Home » » Viwanda 1,845 vyajengwa nchini

Viwanda 1,845 vyajengwa nchini

Written By CCMdijitali on Thursday, December 15, 2016 | December 15, 2016


Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.


 Imeandikwa na Lucy Lyatuu    - Habari Leo 


WIZARA ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, imesema hadi kufikia Oktoba mwaka huu, viwanda 1,845 vimejengwa nchini ikiwa ni hatua mojawapo ya kuwezesha kufikiwa kwa Serikali ya viwanda.

Aidha imeelezwa Tanzania inauza bidhaa zake nje yanchi kwa kiwango kidogo, ambapo ni ya 114 kati ya 185 katika kuuza bidhaa zake nje ya nchi.

Waziri wa wizara hiyo, Charles Mwijage alisema hayo jana, Dar es Salaam wakati akizindua kitabu cha mwongozo wa kuuza bidhaa nje ya nchi, ambacho kitasaidia kutoa maelekezo ya kuanza kuuza bidhaa nje y anchi na pia kusaidia kutoa tathmini kwa wale wanaouza nje ya nchi.

Kuhusu ujenzi wa viwanda, Mwijage alisema Serikali ya awamu ya tano haina mpango wa kujenga viwanda vipya, bali vilivyokuwepo viweze kuboreshwa na kuweza kuzalisha kwa kiwango cha juu zaidi na kuwa na bidhaa zenye ubora.

“Katika kuhakikisha dhana ya Serikali ya viwanda inafikiwa, jambo ambalo ninaweza kujivunia (Mwijage) ni pamoja na kuwepo kwa uhamasishaji mkubwa na wa kutosha juu ya ujenzi wa viwanda ambapo viwanda hivyo vimeweza kujengwa hadi Oktoba,” alisema Mwijage.


Kuhusu uzinduzi wa kitabu hicho aliwataka wataalamu waliobobea katika biashara kuandika vijarida vyenye kutoa muongozo wa namna ya kufanya biashara nje ya nchi ili kwamba watanzania watakaoweza kushiriki waweze kupata muongozo na kuwa na mazingira rafiki ya kufanya biashara.

Alisema Tanzania ina fursa ya kunufaika na bidhaa za viwanda na hivyo inahitaji kuwa na mikakati thabiti ya namna ya kunufaika na fursa hizo.

Alisema ifikapo mwaka 2020 sekta ya viwanda inatakiwa kuchangia katika pato la taifa kwa asilimia 15 ambapo kwa sasa inachangia chini ya asilimia 10 na pia iweze kutoa ajira zinazotokana na viwanda kwa asilimia 40.

Alisema Watanzania wengi hawajui namna ya kufanya biashara nje ya nchi na wengi wamekuwa wakibahatisha na wakati mwingine kuwasababishia hasara iliyo kubwa, hivyo kuandikwa kwa vijarida vyenye kutoa maelekezo ya namna ya kufanya biashara ili wengi waweze kunufaika.

“Ukiwa na utaalamu katika biashara usikubali kukaa nao, utolewe kwa wadau ili nao waandike majarida ili kusiwepo muda wa wafanyabiashara kufanya majaribio katika kufanya biashara,” alisema Mwijage na kusema anawaruhusu wafanyabiashara kuwa na tabia ya kunakili na kukariri kwa waliowazidi kibiashara kwa lengo la kuboresha bidhaa nchini.


Hata hivyo, alisema serikali inatambua sekta binafsi nchini kuwa ndio mhimili mkubwa wa ujenzi wa uchumi wa viwanda, na katika malengo matatu ya uchumi a viwanda ni pamoja na kuzalisha ajira, kuzalisha bidhaa zenye ubora na kuwezesha ukusanyaji wa kodi.

Kwa upande wake, Mshauri wa Masuala ya Biashara, Salum Awadh alisema ushiriki wa Tanzania katika kuuza nje ya nchi bado ni mdogo na hilo linatokana na kuwa na uelewa mdogo ambapo inauza kwa asilimia saba. Kuhusu masoko makuu ambayo hupokea bidhaa za Tanzania aliyataja kuwa ni India Afrika Kusini, China, Japan na Kenya.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link