Home » » Majaliwa aahidi umeme, kituo cha polisi sokoni Arusha

Majaliwa aahidi umeme, kituo cha polisi sokoni Arusha

Written By CCMdijitali on Saturday, December 17, 2016 | December 17, 2016

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa eneo la Kwamrombo wilayani Arusha ambao   walijipanga kwa wingi barabarani na kumshawishi kusimama  ili kuzungumza nao. Alikuwa katika ziara ya mkoa wa Arusha  Desemba 17, 2016.

 Imeandikwa na Veronica Mheta - Habari Leo
 


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewatoa hofu wafanyabiashara katika Soko la Kwa Mrombo mjini hapa, akisema watapelekewa umeme ndani ya soko hilo sambamba na ujenzi wa kituo cha polisi kwenye eneo hilo.

Majaliwa aliyasema hayo jijini hapa wakati aliposimamishwa na wananchi wa eneo hilo kueleza kero mbalimbali walizokuwa nazo.


Akitoa kero za wananchi wenzake mmoja kati ya wafanyabiashara hao, Regina Makorongo alisema wafanyabiashara wanaouza bidhaa katika soko hilo la Kwa Mrombo wanalazimika kuvamia eneo la barabarani kwa sababu soko hilo halina umeme wala maji ya uhakika.

Alisema pia eneo hilo halina shule ya sekondari na pia za msingi ni chache hali inayosababisha watoto kutembea umbali mrefu kwenda kusoma kwenye kata nyingine.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu tusaidie baba hapa hatuna shule wala umeme sokoni. Barabara za mitaani pia hazipitiki, lakini pia hatuna kituo cha polisi tunalazimika kwenda Mbauda kupeleka malalamiko yetu, tunaomba utusaidie,” alisema Makorongo.


Baada ya kusikiliza kero hizo, Waziri Mkuu aliahidi umeme kufikishwa sokoni hapo na kumwagiza Meneja wa Shirika la Umeme (Tanesco) Mkoa wa Arusha, Gaspar Msigwa kutekeleza agizo hilo mara moja. Alisema pamoja na soko hilo, pia maeneo yote ya Kwamrombo yawekwe umeme, kwani serikali ilishatenga fedha kwa ajili ya umeme maeneo ya vijijini.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alisema hivi sasa eneo la Kwamrombo kunajengwa kituo cha polisi cha kisasa pamoja na kusambaza umeme katika eneo hilo. Kuhusu maji, alisema tayari wamepata chanzo cha maji wilayani Arumeru kitakachosaidia upatikanaji wa maji ya uhakika.






Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa eneo la Kwamrombo wilayani Arusha ambao   walijipanga kwa wingi barabarani na kumshawishi kusimama  ili kuzungumza nao. Alikuwa katika ziara ya mkoa wa Arusha  Desemba 17, 2016.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link