Home » » Taarifa ya ziara ya Siku tano ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Gambo,Wilayani Longido - ARUSHA.

Taarifa ya ziara ya Siku tano ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Gambo,Wilayani Longido - ARUSHA.

Written By CCMdijitali on Wednesday, November 2, 2016 | November 02, 2016

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo (aliyeko kwenye mtaro) akishiriki ujenzi wa daraja la chini linalojengwa na wananchi wa Mundarara,Wilayani Longido .

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
OFISI YA MKUU WA MKOA ARUSHA
Tansania-Emblem.png

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Mashaka Gambo katika utaratibu wake aliojiwekea wakutembelea Wilaya zote za Mkoa huu amekamilisha ziara ya kikazi ya SIKU TANO aliyoifanya katika Wilaya ya Longido kuanzia tarehe 24 -28/10/2016. Lengo ni kujitambulisha kwa wananchi, kufahamu changamoto na kuzitafutia ufumbuzi, kuona fursa zilizopo, kushiriki pamoja shughuli za maendeleo na kukagua miradi ya Maendeleo.

Mhe.Gambo alitembelea Tarafa zote nne za Longido, Enduimet, Kitumbeine pamoja na Engarenaibor kwenye Kata za GelaiLumbwa, GelaiMerugoi, Kitumbeine, Engarenaibor, Matale, Tingatinga, Olmolog, Sinya, Namanga, pamoja na Kata ya Longido. Pia alifanya mikutano ya hadhara na wananchi wa Vijiji na vitongoji vipatavyo kumi na tano.

Vilevile, Mkuu wa Mkoa alitembelea eneo la mpaka wa Tanzania na Kenya (Normans Land) na aliweza kukutana na wafanyakazi wa Taasisi za Serikali zinazotoa huduma eneo la mpakani pamoja na wafanyakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido.

Kupitia ziara hiyo ya kazi Mhe.Gambo alibaini na kutoa maelekezo katika maeneo yafuatayo:

i.     Mtandao wa Barabara – Barabara ya Esokonoi yenye urefu wa Km 25 iliyofunguliwa na kujengwa na wananchi kwa kutumia zana za asili iingizwe kwenye mtandao wa barabara za Halmashauri na kutengewa Fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi ili kuunga mkono jitihada za wananchi. Pia aliwajulisha wananchi kuwa barabara ya Namanga – Sinya – Elerai imepandishwa hadhi kuwa barabara ya Mkoa kupitia kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa cha tarehe 22/10/2016; Aliwataka Halmashauri kukamilisha haraka miradi ya Barabara iliyopo ili kuwaondolea kero wananchi.

ii.   Afya ya Jamii na uboreshaji wa miundombinu ya Afya – Wananchi walilalamikia upungufu wa dawa vituoni pamoja na huduma za afya kupatikana mbali na makazi yao. Rc Gambo alisema “Serikali ya Wilaya lazima ianze ujenzi wa Vituo vya Afya kwenye Kata za Kitumbeine na Namanga ili kuwasogezea wananchi huduma na ukizingatia wananchi wa Namanga huenda kutibiwa Kenya kutokana na kukosekana kwa huduma hii; Ujenzi wa Kituo cha Afya Namanga ufanyike kwenye eneo ilipokuwa Kambi ya Mkandarasi Namanga na kwa kuanza nachangia Bati 100 pamoja na mifuko ya saruji 100 nahitaji ujenzi huo uanze mara moja”.

Aliongeza kuwa Idara ya Afya iendelee kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuendelea kujiunga na mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili kupunguza changamoto ya uhaba wa dawa na watumishi wasio waadilifu waache  mara moja tabia ya  wizi wa dawa kwani huleta madhara makubwa kwa wananchi wanyonge.

iii.   Elimu Msingi na Sekondari - Walimu wanaofanya kazi katika Halmashauri ya Longido walisema wanaidai Serikali zaidi Tsh Million 250 za malimbikizo yasiyo kuwa ya mishahara, mishahara ya mwanzo pamoja na nauli. Kutokana na hilo, RC Gambo aliahidi kufuatilia kwa karibu ili madeni hayo yaweze kulipwa haraka iwezekanavyo.

iv.  Upatikanaji wa Maji – Iliripotiwa kuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa Longido na upatikanaji wa maji. Kutokana na hali hiyo RC Gambo aliagiza kuletewa taarifa ya miradi ambayo haijakamilika kutokana na Fedha kutowasilishwa kwa wakati ili aweze kufuatilia Fedha hizo Wizarani pia alisisitiza mradi mkubwa wa maji utakaogharimu Bilioni 13 uanze kutekelezwa mara moja. Mradi huo utaanzia Mto Simba (Siha) hadi vijiji vya Longido, Ollepes, Orbombo, Engikarate mpaka Ranchi na ukikamilika upatikanaji wa maji utaongezeka hadi kufikia asilimia 80.

v.    Nidhamu kwa Watumishi – Rc Gambo alisema “Nakuagiza katibu Tawala Mkoa kumuandikia barua Katibu Mkuu Tamisemi ili awarudishe aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Longido Bw. Julius Challya na Eng. Edwin Rwezaura waje kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya Fedha za mradi wa maji uliogharimu zaidi ya Tsh Mil 400”.

“Wafanyakazi wa mpakani acheni kupokea rushwa, inaonekana vitendo vya rushwa, urasimu na ubadhirifu vimekithiri hapa Namanga hakika sisi kama Serikali hatutasita kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kupokea na kutoa rushwa au kushirikiana na wahalifu kuhujumu mapato ya Serikali kwa namna yeyote ile tutamshughulikia pasipo kujali nafasi yake”.

vi.       Uwekezaji – Kutokana na wingi wa mifugo katika Wilaya ya Longido RC Gambo alishauri Halmashauri kuangalia uwezekano wa kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya Nyama na maziwa pia Viwanda vya kusaga nafaka ili kusitisha biashara inayoendelea sasa ya kusafirisha mazao ya nafaka ambapo inaweza kupelekea baa la njaa kwa wananchi; Uwekezaji huu utasaidia kuongeza mnyororo wa thamani pamoja na kuongeza ajira.

vii.   Ukuaji wa mji Namanga – Kutokana na  ongezeko la Idadi ya watu kumekuwa na uhitaji mkubwa wa huduma za kijamii katika eneo la Namanga hivyo Mkuu wa Mkoa ameagiza uongozi wa Wilaya kupitia madai ya wananchi wake ya kutaka kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mji mdogo katika eneo hilo na kuchukua hatua stahiki.

viii.     Ajira kwa Vijana – Mkuu wa Mkoa aliahidi kutoa boda boda kumi kwa vijana wanaofanya shughuli hizo katika Wilaya ya Longido, na kuangalia uwezekano wa kuongeza pikipiki hizo kwa kadiri atakavyoridhishwa na utendaji kazi wao lengo ni kuwajengea uwezo na kuinua pato la Vijana. Pia aliwaagiza Halimashauri kuhakikisha 10% ya mapato yao inawafikia  vijana na kina mama kama Serikali ilivyoelekeza.

ix.          Kuchangia miradi ya Maendeleo – Kupitia ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Arusha alichangia Mifuko ya saruji 580, Mabati 856, mbao 466, madawati 100 pamoja na mchango wa Fedha zaidi ya Tsh Mil 1.5 pia aliungwa mkono na Umoja wa waendesha Noah za Arusha – Namanga kwa kuchangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi unaondelea wa madarasa, zahanati, vituo vya afya, madaraja pamoja na barabara.

Mkuu wa Mkoa alihitimisha ziara yake kwa kuwataka Viongozi na wataalam kuendelea kujipanga namna gani ya kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kujitoa ili kupunguza malalamiko.

“Hakikisheni mnawatembelea wananchi vijijini, kusikiliza na kujibu hoja, mtatue changamoto zinazowakabili na kuwafariji katika harakati zao za kujitafutia kipato na kuleta maendeleo” Alisisitiza RC Gambo.
Imetolewa na:

     
Nteghenjwa Hosseah
Afisa  Habari





Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link