ASILIMIA 26 YA WATU WAZIMA
WANASHINIKIZO LA JUU LA DAMU.
Na WAF- DOM
MGANGA
Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe amebainisha kuwa asilimia 26 ya
watu wazima wenye umri wa miaka kati ya 25 hadi 64 wana shinikizo la juu
la damu, hali inayosababishwa na mtindo wa maisha ikiwemo ulaji wa
vyakula vya mafuta mengi, matumizi ya pombe kupita kiasi na kutofanya
mazoezi.
Dkt. Sichalwe amebainisha hayo leo Aprili 13, 2022
wakati akifungua Mradi wa Healthy Heart Africa tukio lililofanyika
katika zahanati ya Makole Jijini Dodoma.
"Tumefanya utafiti
mwaka 2012 na kukagundua kwamba asilimia 26 ya watu wazima kati ya miaka
25 na 64 wana shinikizo la juu la damu na tatizo hili linatarajia
kuongezeka kwa kiasi kikubwa endapo hatutachukua hatua." Amesema Dkt.
Sichalwe.
Aliendelea kusema kuwa, tafiti zinaonesha kuwa, zaidi
ya asilimia 75% ya Wagonjwa hao wenye shinikizo la juu la damu hawatumii
tiba yoyote, huku akiweka wazi kuwa zaidi ya robo tatu kati yao hawajui
kama wana shinikizo la juu la damu.
Aidha, Dkt. Sichalwe
amesema kuwa, taarifa za utafiti zilizofanywa katika baadhi ya hospitali
za Rufaa zimebaini kuwa, wastani wa watu 19 katika kila watu 100
wanaolazwa kwa tatizo la shinikizo la juu la damu hufariki Dunia.
Sambamba
na hilo, ameweka wazi kuwa, hali ni mbaya zaidi kwa wagonjwa wa
kiharusi, ambapo katika kila watu 100 wanaolazwa, watu 39 wanafariki kwa
tatizo hilo la shinikizo la juu la damu, hivyo Serikali kupitia Wizara
ya Afya itaendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii ili kuongeza nguvu
za kupambano dhidi ya ugonjwa huo.
Mbali na hayo Dkt. Sichalwe
ameendelea kusisitiza juu ya kuzingatia utoaji huduma za afya kwa
kufuata miongozo, huku akisisitiza weledi na umahiri wakati wa kutoa
huduma ili kuepusha malalamiko yanayoweza kuzuilika kutoka kwa wananchi.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Rashid Mfaume
amewashukuru Wadau wa PATH kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika
mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Shinikizo
la juu la damu.
Amesema, Ukuaji wa miji, Maendeleo ya Sayansi
na teknolojia na mabadiliko ya mtindo wa maisha kwa kiasi kikubwa
yanaendana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza...