Home » » Watoto wa kike kulindwa wasipate mimba

Watoto wa kike kulindwa wasipate mimba

Written By CCMdijitali on Thursday, September 15, 2016 | September 15, 2016


    Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma | Habari Leo
   


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameonesha hofu kutokana na kukithiri kwa mimba za utotoni na kusema serikali itaweka mikakati ya kupambana nazo kutokana na kuathiri maisha ya wasichana kuanzia miaka 14 hadi 17 ambao wengi wapo hatarini kupata Virusi Vya Ukimwi.

Ameyasema hayo jana mjini Dodoma wakati anafunga mafunzo ya wasimamizi na wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi Tanzania wa Mwaka 2016, yaliyokuwa yakifanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa iliyopo Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM).

Amesema serikali itakuja na mkakati ili kulinda maisha ya watoto wa kike, ambayo yamekuwa yakiathiriwa na mimba za utotoni ili kufanikisha jitihada za serikali katika kupambana na umasikini.

“Kiashiria kikubwa ambacho wizara yangu iko katika kuweka mikakati ya kupambana nacho ni mimba za utotoni,” amesema Waziri Ummy.

Amesema takwimu za mwaka 2012 zinaonesha kwamba robo ya wasichana wote nchini wenye mri wa miaka 14 na 17, tayari walikuwa wameshajifungua angalau mara moja. Aliitaja mikoa inayoongoza kwa tatizo hilo kuwa ni Rukwa kwa asilimia 24.5 na Katavi kwa asilimia 27.6.

“Tunajua tatizo la mimba za utotoni ikiwa ni pamoja na uwezekano wa maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi na matatizo mengine ya kiafya,” amesema na kuongeza,

“Tusipowazungumzia wasichana hakuna maendeleo kwao watapata mimba watabaki mitaani hawataweza kuajiriwa au kujiajiri na hawataweza kulisha watoto wao.”

Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mara nyingine inafanya utafiti wa viashiria na matokeo ya Ukimwi na utafiti wa mwaka huu utahusisha watu wote kuanzia watoto wadogo hadi wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, wakati tafiti tatu zilizotangulia zimekuwa ziwahusisha wananchi wenye umri kati ya miaka 15 na 49.

Amesema tofauti na tafiti zilizotangulia, utafiti wa mwaka huu ni wa kipekee kwani kwa mara ya kwanza unahusisha wananchi wa rika zote katika kaya zilizochaguliwa.

Amesema pia ni utafiti wa kwanza kukusanya taarifa zinazohusu maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), kiasi cha VVU mwili kwa watu wanaoishi na VVU na kiwango cha maambukizi ya VVU kwa watu wa rika zote, wingi wa chembechembe za kinga mwilini.

Amesema katika tafiti zilizopita kiwango cha maambukizi ya VVU kimeonekana kupungua kutoka asilimia saba mwaka 2003 mpaka asilimia 5.1 mwaka 2011.

Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dk Albina Chuwa alisema utafiti huo ni wa aina yake kufanyika nchini ingawa umewahi kufanyika utafiti unaofanana na huo.

Alisema taarifa zinazokusanywa katika kila kaya ni siri na hakuna mdadisi yoyote atakayeruhswa kutoa siri ya mtu yeyote hadi yatakapofanyiwa uchambuzi wa kina na kutoa matokeo ya jumla ya hali halisi ya maambukizi ya Ukimwi nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania, Leonard Maboko alisema ukusanyaji sahihi wa takwimu unaweza kusaidia taifa kufahamu idadi ya waathirika na kwa kiwango gani.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link