Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akikagua Daraja la Mto Mkundi mkoani Morogoro linalokarabatiwa baada ya kuharibiwa na mafuriko hivi karibuni.Rais Kikwete alitembelea eneo hilo na sehemu nyingine zilizokumbwa na mafuriko hayo kujionea uharibifu. Picha na Freddy Maro wa Ikulu.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi la Ulinzi na
Usalama, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameliamuru Jeshi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) kuanza mara moja kazi ya kusimamia utoaji huduma kwa watu
walioathiriwa na mafuriko katika Mkoa wa Morogoro, ikiwa ni pamoja na kusimamia
ujenzi wa nyumba za muda wa wahanga hao.
Rais
pia ameliamuru Jeshi kupeleka mashine za kusafisha maji katika makambi ambako
wahanga hao wa mafuriko ya Januari 22, mwaka huu wanaishi kwa muda.
Aidha,
Rais Kikwete amewahakikishia wahanga wa mafuriko hayo kuwa Serikali
itahakikisha inawapatia huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na chakula,
malazi, maji na huduma za afya hadi hapo watakapokuwa na uwezo wa kuanza
kujitegemea tena.
Rais
Kikwete ametoa amri hizo kwa Jeshi leo, Januari 27, 2014, wakati alipotembelea
kambi za wahanga wa mafuriko hayo kuwajulia hali walioathirika katika makambi
yaliyoko Shule ya Sekondari ya Magole katika eneo la Dumila na katika Kijiji
cha Mateteni kilichoko Dakawa, Wilaya ya Kilosa.
Katika
hotuba zake fupi baada ya kuwa ametembelea na kuona mahema ambamo wahanga hao
wanalala, Rais Kikwete amesema ameagiza
Jeshi kuongoza harakati za kuwahudumia wahanga hao kwa sababu zikifuatwa
taratibu za kawaida za Kiserikali huduma zitachelewa sana kuwafia waathirika.
“Kazi
yetu ni kusimamia maisha ya watu hasa
kipindi cha shida za namna hii. Tukifuata taratibu za kawaida za
Kiserikali za tenda tutachelewesha sana huduma za dharura kwa waathirika. Ndiyo
maana nimeliamuru Jeshi kufanya kazi hii ikiwa ni pamoja na kujenga haraka
makazi ya muda wa waathirika,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Katika
mazungumzo hayo na Mkuu wa Majeshi, nimemwagiza pia kuleta mashine za kusafishia
maji ili kuhakikisha kuwa watu wanakunywa maji salama kwa sababu katika hali ya
sasa maji yasiyokuwa salama yanaweza kuwa chanzo cha magonjwa.”
Kuhusu
upatikanaji wa chakula cha msaada kwa wahanga, Rais Kikwete amesema kuwa
Serikali inacho chakula cha kutosha kwa ajili yao. “Tunacho chakula cha kutosha
na hata kile tusichokuwa nacho tutanunua. Tutabanana ndani ya Serikali ili
tupate fedha za kutosha za kuwahudumia.”
Kuhusu
malazi, Rais amesema:”Naambiwa kuna upungufu wa magodoro. Tutahakikisha kuwa
yanapatikana na yatafika katika siku mbili zijazo. Hatutaki watu walale chini
na waje kupata vichomi.”
Kuhusu
maji, Rais Kikwete amesema kuwa Serikali itaendelea kutoa huduma ya maji bure
kwa wahanga. “Tutaendelea kutoa bure huduma hii mpaka hapo huduma ya kawaida ya
maji itakapoanza kupatikana tena.”
Kuhusu
huduma za afya, Rais amesema kuwa anafurahi kuwa kila kambi ya wahanga inayo
huduma ya afya ambayo itaendelea kutolewa kwa kadri watu wanavyozidi kuishi
kwenye makambi.
Rais
ameagiza kuwa baada ya muda mfupi viongozi wa Mkoa wa Morogoro na wilaya husika
wakae chini ya viongozi wa ngazi za chini na wahanga kujadili na kutafuta
mwafaka kuhusu maisha ya baadaye ya wahanga – hasa kuhusu namna gani wanaweza
kupatiwa maeneo yaliyoko nje ya mikondo ya mafuriko.
“Hili
ni lazima kwa sababu hata kama imechukua miaka mingi kwa mafuriko ya sasa
kutokea ni dhahiri kuwa iko siku yatakuja tena – inaweza kuwa hata mwaka huu
kwa sababu zipo mvua za masika. Kwa hiyo ni lazima tukubaliane jinsi gani ya
kurudi ama kutokurudi katika maeneo yetu tulikotoka.”