DKT. BITEKO ATATUA MGOGORO WA
WACHIMBAJI WADOGO CHAMWINO
Waziri
wa Madini Dkt. Doto Biteko ametatua mgogoro wa wachimbaji wadogo wa
madini ya dhahabu katika kijiji cha Nayu Kata ya Dabalo wilayani
Chamwino mkoa wa Dodoma.
Mgogoro huo ulio dumu kwa zaidi ya mwaka
mmoja ulitokea baada ya wachimbaji wadogo kugundua madini ya dhahabu
katika Mlima wa Nayu uliopo ndani ya Hifadhi za Misitu ambapo Mwekezaji
Sarehe Mohamed alitangulia kukata leseni ya uchimbaji mdogo wa madini
katika eneo hilo kabla ya wagunduzi.
Inaelezwa kuwa, kijiji cha
Nayu kina jumla ya leseni 16 ambazo Mwekezaji ana leseni 8 na wanakijiji
wana leseni 8 ambazo zinamilikiwa kihalali kwa kufuata Sheria na
Taratibu zilizowekwa na Serikali.
Akizungumza katika Mkutano wa
hadhara na wachimbaji wadogo wa madini, Dkt. Biteko amesema Wizara ya
Madini inatoa leseni za uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali, pale
inapotokea leseni ipo ndani ya Hifadhi za Misitu ni lazima mmliki apate
Kibali kutoka Mamlaka ya Uhifadhi wa Misitu Tanzania (TSF).
“Sisi Wizara ya Madini tunatoa leseni kwenye maeneo yenye madini lakini ukitaka kuchimba kwenye Hifadhi za Misitu lazima upate Kibali kutoka TSF ili uchimbe kwa utaratibu ambapo Wataalam wa Misitu watakagua eneo na watakupa Kibali cha Tathimini ya Athari za Mazingira ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama,” amesema Dkt. Biteko.
Aidha, Dkt. Biteko amemtaka Mwekezaji wa madini ya dhahabu katika kijiji hicho Sarehe Mohamed kujenga mahusiano mazuri na wanakijiji aliowakuta katika eneo hilo ili afanye kazi kwa ushirikiano.
Dkt. Biteko amesema, Rais wa Nchi hii Mhe. Samia Suluhu Hassan anataka kuona wachimbaji wadogo wa madini wananufaika na rasilimali zilizopo nchini, anataka kuwaona wachimbaji wadogo wanatoka kwenye uchimbaji mdogo kwenda wa kati na hatimaye kuwa wachimbaji wakubwa.
“Mwenyezi Mungu amewapa bahati ya kuwa na madini katika eneo lenu, niwaombe mchimbe madini haya kwa kupendana na kushirikiana, madini yawaunganishe acheni mambo ya kufitianiana na kuleteana majungu chimbeni kwa ushirikiano,” amesisitiza Dkt. Biteko.