MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) inatarajia kubadilisha vitambulisho vyote vya zamani ambavyo havina saini, huku ikitarajia kutoa vitambulisho vipya vyenye saini kwa wananchi wote, waliokamilisha taratibu za usajili na utambuzi kwa kuchukuliwa alama za kibayolojia, ikiwemo alama za vidole, picha na saini ya kielektroniki.
Aidha, inatarajia kutoa vitambulisho vipya kuanzia Septemba 14, mwaka huu katika ofisi zote za Nida za wilaya. Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Andrew Massawe, ilisema kwa sasa vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika sambamba na vipya huku taratibu za kuvibadilisha zikiendelea.
‘’Kutokana na uwepo wa njia nyingi na salama za kusoma taarifa za mwombaji zilizomo ndani ya kifaa maalumi kilichofichwa kwenye kadi ya mtumiaji; ndiyo maana vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumikakatika huduma mbalimbali zinazohitaji kumtambua mtumiaji kabla ya kupata huduma,’’ alisema Massawe.
Alisema kuwa ofisi za wilaya zilizoanza usajili wa vitambulisho hivyo vipya kwa Tanzania Bara na Zanzibar ni mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Ruvuma na Dodoma.
‘’Waombaji wote ambao vitambulisho vyao viko tayari watatumiwa ujumbe mfupi wa maandishi katika simu zao za mkononi kuwafahamisha kufika vituo vya usajili kuchukua vitambulisho vyao,’’ alisisitiza Massawe.
Alifafanua kuwa wananchi ambao hawakuwahi kusajiliwa na wana umri wa miaka 18 na kuendelea na kwa mikoa ambayo tayari kuna ofisi za usajili, wajitokeze kwa wingi kusajiliwa ili kupata vitambulisho hivyo.
‘’Kwa wale ambao walisajiliwa kupitia Daftari la Kudumu la Mpiga Kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Nida iko mbioni kuanza kutoa nambari za utambulisho wakati taratibu za uzalishaji zikiendelea,’’ alisema.
Pia aliwakumbusha wananchi kutunza vitambulisho vyao ili kuepuka gharama kwani kitambulisho cha awali kilitolewa bure na iwapo kitapotea, ili kupata kingine lazima mtumiaji alipie.
Aliongeza kuwa kwa sasa vitambulisho hivyo vimeanza kutumika katika baadhi ya huduma hususani kwenye benki kwa ajili ya kufungua akaunti na kuthibitisha taarifa za mtu kabla ya kupata huduma.