Tume ya Madini imekabidhiwa magari saba kati ya magari 40 yanayotarajiwa kutolewa na Serikali kama moja ya mikakati ya kuboresha mazingira ya ukusanyaji wa maduhuli kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini nchini.
Akizungumza
kabla ya kuzindua magari hayo leo tarehe 21 Februari, 2022 Waziri wa
Madini, Dkt. Doto Biteko mbali na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa magari hayo yatatumika
kama kichocheo cha ukusanyaji wa maduhuli kwenye shughuli za uchimbaji
na biashara ya madini.
Ameongeza
kuwa, Serikali itaendelea kununua vifaa vingine kama vile mashine za
kupima madini kwenye masoko ya madini na kusimamia kwa karibu shughuli
za madini ili kuhakikisha Serikali inapata mapato yake stahiki.
Aidha,
amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha magari yanatunzwa na
kuendelea kuchapa kazi kwa ubunifu mkubwa ili kuhakikisha lengo la
kukusanya shilingi bilioni 650 kwa Mwaka wa fedha 2021/2022 linafikiwa
ifikapo mwezi Juni mwaka huu.
Katika
hatua nyingine akizungumzia mikakati iliyowekwa na Wizara ya Madini
kwenye udhibiti wa utoroshaji wa madini, Dkt. Biteko amesema kuwa
mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuongeza maafisa kwenye usimamizi wa
shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.
Waziri Biteko amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa kufuata sheria na kanuni za madini na kusisitiza kuwa Serikali haitamwonea huruma mtu yeyote ayakayebainika anatorosha madini.
Wakati
huohuo Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula sambamba na
kuishukuru Wizara ya Madini kwa ununuzi wa magari kwa ajili ya kutumiwa
kwenye shughuli za madini amesema kuwa magari yatarahisisha kwa kiasi
kikubwa utendaji kazi kwa kufika maeneo yasiyofikika kirahisi.