SERIKALI YATOA MILIONI 950
KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NA
ELIMU MSOMERA - HANDENI DC
OR TAMISEMI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Innocent Bashungwa amesema Serikali imetoa Milioni 500 kuanza ujenzi wa kituo cha afya Msomera katika eneo la mradi wa wakazi wanaotoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kuhama kwa hiari Wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga
Pia, Serikali imetoa Milioni 50 kwa ajili ya kupanua na kuboresha huduma za afya katika zahanati ya kijiji cha Msomera katika kata ya Misima Wilaya ya Handeni mkoa wa Tanga kinachotoa huduma kwa wananchi wasiopungua 10,000.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Aprili 15, 2022) wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua huduma za msingi za afya, elimu na miundombinu katika eneo la mradi wa wakazi wanaotoka eneo la hifadhi Ngorongoro wanahama kwa hiari katika kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni mkoani Tanga.
Bashungwa amesema tayali Serikali imetoa Milioni 400 kuanza ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari na bweni moja katika kata ya Misima katika kiijiji cha Msomera ili wanafunzi wasitembee mwendo mrefu kupata masomo ya elimu ya msingi na sekondari.
Aidha, Bashungwa amesema Serikali itaboresha shule ya Msomera kwa kuongeza vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na kuongeza walimu kutoka na upungufu uliopo kwa sasa katika shule hiyo.
Bashungwa amesema Serikali kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI itaongeza watumishi ambao ni Wauguzi, wataalam wa maabara na madawa ili ukarabati unaofanyika katika zahanati ya Msomera uendane na huduma nzuri zinazoendelea kutolewa hapo.
Vile vile, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TARURA kufanya upembuzi yakinifu wa Barabara inayotoka Handeni mjini hadi Kata ya Misima ili iweze kutengewa bajeti ya kuweka kifusi, kujenga makalavati na boksi kalvati katika maeneo korofi.