Home » » Nassari aipa tano serikali ya JPM

Nassari aipa tano serikali ya JPM

Written By CCMdijitali on Monday, December 19, 2016 | December 19, 2016

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Meya wa Jiji la Arusha, Kalisti Lazaro (wa pili kulia) na wabunge wa upinzani waliohudhuria katika mkutano wake wa majumuisho wa ziara ya Mkoa wa Arusha kwenye ukumbi wa mkuu wa mkoa huo, jana. Wa pili kutoka kushoto ni Mbunge wa Arumeru Magharibi, Gipson Mesiek, Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).



Imeandikwa na Jeremiah Vitalis Sisya - Habari Leo

Mwandishi Maalumu, Arusha MBUNGE wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) ameipongeza na kuisifu Serikali ya Awamu ya Tano kwa jitihada kubwa inazofanya katika kuwaletea wananchi maendeleo bila kujali maeneo wanakotoka kote nchini.

Aidha, Nassari amewataka wabunge wenzake kushirikiana na serikali hiyo inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwani sasa imeonesha dira ya maendeleo kwa wananchi wake na ameahidi kushirikiana nayo bega kwa bega kuhakikisha maendeleo yanakuwa endelevu.

Nassari ametoa pongezi hizo jana mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyekuwa katika majumuisho ya ziara yake ya siku 10 ya kikazi mkoani Arusha.

Mbunge huyo aliyelazimika kuja nchini kwa dharura akitokea masomoni nchini Uingereza ili kumuwahi Waziri Mkuu, alisema ameridhishwa na hatua za utatuzi wa migogoro ya ardhi zinazochukuliwa na Serikali.

Alisema ziara ya Waziri Mkuu mkoani Arusha, imesaidia kutibu majeraha na makovu makubwa yalitokana na matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.

“Kama kuna kiongozi ambaye hawezi kuunga mkono jitihada hizi za kuwaletea maendeleo watu wetu, atakuwa na matatizo,” alisema Nassari.

Alisema kitendo cha Waziri Mkuu kuweka mikakati ya kushughulikia migogoro ya ardhi iliyodumu kwa miaka mingi ni ushahidi tosha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwasaidia wananchi wa kawaida.

Nassari alisema mwaka 1952 wazee wa Meru walimtuma mtu kwenda Uingereza kuomba Uhuru wa wananchi wa Arumeru ili waweze kujitawala na kumiliki ardhi yao kutoka kwa wakoloni. Alisema wazee hao walichukua uamuzi huo baada ya kuchoshwa na vitendo vya unyanyasaji vilivyokuwa vinafanywa na wakoloni dhidi yao.

Lakini miaka 55 imepita tangu nchi ipate Uhuru bado migogoro na mateso hayo yapo. Kutokana na hatua zinazochukuliwa sasa, Nassari alimpongeza Waziri Mkuu kwa kuamua kuitafutia ufumbuzi changamoto ya ardhi wilayani Arumeru, jambo ambalo litawawezesha wananchi kupata ardhi kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kimaendeleo zikiwemo za kilimo na ufugaji.

Waziri Mkuu juzi alifanya ziara katika wilaya ya Arumeru ambapo alisema serikali itawanyang’anya ardhi wamiliki wote wenye mashamba makubwa wilayani Arumeru ambao hawajayaendeleza kwa sababu wamekiuka mkataba wa umiliki.

Alisema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi atakwenda Arusha kwa ajili ya kufanya mapitio ya mashamba yote makubwa ambayo hayajaendelezwa na kuyarudisha Serikalini.

“Tufanya mapitio ya kila shamba ili kujua linamilikiwa na nani na alipewa lini na tangu alipokabidhiwa amefanya nini. Shamba lisiloendelezwa litarudisha kwa wananchi. Kama mtu ameshindwa kupata mtaji kwa muda wa miaka 10 atapata leo,” alisema Majaliwa akiwa Arumeru juzi.

Alisema wilaya ya Arumeru inaongoza kwa migogoro ya ardhi na maeneo mengi yametwaliwa na mtu mmoja na baadhi yao wamekuwa wakilitumia vibaya Jeshi la Polisi kwa kuwanyanyasa wananchi wanaokatiza au kulima kwenye maeneo hayo, na aliwataka polisi kuacha tabia hiyo mara moja.





Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo (kushoto) wakizungumza na Mbunge wa Monduli, Julius Kalanga (wapili kulia) na Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Monduli, Isaac Joseph (kulia) baada ya Waziri Mkuu kumaliza kikao cha majumuisho ya ziara yake mkoani Arusha kwenye ukumbi wa Mkuu wa mkoa huo, Desemba 18, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link