.

Ummy alisema kupitia muswada huo wa sheria itaanzishwa kanzidata ya Taifa ya vinasaba vya binadamu na kuwa utawekwa utaratibu wa upatikanaji wa taarifa zinazohifadhiwa kwenye Kanzidata ya Vinasaba vya Binadamu.

Alisema kitaanzishwa pia Kituo cha Taifa cha Udhibiti Matukio ya Sumu kitakachokuwa kinatoa taarifa kwa umma, kufanya uchunguzi wa kimaabara, utambuzi na tiba ya matukio ya sumu, utafiti na mafunzo.

Alisema kitakuwepo kifungu maalumu chini ya mamlaka ya maabara hiyo kitakachogharimiwa na serikali kwa ajili ya uchunguzi wa vielelezo vya makosa ya jinai, majanga na masuala mengine yenye maslahi ya taifa ili kuwezesha utekelezaji wa jukumu hilo kwa ufanisi na kusaidia utoaji haki katika vyombo vya maamuzi na kuleta utengamano katika jamii.

Kwa mujibu wa Ummy, chini ya sheria hiyo maabara husika itasimamia na kudhibiti sampuli, matokeo ya uchunguzi pamoja na kuweka utaratibu wa utoaji ripoti za uchunguzi wa kimaabara na matumizi yake.

Alilifahamisha Bunge kuwa sheria iliyopendekezwa kutungwa haitafuta wala kurekebisha sheria nyingine yoyote ila itaongeza ufanisi katika utekelezaji wa sheria zilizopo na kutatua changamoto ambazo maabara imekuwa ikikumbana nazo kutokana na majukumu hayo kubainishwa katika sheria yake pia.

Akiwasilisha maoni na ushauri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu muswada huo, Mbunge wa Kigamboni, Faustine Ndugulile (CCM) kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba alisema kamati hiyo ilishauri maabara kufanya uchunguzi wa kina wa matumizi ya shisha ili kubaini athari zake na kuishauri hatua za kuchukua kukabiliana na madhara hayo.

Alisema kamati imebaini matumizi ya shisha yamekuwa na madhara makubwa kwa watu wanaotumia nchini, hasa vijana na kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakichanganya shisha na dawa za kulevya ambayo ni hatari zaidi sio kwa afya tu, lakini pia kwa uchumi wa taifa.

Kamati hiyo pia ilishauri maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kufanya uchunguzi wa kemikali zinazotumika kuua vijidudu kwenye maji ili zisilete madhara kwa watumiaji. Kwa mujibu wa kamati hiyo, pamoja na nia nzuri ya kuweka dawa kwa ajili ya kuua vijidudu kwenye maji kwa ajili ya matumizi ya majumbani, lakini kuna wakati dawa hizo zimekuwa kali na hivyo kuhofiwa kuleta madhara.

Kamati hiyo pia ilisema watu wengi bado hawafahamu kwa kina kazi zinazofanywa na maabara ya mkemia mkuu wa serikali, hivyo kupendekeza wakala uanze kutangaza kazi zake, lakini pia itoe elimu kwa wananchi juu ya madhara ya kemikali kwa mfano sehemu zenye madini ya urani.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link