SIKU moja baada ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu atoe taarifa ya hali ya uchumi nchini inayoonesha uchumi unakua na deni la taifa ni stahimilivu, wataalamu wa uchumi wamesema, taarifa hiyo ni sahihi na imetolewa kwa wakati muafaka.
Aidha, wamesema ni vyema wananchi wakaishi maisha ya kipato chao cha halali, kwani wengi wao walizoea maisha ya juu kutokana na uwepo wa fedha chafu kwenye mzunguko na sasa mianya hiyo imefungwa ndio maana fedha zimepungua kwenye mzunguko.
Wakizungumzia taarifa hiyo jana jijini Dar es Salaam, wataalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), walisema ni vyema wananchi wakaongeza bidii kufanya kazi na kwamba viashiria vyote vya ukuaji wa uchumi vilivyotolewa na Profesa Ndulu viko sahihi.
“Sina kipingamizi, viashiria vyote vinavyotumika kupima hali ya uchumi wa taifa viko chanya, hii ni dalili nzuri ni vyema Watanzania wakakubali kuishi maisha ya uwezo wao, baada ya muda kidogo watazoea, zile fedha za dili hazipo tena kwenye mzunguko,” alisema Profesa Rozack Lokina wa Idara ya Uchumi chuoni hapo.
Profesa Lokina akifafanua alisema wananchi wanachotakiwa sasa ni kufanya kazi kwa tija na kuukubali ukweli kwamba fedha za bure katika Serikali ya Awamu hii ya Tano hazipo, na kuwataka watu wanaosema uchumi umedorora, wakaacha kauli hiyo kwa sababu uchumi unapimwa kwa viashiria.
“Mi sioni uchumi ukidorora, watu wanaosema uchumi wa nchi umedorora, wamepima kwa viashiria gani? Chombo chenye mamlaka ya kutoa taarifa za uchumi kimetoa taarifa na ndio tunayopaswa kuiamini,” alisema Profesa Lokina.
Profesa Benson Bana ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Udsm alisema, taarifa hiyo ya BoT imetolewa kwa muda muafaka kwani siku chache zilizopita watu wenye nia mbaya walieneza taarifa potofu kuwa uchumi wa nchi umedorora.
“Chombo chenye mamlaka ya kutoa taarifa za hali ya uchumi nchini ni BoT na Gavana Ndulu amelizungumzia vizuri kwa kutumia viashiria vinavyotumika duniani, na vimeonesha uchumi wetu unakua kiwango cha kuridhisha,” alisema Profesa Bana.
Akifafanua hali ya uchumi, alisema suala hilo halihitaji siasa kwa sababu linatumia viashiria vinavyotambulika kimataifa na ndivyo vilivyotumika kujua hali ya uchumi ulivyo kwa sasa, ambapo takwimu zimetolewa Pato la Taifa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2016, unakadiriwa kuongezeka kwa asilimia 5.5 ikilinganishwa na kipindi hicho mwaka jana cha asilimia 5.7.
Profesa Bana alisema kuna tofauti ndogo ya asilimia 0.2 ambayo haina athari yoyote kiuchumi na kwamba tofauti hiyo ni jambo la kawaida na kwamba mzunguko wa fedha chafu uliokuwepo nchini mianya yake imezibwa, ndio maana watu wanalalamika hakuna fedha mtaani.
“Unajua fedha chafu ziliingia kwenye mzunguko wa uchumi na sasa mianya yake imezibwa ni lazima watu walalamike ila cha msingi ni wao warudi kwenye maisha halisi na wafanye kazi,” alisema Profesa Bana.
Akizungumzia hali ya uchumi wa nchi na mtazamo wake duniani, Profesa Bana alisema Tanzania inafanya vizuri na kimataifa imekuwa miongoni mwa nchi 10 barani Afrika ambazo uchumi wake unakua vizuri. Aidha, katika kiwango cha ukuaji kwa nchi za Afrika Mashariki, Tanzania ni nchi ya kwanza ambayo uchumi wake unakua vizuri, hivyo kauli za baadhi ya wanasiasa kujaribu kuupotosha umma kwamba uchumi wa nchi umedorora, sio jambo sahihi.
“Hapa Gavana alituelimisha kwa njia sahihi na ndiye mwenye mamlaka ya kutoa takwimu za hali ya uchumi na vigezo vya kimataifa vimetumika sasa wanasiasa wasijaribu kutafuta umaarufu kwa kusema uchumi umedorora, uchumi una vigezo vyake,” alisema Profesa Bana.
Alisema jambo la msingi sasa ni kuona ukuaji huo wa uchumi ukimgusa mwananchi mmoja mmoja na hiyo inawekezana kwa serikali kuhimiza sera nzuri zitakazosaidia watu kupata fedha kwa kufanya kazi. Naye Dk John Mtui ambaye ni mtaalamu wa uchumi kutoka Udsm alisema ni vigumu kusema uchumi wa nchi ni mbaya ingawa fedha kwenye mzunguko zimepungua.
“Hapa kinachoangaliwa ni viashiria vya uchumi, ingawa fedha zimepungua kwenye mzunguko, hii haimaanishi kwamba hali ya uchumi ni mbaya, kinachotakiwa ni watu kufanya kazi na kuachana na hulka ya kungoja fedha za dili,” alisema Dk Mtui.
Alisema watu wakifanya kazi, itawalipa na kwamba fedha chafu ziliingia kwenye mzunguko kwa wingi kwani wapo baadhi walikuwa wakifanya biashara bila kulipa kodi, wapo waliokuwa wakipata zabuni kwa njia haramu na mianya hiyo imezibwa hivi sasa.
“Yaani mambo mengi yaliendeshwa kwa kupeana dili, unakuta mtu ana kampuni ya kuuza chakula, wanapeana rushwa halafu ile zabuni inaongezwa fedha ambazo sio halali, zinaingia kwenye mzunguko sasa hayo mambo yamezibwa watu lazima walalamike,ila hali itatulia baada ya muda“, alisema Dk Mtui.
Wakati wasomi wakisisitiza hali ya uchumi inaridhisha kutokana na viashiria vya uchumi, Chama cha Wananchi (CUF), wamemuomba Gavana Ndulu kuondoa kilio cha ukosefu wa fedha kwa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyotolewa jana na Naibu Mkurugenzi Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, Mbarara Maharagande, ilisema kiuhalisia hali ya uchumi haiwezi kuwa nzuri kama Watanzania wanalia kukosa fedha mtaani.
“Haiwezekani Watanzania wote walipata fedha kwa njia zisizo halali kwa kuwa serikali imebadili mfumo wa ukusanyaji,” ilisema taarifa hiyo na kumtaka gavana kuingilia kati na kuhakikisha fedha kwenye mzunguko zinakuwepo ili wananchi waweze kuendesha maisha yao.
Mbunge wa Vunjo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia amemshauri gavana kuandaa mdahalo utakaowashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya uchumi ili kujadili taarifa hiyo kwa kina kwa kuona jinsi ukuaji huo wa uchumi utakavyosaidia mwananchi mmoja mmoja.
“Tunaposema uchumi unakua ni vyema tukaangalia pia, unasaidiaje maisha ya mtu mmoja mmoja, je anaweza kupata kipato cha kula milo mitatu kwa siku, je hali ya maisha ya Mtanzania wa kipato cha chini ikoje, lazima ukuaji uchumi uakisi maisha ya watu hawa,” alisema Mbatia.