MAJALIWA AZINDUA VITUO VINNE VYA
KURUSHA MATANGAZO YA REDIO YA
TBC TAIFA NA TBC FM RUANGWA
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa amezindua vituo vinne vya kuongeza usikivu wa redio za TBC Taifa na TBC FM vilivyopo Ruangwa (Lindi), Ludewa (Njombe), Mlimba (Morogoro) na Ngara (Kagera) ambapo tukio la uzinduzi limefanyika Ruangwa mkoani Lindi
Akizungumza katika uzinduzi huo Aprili 14, 2022, Mhe. Majaliwa amevitaka vyombo vya habari nchini kuendelea kuuhabarisha umma kwa kuweka mbele uzalendo, utaifa na kujali maslahi ya nchi kwa kulisemea Taifa la Tanzania ndani na nje ya nchi Waziri Mkuu Majaliwa ametoa maelekezo kwa wanahabari nchini kufanya kazi zao za kuuhabarisha umma kwa weledi mkubwa kwa kufanya utafiti wa kina wa habari wanazozitoa ili kuepeka utoaji wa taarifa chonganishi au za kuidharaurisha nchi kwani kwa kufanya hivyo ni kuidharaurisha tasnia ya habari.
Aidha, ameielekeza Wizara inasosimamia Sekta ya Habari nchini kuhakikisha maslahi na mikataba ya wanahabari kutoka kwa wamiliki wa vyombo vya habari nchini, kuendelea kusimamia mitandao ya kijamii pamoja na kuhakikisha uhuru wa wanahabari unalindwa kwa kuzingatia maadili na miongozo ya tasnia ya habari Kwa upande wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amezipongeza taasisi zilizo chini ya Wizara yake za Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kutoa ruzuku ya shilingi Bilioni 3.1 kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ikiwa ni utekelezaji wa mpango wa tatu wa kuongeza usikivu wa TBC Taifa na TBC FM katika maeneo mbalimbali nchini
Waziri Nape amezipongeza taasisi za UCSAF na TBC kwa ushirikiano mzuri katika kuhakikisha umma wa watanzania unapata habari za ukweli na uhakika, lakini pia ametumia fursa hiyo kulipongeza Bunge la Tanzania kwa kurudisha Bunge mubashara ambapo kwa kufanya hivyo ni hatua kubwa ya kulinda uhuru wa vyombo vya habari nchini
Kwa upande wa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema mfuko huo umefadhili miradi ya kuongeza usikivu katika maeneo 13 nchini na kati ya hivyo miradi minne ndio imezinduliwa na mingine inaendelea kutekelezwa lengo likiwa ni kuhakikisha watanzania wote wanapata taarifa kupitia redio za ndani ya nchi.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba amesema kuwa kuna miradi mingi inaendelea ya kuongeza usikivu ambayo ikikamilika usikivu utakuwa kwa asilimia 83, kutoka asilimia 50 ya mwaka 2016, aidha, kwa sasa baada ya uzinduzi wa vituo hivyo nne usikivu wa TBC kwa sasa ni asilimia 70.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.