Home » » Waziri Mkuu Majaliwa aibukia bandari ya Tanga

Waziri Mkuu Majaliwa aibukia bandari ya Tanga

Written By CCMdijitali on Saturday, February 20, 2016 | February 20, 2016

 Matishari matatu ambayo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametaka apewe maelezo kwa maandishi kuwa ni nani aliyeidhinisha mchakato wa manunuzi yake bila kuzingatia viwango na ubora uliokusudiwa na serikali.. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)

Na Habari Leo

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ziara ya kushitukiza ya kukagua Bandari ya Tanga na kumtaka Mkuu wa Bandari hiyo (Port Master), Henry Arika ampelekee maelezo kuhusu ukiukwaji wa ununuzi wa tishari ifikapo leo saa 6 mchana.

Waziri Mkuu ambaye aliwasili Tanga jana mchana kushiriki maziko ya Mzee Ally Mwalimu Makwaya, ambaye ni baba mzazi wa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, aliamua kuzuru bandari hiyo kabla ya kuelekea uwanja wa ndege akiwa njiani kurejea Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo fupi, Waziri Mkuu alikataa kuingia ofisini (bandarini) na akataka apelekwe mahali tishari tatu za bandari hiyo zilipo.

Katika maswali aliyoulizwa na Waziri Mkuu, Arika alikiri kuwa matishari hayo hayafanyi kazi kama inavyotakiwa kwa sababu yanasubiri kusukumwa na tugboat (meli ndogo).

“Nataka kesho saa 6 mchana uniletee barua yenye maelezo ni kwa nini mlinunua tishari tatu ndogo badala ya mbili kubwa, wakati mnajua Serikali ilitenga Dola za Marekani milioni 10.113, kwa ajili ya kununua tishari mbili zenye uwezo wa kujiendesha zenyewe. “Nataka maelezo ni kwa nini mlizinunua tangu mwaka 2011 lakini zimekaa bila kufanya kazi hadi Novemba mwaka jana? 

Na kwa nini mnaendelea kutumia fedha za Serikali kwa kukodisha tishari kutoka Mombasa, badala ya kutengeneza za kwenu au kufundisha vijana wa Kitanzania? Kwani tunao wahitimu wangapi wa fani hii?” Alihoji Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema anazo taarifa kwamba moja ya tishari lilidondoka baharini, wakaenda kutafuta huko na kulivuta hadi pwani ndiyo maana yameshindwa kufanya kazi inavyotakiwa.

Katika majibu yake, Arika alisema wao waliagiza tishari hizo kupitia ofisi ya Bandari Makao Makuu ambayo iko Dar es Salaam.

“Pia wakati zinaagizwa sikuwepo hapa Tanga. Nimekuja mwishoni mwa mwaka jana,” alisema Mkuu huyo wa Bandari ambaye inaelezwa alitokea Mamlaka ya Bandari Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza awaite watu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Mamlaka ya Bandari na Jeshi la Polisi wakae na kutafuta mbinu za kudhibiti njia za panya zinazotumika kupitisha sukari ya magendo.

“Mkuu wa Mkoa simamia hawa watu, msaidiane kudhibiti uingizaji wa sukari kwa njia za panya. Kuna majahazi yanaleta sukari kutoka Brazil. “Mheshimiwa Rais amepiga marufuku uingizaji wa sukari kutoka nje ili viwanda vyetu vya ndani viongeze uzalishaji. Dhibitini bandari zote ndogondogo hadi Pangani,” aliagiza Waziri Mkuu.

Alisema changamoto inayoikabili Serikali ni kwamba hata Shirika la Viwango Tanzania (TBS) au Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) hawawezi kukagua sukari hizo na hazijulikani ubora wake licha ya kuwa zinafika kwa walaji.

 Waziri Mkuu Kassim Majliwa akizungumza na Mkuu wa bandari ya Tanga, Henry Arika (kulia kwake ) na Mhandisi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Felix Mahangwa ( kulia wakati alipotembelea bandari ya Tanga Februari 19, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kssim Majaliwa akiongozwa na Mkuu wa Bandari ya Tanga , Henry Arika (kulia kwake) kukagua bandari hiyo Februari 19, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link