Home » » Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la Barabara ya ndani ya Kilomita 3.5

Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la Barabara ya ndani ya Kilomita 3.5

Written By CCMdijitali on Monday, July 27, 2015 | July 27, 2015

 Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Wananchi wa Jimbo la Mpendae wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bara bara ya ndani kutoka Mtaa wa Mombasa kwa Mchina hadi Skuli ya Sekondari ya Jang’ombe.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la Barabara ya ndani ya Kilomita 3.5 iliyoanzia soko la mboga mboga Mtaa wa Mombasa hadi Skuli ya Sekondari ya Jang’ombe inayojengwa na Uongozi wa Jimbo la Mpendae.

Nyuma ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Mindombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Issa Haji Gavu na Kushoto ya Balozi Seif ni Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae anayemaliza muda Mh. Moh’d Said Dimwa.
 Wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Mpendae wakimpongeza Mbunge wao Mh. Salim Hassan Turky mwenye kanzu nyeupe kati kati yao kwa uamuzi wake wa kuwapatia zawadi ya Bara bara ya ndani inayojengwa kwa kiwango cha lami kutoka Mtaa wa Mombasa hadi Jang’ombe.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpongeza Mbunge wa Jimbo la Mpendae Mh. Salim Hassan Turky kwa kusimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya Jimbo lake kwa asilimia 97%.
Picha na – OMPR – ZNZ.

 Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewatahadharisha wananchi na wafuasi wa Vyama vya Siasa kuwa makini katika kuwachaguwa Viongozi watakaokubali kwa dhati kuwasimamia katika kupambana na changamoto zinazowazunguuka kwenye maeneo yao.

Alisema wakati wa kukumbatia watu wanaojali maslahi yao binafsi kwa kukumbuka shida za Wananchi wakati wa kuomba kura pekee kwa sasa umekwisha na unapaswa kuepukwa kwa nguvu zote.

Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati alipokuwa akizungumza na Wananchi pamoja na Viongozi wa Jimbo la Mpendae baada ya kuweka jiwe la msingi la Bara bara ya ndani iliyoanzia Soko la Mboga mboga kwa Mchina hadi kumalizikia skuli ya Sekondari ya Jang’ombe.

Bara bara hiyo ya Kilomita Tatu Nukta Tano inajengwa kwa gharama zilizotolewa na Uongozi wa Jimbo la Mpendae zinazokisiwa kufikia Shilingi za Kitanzania Milioni 1,000,000/- katika kiwango cha Kifusi.

Balozi Seif alisema kazi ya Mbunge, Mwakilishi na Diwani katika Majimbo na Wadi ni kusimamia utatuzi wa kero zinazoipata Jamii katika Majimbo husika. Hivyo Wananchi wana wajibu na haki ya kuwauliza wale wanaoomba ridhaa ya kutaka kuwaongoza watawafanyia nini watapowachagua.

Alifahamisha kwamba wapo baadhi ya Viongozi wanaoteuliwa na Wananchi kazi yao kubwa ni kupika majungu pamoja na kuleta malumbano yasiyo na msingi na kusababisha upotevu wa muda badala ya ile kazi waliyoomba ya kusimamia huduma za Kijamii.

“ Wapo baadhi ya Viongozi Majimboni kazi yao kubwa ni kuleta fitna na majungu ndani ya kipindi chao cha miaka mitano ambao baadaye hurudi tena kwa wananchi kuomba ridhaa bila ya juhudi zilizoonekana za kuwaletea maendeleo wananchi waliowachagua “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif ameupongeza Uongozi wa Jimbo la Mpendae kwa uamuzi wake wa kuwapatia zawadi hiyo ya Bara bara Wananchi hao wa Mpendae.

Alisema ujenzi wa Bara bara unaofanywa na Serikali kwa kushirikiana na washirika wa Maendeleo wakiungwa Mkono na Viongozi wa Mjaimbo kwa zile bara bara za ndani lengo lake kuu ni kuwarahisishia Wananchi Usafiri.

Balozi Seif aliwataka Wananchi watakaoitumia Bara bara hiyo kuendelea kuilinda na kuitunza ili idumu kwa muda mrefu zaidi kwa vile tayari imeshakuwa mkombozi wao katika sekta ya mawasiliano ya usafiri wa Bara bara.

Akitoa Taarifa za ujenzi wa Bara bara hiyo Mbunge wa Jimbo la Mpendae Mh. Salim Hassan Turky alisema kwamba ujenzi wa Bara bara hiyo ya Mombasa hadi Jang’ombe ni zawadi maalum iliyoamuwa kutolewa na Uongozi wa Jimbo hilo kwa Wananchi wake.

Mh. Turky alisema zawadi hiyo imekuja kufuatia kazi kubwa iliyofanywa kwa pamoja kati ya Uongozi na Wananchi hao katika kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 -2015 kwa njia ya amani na utulivu iliyowawezesha kufikia kiwango kizuri cha asilimia 97%.

Mbunge huyo wa Jimbo la Mpendae anayemaliza muda wake wa Miaka mitano alieleza kwamba endapo Wananchi wa Jimbo hilo wataamua kumpa ridhaa tena ya kuliongoza Jimbo hilo mkazo mkubwa utawekwa katika kubuni miradi ya amali pamoja na kuomba kibali Serikalini cha ujenzi wa Chuo cha amali iwapo watapatiwa eneo la ardhi.

Alisema mipango hiyo itakwenda sambamba na ujenzi wa kiwanda cha vibiriti lengo likiwa ni kujenga fursa za ajira kwa vijana wanaomaliza masomo yao ndani ya Jimbo hilo pamoja na Majimbo mengine hapa Nchini.

Naye Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Issa Ussi Gavu alisema kwamba Serikali kupitia Wizara hiyo itaunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Viongozi wa Majimbo katika ujenzi wa Bara bara za ndani.

Mh. Gavu alisema katika kuunga mkono jitihada zilizoonyeshwa na Uongozi wa Jimbo la Mpendae Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano itasaidia kuweka Lami kwenye bara bara hiyo licha ya kwamba bara bara za ndani zinapaswa kusimamiwa na Viongozi wa Majimbo.

Bara bara ya ndani iliyoanzia Soko la Mboga mboga kwa Mchina hadi kumalizikia skuli ya Sekondari ya Jang’ombe ambayo haikuwamo ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya Jimbo la Mpendae ni zawadi njema, nzuri na ya faraja iliyotolewa na Viongozi wa Jimbo hilo wanaomaliza muda wao wa utumishi wa miaka mitano.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
26/7/2015.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link