Home » » Kampuni ya Ujerumani kujenga kiwanda Kilwa

Kampuni ya Ujerumani kujenga kiwanda Kilwa

Written By CCMdijitali on Monday, December 19, 2016 | December 19, 2016


Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke
Imeandikwa na Mwandishi Maalumu - Habari Leo

KAMPUNI ya Ujerumani ya Ferrostaal inatarajia kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea katika wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, kitakachogharimu zaidi ya Euro bilioni 1.2, ambacho kitakuwa moja ya viwanda vikubwa vya mbolea barani Afrika.

Aidha, Balozi huyo wa Ujerumani ameahidi kuwa nchi yake iko tayari kutoa kiasi kikubwa cha fedha ili kuifanyia ukarabati meli ya mv Liemba, inayofanya safari zake katika ziwa Tanganyika.

Meli hiyo ya kihistoria yenye umri wa zaidi ya miaka 100, itakarabatiwa ili iweze kuendelea kutoa huduma kwa watanzania na nchi jirani za Zambia, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Hayo yamesemwa na Balozi wa Ujerumani nchini, Egon Kochanke, wakati alipomtembelea na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, Dar es Salaam jana. Wawili hao walizungumzia masuala kadhaa yanayohusu uhusiano kati ya Tanzania na Ujerumani, uliodumu kwa muda mrefu.

Balozi Kochanke alisema kuwa kiwanda hicho, kitajengwa kwa ubia kati ya kampuni hiyo ya Ujerumani na wawekezaji wazawa na wengine kutoka Bara la Asia. Kitajengwa kutokana na hamasa kubwa ya serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dk John Magufuli kuhusu ujenzi wa viwanda.

“Kiwanda hiki kitakuwa kikubwa zaidi ya mara mbili ya kiwanda cha saruji cha Dangote kilichoko Mtwara na kitagharimu Euro bilioni 1.2, kitasisimua uchumi wa nchi na kukuza ajira,” alisema balozi huyo aliyeambatana na Naibu Balozi wa Ujerumani nchini, John Reyels na Mkurugenzi wa Ushirikiano wa nchi hiyo, Julia Hannig. “Mbali ya Kampuni hiyo ya Ferrostaal, wawekezaji wengine ni kampuni ya Mbolea ya Minjingu, na kampuni nyingine kutoka Pakistan ambayo kwa pamoja wameingia ubia wa kujenga kiwanda hicho cha mbolea kitakachokuwa uwekezaji mkubwa,” aliongeza Balozi Kochanke.

Kochanke aliiomba serikali kutatua changamoto ya gharama za gesi ili kiwanda hicho kiweze kuanza ujenzi wake mapema, hivyo kuchochea maendeleo ya kilimo nchini. Kwa upande wake, Dk Mpango aliishukuru Ujerumani kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.

Alisema kwamba Tanzania iko tayari kuendeleza ushirikiano huo. Alisema kuwa uwekezaji wa kiwanda kikubwa na cha mfano cha mbolea huko mkoani Lindi, utachochea sekta ya kilimo ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya watanzania, kwa kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya wakulima na mbolea ya ziada itauzwa nchi za nje.

Dk Mpango alimshukuru Balozi huyo wa Ujerumani kwa ahadi yake ya kusaidia kukarabati meli ya mv Liemba. Aliiomba nchi hiyo kusaidia kununua meli mpya ili kuimarisha usafiri wa watu na mizigo katika eneo la maziwa makuu.





Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link