Kwa ufupi
Mikataba miwili imesainiwa leo jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Dk Tonia Kandielo.
Mikataba miwili imesainiwa leo jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Dk Tonia Kandielo.
By Benny Mwaipaja-WFM - Mwananchi
Dar es Salaam.
Benki ya Maendeleo ya Afrika(AfDB) imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa Sh360 bilioni, kwaajili ya kuchangia Bajeti kuu ya Serikali katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2016/2017 pamoja na kuongeza mtaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini(TADB).
Mikataba miwili imesainiwa leo jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James na Mwakilishi Mkazi wa AfDB, Dk Tonia Kandielo.
Mkataba wa kwanza uliosainiwa ni kwa ajili ya kutunisha Mfuko Mkuu wa Serikali ambapo benki hiyo imetoa Sh 154 bilioni ambazo zitaelekezwa kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania(Tanesco).
Mkataba wa pili ni kwaajili ya kuongezea mtaji wa TADB wenye thamani ya Sh 204 bilioni kwa ajili ya kuiongezea uwezo benki hiyo kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima ili kuongeza mnyonyoro wa thamani kuanzia uzalishaji, uongezaji thamani na upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima.
Uhai wa mikopo yote miwili utakuwa ni miaka 40 ambapo Serikali itaanza kuilipa baada ya miaka kumi tangu kutolewa kwake, huku riba yake ikiwa chini ya asilimia 1.
Akizungumza baada ya kusainiwa kwa mkopo huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amesema mkopo huo umekuja wakati muafaka na utasaidia kukuza na kuimarisha Tanesco na kuendeleza kilimo nchini.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkazi wa AfDB anayeondoka Dk Kandielo amesema kuwa hadi sasa benki yake imeipatia Tanzania mkopo wenye thamani ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 2, ambazo zimewekezwa kwenye miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, nishati ya umeme, elimu na kilimo.
“Ninaamini kuwa hatua ya kuongeza mtaji katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo-TADB itachochea maendeleo ya kilimo nchini, na tunaahidi kuwa tutaendelea kuiwezesha zaidi siku zijazo” Alisema Dkt. Kandielo.