Home » » Taifa Stars yarejea nchini na matarajio mapya

Taifa Stars yarejea nchini na matarajio mapya

Written By CCMdijitali on Monday, September 9, 2013 | September 09, 2013


Wachezaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) wamerejea nyumbani baada ya mechi yao na Gambia ambapo walifungwa 2-0 huku matarajio yote sasa yakiwa ni kufuzu kucheza Kombe la Afrika 2015.

Wachezaji hao 18 pamoja na benchi la ufundi waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere saa nane mchana kwa ndege la shirika la Kenya.

Hii ni mechi ambayo Taifa Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, ilitakiwa kushinda lakini ilikosa wachezaji tisa muhimu ambapo baadhi yao hawakuruhusiwa na vilabu vyao na wengine walikuwa majeruhi.

Akizungumza baada ya kuwasili kocha Kim Poulsen alisema kuutkana na hali halisi alilazimika kuwachezesha wachezaji vijana ambao uzoefu wao sio mkubwa sana kama ule wa wachezaji wa kawaida ambao mara nyingi huwa wanaanza.

“Tumesikitishwa na matokeo haya lakini kama nilivyosema Gambia waliita wachezaji wao wote wanaocheza nje lakini sisi tulikosa timu karibu nzima….vijana waliocheza walijitahidi lakini wenzetu waliwazidi uzoefu,” alisema.

Alisema ni muhimu watanzania watambue kuwa mechi za kufuzu kucheza kombe la dunia zimekuwa muhimu sana kwa Tanzania kwani wachezaji wengi wametambulika na wameitwa nje. “Kuna wachezaji kama Shomari kapombe, Mwinyi Kazimoto, ambao kutokana na mechi hizi wamepata nafasi ya kwenda kucheza nje,” alisema.

Kocha huyo alisema yuko makini sana kutekeleza mpango wa muda mrefu ambao ni kuhakikisha Tanzania inafuzu kucheza Kombe la Afrika 2015,” alisema na kuongeza kuwa timu anayoendelea kujenga itafanya kazi hiyo.

Alisisitiza kuwa ni lazima TFF ihakikishe wachezaji wote muhimu wanakuwepo wakati mechi za kufuzu kucheza Kombe la Afrika zitakapoanza mwakani.

“Kwa sasa wachezaji watarudi vilabuni kwao na baada ya muda mfupinitawaita tena ili tujiandae na Mashindano ya CECAFA Senior Challenge yatakayofanyika Nairobi,” alisema.

Aliwataka watanzania wawe na subira kwani ana imani na timu anayoijenga.

Akiunga mkono maneno ya Poulsen, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe, ambaye bia yake inadhamini Taifa Stars, alisema ni lazima nguvu zote zielekezwe katika AFCON 2015.

“Tungefurahi kama tungefuzu kucheza Kombe la Dunia lakini ni mapema sana kwa timu yetu ambayo bado inajengwa…tumpe kocha nafasi aweze kutimiza haya malengo na sio kumkatisha tama,” alisema.

Alisema wao kama wadhamini wanafarajika na mabadiliko mbalimbali yaliyofanyika katika Timu ya Taifa tangu waanze kuidhamini Timu hiyo mwezi Mei mwaka uliopita.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link