Home » » OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAVISHIRIKISHA VYAMA VYA WAFANYAKAZI KUBORESHA MFUMO MPYA WA KUPIMA UTENDAJI KAZI WA WATUMISHI

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAVISHIRIKISHA VYAMA VYA WAFANYAKAZI KUBORESHA MFUMO MPYA WA KUPIMA UTENDAJI KAZI WA WATUMISHI

Written By CCMdijitali on Sunday, April 10, 2022 | April 10, 2022

 







 OFISI YA RAIS-UTUMISHI YAVISHIRIKISHA VYAMA VYA WAFANYAKAZI KUBORESHA MFUMO MPYA WA KUPIMA UTENDAJI KAZI WA WATUMISHI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema, ofisi yake imevishirikisha Vyama vya Wafanyakazi ili kupata maoni na ushauri utakaoisaidia Serikali kupata mfumo mpya mzuri wa kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma utakaochukua nafasi ya mfumo wa awali wa OPRAS ambao umebainika kuwa na mapungufu wakati wa kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma.


Mhe. Jenista amesema hayo jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha ofisi yake na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi kilichoandaliwa kwa lengo la kupata maoni ya wadau yatakayoboresha mfumo mpya wa Usimamizi wa Utendaji Kazi kwa watumishi wa Umma (Public Employees Performance Management Information System-PEPMIS) ambao utaanza kutumika rasmi kuanzia mwezi Julai, 2022.

Mhe. Jenista amesema, wakati ofisi yake iko katika hatua za mwisho kukamilisha mfumo huo mpya wa kupima utendaji kazi wa Watumishi wa Umma, aliona kuna ulazima wa wadau kupitishwa kwenye mfumo huo na ndio maana alielekeza watendaji wa ofisi yake kuandaa kikao kazi na Viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi ili kupata maoni ya kuuboresha.

“Tushaurini vizuri ili tupate mfumo bora wa kupima utendaji kazi wa watumishi ambao utaliwezesha taifa kuwa na Watumishi wa Umma wanaowajibika bila kushurutishwa kama ambavyo Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza mara kwa mara,” Mhe. Jenista amesisitiza.


Mhe. Jenista amesema, dhamira yake ya muda mrefu ni kutamani kuona Watumishi wa Umma wanafanya kazi muda wote wa kazi na ikitokea mtumishi anakosa kwenda kazini kwa sababu yoyote ile ahuzunike kwa kitendo hicho.

Ameongeza kuwa, Serikali inatamani mfumo huo mpya uwe na uwazi wa kutosha katika usimamizi wa Watumishi wa Umma, uwe ni mfumo ambao utaondoa kabisa upendeleo, uonevu na upime utendaji kazi wa watumishi kwa haki ili kuendana na dhamira ya Mhe. Rais ya kuujenga Utumishi wa umma unaowajibika kwa hiari.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link