Home » » MHE. SAMIA SULUHU AHUDHURIA UFUNGUZI WA MKUTANO WA 36 WA SADC MJINI MBABANE SWAZILAND

MHE. SAMIA SULUHU AHUDHURIA UFUNGUZI WA MKUTANO WA 36 WA SADC MJINI MBABANE SWAZILAND

Written By CCMdijitali on Tuesday, August 30, 2016 | August 30, 2016

Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika -SADC-
ambaye pia ni Rais wa Botswana Luteni Jenerali Dkt. Seretse Khama Ian
Khama amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli kwa kuchaguliwa kwake kwa kishindo katika uchaguzi mkuu
uliofanyika mwaka jana.

Rais huyo wa Botswana ametoa kauli hiyo
ya pongezi katika hotuba yake kwenye ufunguzi wa Mkutano wa 36 wa Wakuu
wa Nchi na Serikali wa SADC unaofanyika Mbabane- Swaziland ambapo Katika
Mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dakta JOHN POMBE
MAGUFULI anawakilishwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Rais huyo wa Botswana amesema ukuaji
wa demokrasia katika nchi wanachama wa jumuiya ya SADC unaendelea
kuimarika hivyo ni muhimu jitihada hizo zikaendelezwa zaidi.

Amesema ana Imani kubwa na Viongozi waliochaguliwa kwa njia ya
amani,uhuru na haki katika ukanda wa SADC akiwemo Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Visiwa shelisheli kwamba
watafanya kazi kwa bidii ili kuharakisha maendeleo kwa wananchi wao.


Wakuu wa nchi na Serikali wa SADC katika mkutano huo wameshuhudia
utoaji wa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika
utunzi wa insha na kwa wanahabari ambao wameandika habari mbalimbali
kuhusu SADC ikiwemo masuala ya huduma ya maji.

Aidha katika Mkutano huo wa 36 wa SADC viongozi wanaohudhuria watafanya uchaguzi wa
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa SADC na Uchaguzi wa Mwenyekiti na
Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, 
Ulinzi na Usalama ( SADCTroika).

Katika mkutano huo Wakuu wa nchi na serikali pia
watapokea rasimu za maboresho ya mikataba mbalimbali kutoka kwenye
Baraza la Mawaziri kwa ajili ya kutia saini. Miongoni mwa rasimu hizo ni
mkataba wa kuboresha itifaki ya SADC dhidi ya rushwa, maboresho ya
itifaki ya ushirikiano wa siasa, ulinzi na usalama ya SADC na maboresho
ya itifaki ya biashara.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisaini ubao wa kumbukumbu kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli wenye majina ya viongozi waliohudhuria mkutano wa 36 wa SADC uliofanyika Lozitha, Mbabane Swaziland.

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan (katikati) akiwa kwenye mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofunguliwa leo kwenye ukumbi wa Mandvulo uliopo Lozitha, Swaziland.

 Mfalme Mswati wa III (kushoto) akihutubia kwenye ufunguzi wa mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC kwenye ukumbi wa Mandvulo, Lozitha Swaziland.

 Binti akionyesha bendera ya Tanzania wakati wa kuimba shairi maalum ya ufunguzi wa mkutano wa 36 wa SADC

Wakuu wa nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa  Afrika (SADC) wakiwa kwenye picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi wa mkutano wa 36, Lozitha Swaziland.
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link