Anwani za Makazi kuwa Msingi wa Utambuzi wa Kila Mwananchi
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi (kushoto) akiongea na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bi. Mariam Mtunguja, baada ya kuwasili ofisini kwake mkoani humo kwa ajili ya kufungua semina ya kuwajengea uwezo viongozi wa Mkoa huo kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mbaraka Mwinshee leo Januari 19, 2022.
Na Prisca Ulomi, WHMTH, Morogoro
Serikali imejikita kutekeleza mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi nchi nzima kwa
lengo la kuibadilisha Tanzania kuwa ya kidijitali kwa kuwa anwani za makazi na postikodi
ni msingi wa utambuzi wa kila mwananchi.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape
Nnauye ambaye amewakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi wakati
akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kwa viongozi, watendaji na wataalam wa Mkoa
wa Morogoro kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi.
Dkt. Yonazi amesema kuwa anwani za makazi na postikodi ni msingi wa utambuzi ili kila
mwananchi aweze kutambuliwa pale alipo ambapo nia ya Serikali ni kuihakikisha kuwa
kila mtaa, barabara, inakuwa na jina la mtaa na kila nyumba inakuwa na namba ya
nyumba
Vile vile, ameitaka Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro kusimamia utekelezaji wa mfumo
huu ili ifikapo Mwezi Mei mwaka huu jambo hili liwe limekamilika kwa kuwa utekelezaji
wa mfumo huu utaiwezesha Serikali kuwa na sensa bora ya watu na makazi
inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.
Ameongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inayoratibu jambo hili, imeelekeza taasisi zote za
Serikali nchi nzima zinatekeleza mfumo huu wamiliki wote wa majengo na nyumba nao
waweke namba za nyumba kwenye nyumba na majengo yao na wataalam wote
waliojengewa uwezo watumike vizuri kutekeleza mfumo wa anwani za makazi na
postikodi na jambo hili liwe ajenda kwenye vikao.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bi. Mariam Mtunguja akizungumza kwa niaba ya
Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela amesema kuwa kimsingi tumechelewa kutekeleza
mfumo huu wa anwani za makazi, ila kwa kuwa viongozi mtajengewa uelewa, ni
matumaini yangu kuwa kwa pamoja tutashirikiana na wataalam wetu kutekeleza jambo
hili kwenye maeneo yetu ndani ya muda uliopangwa na niahidi kuwa Mkoa wa
Morogoro hatutawaangusha Wizara.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi, amesema kuwa mfumo wa anwani za makazi na postikodi
ni moja ya aina ya mawasiliano kama zilivyo aina nyingine za mawasiliano na mfumo huu
unahusisha eneo husika ambapo utamuwezesha mwananchi kutoka sehemu moja
kwenda sehemu nyingine; utarahisisha shughuli za kiuchumi, kijamii na utawala
Wakitoa salamu za shukrani kwa niaba ya viongozi wengine, Mwenyekiti wa CCM Wilaya
ya Morogoro Mjini Fikiri Juma, amesema kuwa viongozi watoe majina ya mitaa ndani ya
siku moja ili kufanikisha utekelezaji na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal
Kihanga amesema watahamasisha wananchi kununua vibao vya nyumba ili kufaniisha
uwekaji wa mfumo wa anwani za makazi kwenye Mkoa huo
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari