Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Brazil Nchi Mhe. Carlos Alfonso Puente, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Habari Leo
MABALOZI wa Brazil na Kenya nchini wameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa mipango yake madhubuti ya kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ikiwa ni pamoja na kununua ndege mpya za shirika hilo.
Aidha, mabalozi wa nchi hizo wamesema hatua hiyo ya kuliimarisha shirika hilo itasaidia kukuza utalii na pato la taifa sambamba na kulifanya shirika hilo kuwa bora katika utoaji wa huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchini.
Balozi wa Brazil nchini, Carlos Alfonso Puente na Balozi wa Kenya hapa nchini, Chirau Ali Makwere wametoa pongezi hizo mara baada ya kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kenya kupitia shirika lake la Kenya Airways ambalo lilianza kufanya kazi zake mwaka 1977 baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki sasa kampuni hii inatoa huduma barani Afrika, Ulaya na India na ina safari nyingi za ndege nje ya Afrika kuliko kampuni yoyote barani Afrika.
Balozi wa Brazil, Puente amesema kutokana na nchi hiyo kuwa ni miongoni mwa nchi kadhaa duniani zenye viwanda vya kutengeneza ndege, hivyo serikali ya Tanzania ina nafasi nzuri ya kununua ndege nchini Brazil, hasa kulingana na mahusiano mazuri na ya muda mrefu yaliyopo kati ya nchi hizo mbili.
Kutokana na mwito, Makamu wa Rais ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wa nchi ya Brazil kuja nchini kutangaza bidhaa wanazotengeneza hasa ndege kama hatua ya kuimarisha uhusiano wa biashara kati ya Brazil na Tanzania.
Makamu wa Rais amewapongeza wawekezaji kutoka Brazil kwa kupiga hatua kubwa katika uzalishaji wa sukari na Tanzania ni moja ya nchi yenye maeneo mazuri kwa ajili ya uwekezaji hivyo amewakaribisha kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza katika sekta hiyo.
Balozi Puente amesema serikali ya nchi hiyo imeanzisha mradi unaolenga kusaidia uzalishaji bora wa pamba katika mikoa ya kanda ya ziwa mradi ambao utagharimu dola za Kimarekani milioni sita kwa miaka nne nchini.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais katika mazungumzo yake na balozi wa Kenya amesisitiza kudumisha na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili hasa katika uimarishaji wa biashara na uwekezaji na amewaasa watanzania kuchangamkia fursa ya kufanya biashara.
Wakati huo huo, Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Denmark nchini, Hebogand Jensen ambaye amemweleza Makamu wa Rais nia ya nchi hiyo kuwa na ushirikiano katika kujenga kiwanda kikubwa cha mbolea wilayani Kilwa mkoani Lindi.
Balozi huyo amesema ana imani kiwanda hicho kitakachojengwa nchini kitakuwa na uzalishaji mkubwa na kutoa ajira kwa wananchi wengi.
Makamu wa Rais alimhakikishia kuwa serikali katika kuelekea kwenye uchumi wa viwanda imeweka mazingira mazuri kwa ajili ya wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali nchini kama hatua ya kukuza uchumi wa nchi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Balozi wa Denmark Nchi Mhe. E. Hebogand Jensen, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), Mhe. Maniza Zaman, mara baada ya kumaliza mazungumzo,Ikulu jijini Dar es Salaam.