Halmashauri ya Jiji la Arusha imesaini makubaliano na Jimbo la Hubei nchini China ili kuwasaidia jiji hilo katika nyanja za kilimo, biashara, sayansi na teknolojia.
Akizungumza mara baada ya kuingia makubaliano hayo leo, Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Athuman Kihamia amesema makubaliano hayo ni ya mwaka mmoja na yanatarajia kufungua fursa mbalimbali za kibiashara baina ya pande zote mbili.
Mkurugenzi wa jiji la Arusha, Athuman Kihamia amesema wanalenga Arusha kuwa miongoni mwa majiji bora kibiashara na hivyo makubaliano hayo yatasaidia wafanyabiashara jijini hapa kufungua milango ya kibiashara na jimbo la Huangshi nchini China.
Makamu mwenyekiti wa kamati maalumu ya Bunge la Huangshi nchini China, Weng Bin alisema mbali na biashara, makubaliano hayo yatafungua fursa mbalimbali kwa walimu wanaofundisha lugha ya Kiswahili mkoani Arusha kwenda kufundisha nchini China.