Balozi Seif akijibu na kufafanua hoja zilizotolewa na Wananchi wa Vijiji vya Matemwe Mbuyu Tende na Kijini kuhusu malalamiko ya kutolipwa fidia kwa ardhi yao kwa ajili ya ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa.
Baadhi ya Wananchi wa Vijiji vya Matemwe Mbuyu Tende na Kijini wakimsikiliza Balozi Seif hayupo pichani akijibu hoja na malalamiko yao kufuatia kero ya kutolipwa fudia ya ardhi yao mwa zaidi ya miaka Mitano sasa na muwekezaji anayetaka kujenga Hoteli ya Kimataifa ya Zanzibar Amber Resort.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeonya kwamba haitasita kumfukuza Muwekezaji yeyote aliyepewa fursa kuwekeza miradi yake Nchini na akashindwa kufuata masharti na taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa vigezo vya uwekezaji liliwemo suala la kunyanyasa Wananchi wa maeneo ya uliopo mradi.
Onyo hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi baada ya kusikiliza kero zinazowakabili wananchi wa Vijiji vya Matemwe Kijini na Mbuyu Tende kuhusu kutolipwa fidia kwa maeneo yao ya ardhi yaliyochukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa Mradi Mkubwa wa Hoteli ya Kimataifa ya Penny Royal.
Akijibu na kutoa ufafanuzi wa changamoto za Wananchi hao wa Matembwe Mbuyu Tende na Kijini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema azma ya Serikali katika kukaribisha wawekezaji ya kuanzisha miradi yao nchini imelenga kusaidia pato la Taifa sambamba na kunyanyua maisha ya Wananchi.
Balozi Seif alisema pamoja na kumuagiza Muwekezaji wa Mradi huo kulipa fidia Wananchi waliochukuliwa ardhi yao lakini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeunda Kamati Maalum itakayofuatilia suala hilo ili itowe ripoti itakayozingatia kutolewa haki kwa kila upande.
Aliwaeleza Wananchi hao wa Vijiji vya Matemwe Mbuyu Tende na Kijini kwamba Serikali Kuu hadi sasa haiendelea kumuongezea eneo zaidi ya Hekta 411 ilizompa Mwekezaji wa Mradi huo wa Penny Royal hadi hapo itakaporidhika na maendeleo ya hatau ya awali ya mradi huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Wananchi hao wa Jimbo la Kijini kwamba kila mwenye haki yake hatokosa kupatiwa lakini aliwaomba kuendelea kuwa na subra na uvumilivu ili maamuzi yatakayotoka yasije zaa kero jengine.
Balozi Seif aliwataka Wananchi wote waliohusika na tatizo hilo kuorodhesha majina na vielelezo vyao kwa Kamati husika kwa lengo la kutoa fursa za upatikanaji wa malipo yao bila ya dhulma wala ghushi yoyote.
Alisema Serikali haitaki kuona mizozo ya ardhi inaendelea katika maeneo mbali mbali nchini na hatimae kupelekea baadhi ya wawekezaji kuonyesha tabia ya kunyanyasa wananchi.
Mapema Balozi alisikiliza kero za Wananchi hao zilizowasilishwa kwa niaba yao na Mzee Khamis Hassan, Mzee Zaja Haji Khamis, Mzee Ali Mcha Ali, Mzee Simai Mshindani pamoja na Mzee Makame Haji hapo Mbuyu Tende pembezoni mwa eneo la maegesha ya boti zinazopeleka watalii katika Kisiwa cha Mnemba.
Wazee hao walitoa maduku duku yao hayo kubwa zaidi likiwa ni lile la muwekezaji huyo kushindwa kulipa fidia ya maeneo yao kwa takriban miaka mitano sasa wakiweka wazi kutokataa kuwekwa kwa mradi katika eneo lao lakini cha kuzingatia mwanzo na umuhimu wa kufuatwa kwa masharti na taratibu zilizokubalika kwa pande zote husika.
Walisema katika kutafua ufumbuzi wa tatizo hilo ipo haja kwa Wananchi, Serikali pamoja na Muwekezaji husika kukaa pamoja katika kuangalia njia sahihi itakayosaidia pande zote kupata muwafaka kwa amani.
Naye Mzee Makame Haji akizungumza kwa hamasa alitahadharisha wazi kwamba Serikali inapoamua kuwapelekea Wananchi muwekezaji lazima izingatie masuala ya utamaduni na silka za eneo husika ili kuwepuka mapema mtafaraku kwa pande zote mbili.
Mzee Makame alisema Jamii ya watu wa Matemwe Mbuyu Tende na Kijini hivi sasa imepata ufa na mtafaruku kufuatia eneo wanalolitumia kwa shughuli za mazishi ni miongoni mwa maeneo yaliyomo ndani ya mradi huo wa Hoteli.
Kampuni ya Penny Royal iko mbioni kuanzisha mradi mkubwa wa Hoteli ya Kimataifa itakayopewa jina la Zanzibar Amber Resort katika kijiji cha Matemwe Mbuyu Tende ndani ya Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mradi huo utakwenda sambamba na ujenzi wa Skuli, Hospitali, Kituo cha Polisi sambamba na ujenzi wa Kituo cha Jamii kitakachowapa fursa Wananchi wa Matemwe hasa wajasiri amali kuendesha miradi yao katika eneo la kisasa.
Mbali ya ujenzi wa uwanja wa ndege na kiwanja cha mchezo wa Golf unaopendwa zaidi na matajiri wakubwa Ulimwenguni, Wataalamu wa Kampuni inayosimamia mradi huo watatengeneza Visiwa vidogo vidogo kwa kufukia Bahari ili kuongeza mandhari nzuri ya mradi huo wa Hoteli.
Matengenezo hayo ya visiwa vidogo vidogo yatakwenda sambamba na ujenzi wa mkahawa maalum utakaojengwa chini ya Bahari zikiwemo nyumba za wafanyakazi.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
14/10/2016.