Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba |
Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem |
BENKI YA DUNIA YAAHIDI KUISAIDIA
ZAIDI TANZANIA KUFUFUA UCHUMI
Na Benny Mwaipaja, Washington DC
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishukuru
Benki ya Dunia kwa kuahidi kuisaidia Tanzania kukabiliana na athari za
kiuchumi zinazotokana na madhara ya UVIKO-19 na vita vinavyoendelea
baina ya Urusi na Ukraine.
Dkt.
Nchemba amesema hayo baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Makamu
wa Rais wa Benki ya Dunia, anayesimamia nchi za Kanda ya Mashariki na
Kusini mwa Afrika, Dkt. Hafez Ghanem, wakati wa Mikutano ya Kipupwe ya
Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), inayoendelea
Jijini Washington DC, Marekani.
Alimweleza
Kiongozi huyo kwamba Tanzania inafanya kila njia kuhakikisha kuwa
uchumi wake ulioathiriwa na matukio hayo unarejea katika hali ya kawaida
kwa kutafuta rasilimali fedha na kuzielekeza kwenye sekta
zitakazochochea ukuaji wa uchumi ikiwemo kilimo, na kuimarisha sekta
binafsi.
‘Tumepokea taarifa ya namna Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linavyokusudia kufufua uchumi wetu kwa kuwekeza kwenye sekta za uzalishaji ikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kuisaidia sekta binafsi hususan wajasiriamali wakiwemo wamachinga” alisema Dkt. Nchemba.
Dkt.
Nchemba alisema kuwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na
wataalam wa Benki ya Dunia, IMF na Benki ya Maendeleo ya Afrika,
watakutana ili kupitia maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi ili
utekelezaji wa miradi hiyo ianze mwaka mpya wa fedha 2022/2023.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba yuko nchini
Marekani akiongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye mikutano ya Kipupwe ya
Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF, ambayo
imewakutanisha Magavana wa Taasisi hiyo, mashirika yasiyo ya kiserikali
na sekta binafsi ambapo dhima kubwa ya mwaka huu ni kuchambua na kutoa
mapendekezo ya namna ya kufufua uchumi wa nchi ulioathiriwa na matukio
hayo.
#Kaziiendelee #royaltour