Home » » Magufuli azuia wamachinga kuondolewa

Magufuli azuia wamachinga kuondolewa

Written By CCMdijitali on Friday, August 12, 2016 | August 12, 2016




Na "MwananchiNews"

Kwa ufupi

  • “Hakuna kuondoa machinga mjini kwani huko nje mnakowapeleka hakuna wateja,” ilikuwa ni kauli ya Rais Magufuli iliyopokewa kwa shangwe na umati wa wakazi wa Mwanza uliofanyika katika Viwanja vya Furahisha.

Mwanza. Rais John Magufuli amepiga marufuku operesheni za kuwaondoa mijini wamachinga badala yake ameziagiza mamlaka husika kuboresha mazingira ya biashara kwa kundi hilo.

“Hakuna kuondoa machinga mjini kwani huko nje mnakowapeleka hakuna wateja,” ilikuwa ni kauli ya Rais Magufuli iliyopokewa kwa shangwe na umati wa wakazi wa Mwanza uliofanyika katika Viwanja vya Furahisha.

Amesema kila mtu ana haki ya kuishi mjini na kuendesha shughuli halali za kiuchumi zitakazomwezesha kuwa na maisha bora kulingana na sheria, kanuni na taratibu, hivyo ni wajibu wa halmashauri za majiji, manispaa, miji na wilaya kuwawezesha wamachinga kuendesha shughuli zao.

“Viongozi wa mikoa wakae na kujadiliana nao (wamachinga) kuona ni sehemu gani watawapeleka kwa kuzingatia mazingira mazuri ya kufanya biashara,” ameagiza.

Hata hivyo, Rais Magufuli aliwaonya wamachinga kuhusu tabia ya kukubali kutumiwa na wafanyabiashara wakubwa kwa kuwauzia bidhaa zao na hivyo kuikosesha mapato Serikali.

Rais Magufuli amerejea agizo lake kwa halmashauri zote nchini na mamlaka nyingine zinazohusiana na ukusanyaji wa kodi kuacha kuwarundikia kodi na ushuru wa kero wakulima na wajasiriamali wadogo, badala yake, nguvu nyingi zielekezwe kwenye kukusanya kodi kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa.

“Ninataka kodi, lakini siyo kwa watu maskini wakiwemo wakulima na wajasiriamali wadogo, bali kwa wafanyabiashara wakubwa. Machinga ndiyo walionichagua, hivyo sitaki wabughudhiwe. Hatuwezi kuwa na Serikali nzuri tukiwasumbua wananchi.”amesema
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link