Home » » Mawaziri 11 wakutana Dar kutokomeza ukatili wa kijinsia

Mawaziri 11 wakutana Dar kutokomeza ukatili wa kijinsia

Written By CCMdijitali on Tuesday, December 13, 2016 | December 13, 2016


 Imeandikwa na Katuma Masamba     - Habari Leo

KWA mara ya kwanza mawaziri 11 wamekutana kwa ajili ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia, huku Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikiweka wazi mpango wake wa kuanzisha madawati ya kuwalinda watoto katika shule za msingi na sekondari.

Aidha, ina mpango wa kuanzisha kamati za ulinzi na usalama wa mtoto katika kila mtaa na kijiji nchi nzima, lengo likiwa ni kutokomeza vitendo vya ukatili na unyanyasaji kwa watoto.

Mawaziri hao walikutana jana katika uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto wa miaka mitano 2017/18 hadi 2021/22 uliofanyika jijini Dar es Salaam.


Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hatua hiyo inatokana na kuwepo vitendo vya ubakaji pamoja na vitendo vya watoto wa kiume kulawitiana.

Aliongeza kuwa licha ya kuwepo walimu wa nidhamu lakini wamekuwa wakiogopwa hivyo madawati hayo yatakuwa ni rafiki pindi mtoto anapokutana na vitendo hivyo anakimbilia katika dawati hilo.

Alifafanua kuwa kamati za ulinzi na usalama wa mtoto kwa kila mtaa na kijiji pamoja na kuanzisha mtandao wa wanaume katika kila kata ambao watakuwa wakitetea na kulinda vitendo vya ukatili.

“Ukatili mashuleni tunazungumzia ubakaji wa wakubwa, kinachosikitisha watoto wa kiume wanalawitiana katika mazingira ya shule, sisi kama wizara tumeona tuanzishe dawati la kuwalinda watoto katika shule zetu zote za msingi na sekondari,” alisema.


Akizungumza kwenye mkutano huo, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Alvaro Rodriguez alisema dhamira ya serikali imechangia katika kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika chini ya mpango mpya wa ushirikiano wa kimataifa katika kukomesha ukatili dhidi ya watoto.

Rodriguez alisema malengo ya dunia yanataka kumaliza vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto na badala yake kuwekeza katika kuwawezesha na kuwalinda.

Alisema UN itaendelea kushirikiana na serikali katika kuzuia ukatili wa aina yoyote kwa wanawake na watoto.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliagiza wizara, taasisi za serikali, mikoa, wilaya pamoja na mamlaka za mitaa, kuhakikisha zinazingatia mpango kazi huo kwa kutenga fedha katika bajeti zao kuanzia mwaka wa fedha 2017/18 ili kukidhi utekelezaji wa mpango huo.

Alisema utekelezaji wa mpango huo utagharimu Sh bilioni 267.4 kwa miaka mitano, ambapo unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.

Kwa upande wake, waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Jenista Mhagama alisema mpango huo ni muhimu kwa taifa hasa kwa wakati huu, kwa kuwa vitendo vya unyanyasaji vimekuwa vikiongezeka.

Alisema imefika mahali ambapo vitendo hivyo vinatakiwa vikome na kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu itasimamia mpango kazi huo ili kuhakikisha unatekelezeka na kuendana na gharama halisi ili kufikia malengo.

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe alisema serikali inataka kupitia sheria ya mtoto ya mwaka 2009 ili kubaini mapungufu ambyo wadau wameyaona na kuyafanyia marekebisho.

Alisema pia wanaangalia namna ya kupanua wigo wa fursa kwa wanawake na watoto katika kutafuta haki na hatua mojawapo ya kufanikisha suala hilo ni kuanzisha mfumo wa msaada wa kisheria kwa wananchi wasio na uwezo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya alisema kuwa katika kutekeleza mpango huo, wizara hiyo itahakikisha inasimamia ipasavyo katika maeoneo yote inayohusika.

Naye Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani alisema, lengo la serikali ni kuhakikisha wanapeleka umeme katika vijiji vyote kupitia REA awamu ya tatu hasa katika zahanati ili kuwasaidia akinamama kujifungua katika mazingira salama.

Aidha, pia alisema shule nyingi zinaungua kutokana na matumizi ya vibatari hivyo wamekusudia kufikisha umeme katika shule zote. Dk Kalemani pia aliwaonya wamiliki wa migodi ambao wamekuwa hawawashirikishi wanawake katika shughuli za kiuchumi.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura alisema wizara yake itatumia idara za sanaa na utamaduni ili kuhakikisha wanatokomeza vitendo vya ukatili.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi alimwakilisha waziri wa wizara hiyo, Mwigulu Nchemba alisema matukio ya ukatili yamekuwa ni mengi, na kuahidi kuwa wizara itaendelea kuhakikisha wanatumiwa wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Mawaziri wengine waliozungumza katika mkutano huo ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage. Wizara nyingine zinazoshiriki ni Ofisi ya Rais, TAMISEMI.





 Waziri wa Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akizungumza katika uzinduzi Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na Watoto 2017 - 2022 leo jijini Dar es Salaam.


 Waziri wa Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akikata utepe kuashiria katika uzinduzi Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na Watoto 2017 - 2022, leo jijini Dar es Salaam.



Sehemu ya wadau waliohudhuria uzinduzi wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya wanawake na Watoto 2017 - 2022, leo jijini Dar es Salaam.


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link