Na Mwandishi wetu, Dar
Uongozi
wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
umewaelekeza mabalozi kufanya kazi kwa bidii na weledi pamoja na kuweka
maslahi ya Taifa mbele katika utekelezaji wa majukumu yao.
Maelekezo
hayo yametolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Balozi Liberata Mulamula pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara
Balozi Joseph Sokoine wakati walipokutana na mabalozi wanne walioapishwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
tarehe 10, 2022. Uomngozi wa Wizara umekutana na mabalozi hao katika
Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Mabalozi
hao ambao ni miongoni mwa Mabalozi 23 walioteuliwa na Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Mei 22, 2021, wamekabidhiwa majukumu mbalimbali ya Wizara kwenye ngazi ya ukurugenzi.
Akiwaasa
Mabalozi hao, Waziri Mulamula alisisitiza kwamba Wizara ya Mambo ya Nje
ni kiungo muhimu kati ya Serikali na dunia hivyo mawasiliano ya ndani
na nje ya Wizara yafanyike kwa weledi na wakati kwa kuzingatia viwango
vya taifa na kimataifa. “Hii itasaidia sana kuendeleza diplomasia ya
Tanzania hususan wakati huu ambapo Mheshimiwa Rais amefungua nchi kwenye
nyanja zote” alisema.
Waziri
Mulamula aliongeza kuwa matarajio ya Mheshimiwa Rais kwa kuwaapisha
Mabalozi vijana ni kwamba wataimarisha utendaji kazi wa Wizara kuendana
na kasi yake, hivyo ni muhimu kuchapa kazi bila urasimu. “Pale ambapo
mnaweza kuweka ubunifu, fanyeni hivyo, leteni mawazo mapya milango yetu
ipo wazi wakati wote ili tupige hatua”
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara aliongeza kuwa Mabalozi hao watapangiwa majukumu
mengine ya kutoa mihadhara kwenye Chuo cha Diplomasia kwa watumishi
wapya lakini pia Mabalozi hao wawe kiungo baina ya Taasisi zilizo chini
ya Wizara na Taasisi nyingine Serikalini kama vile Chuo cha Diplomasia
(CFR) na Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC)
Kwa
mujibu wa viongozi hao, vyeo vya mabalozi hao ni: Mkurugenzi wa Idara
ya Ushirikiano wa Kimataifa (Director of Multilateral Cooperation),
Balozi Macocha Tembele, Mkurugezi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
(Director of Government Communication) Balozi Mindi Kasiga, Mkurugenzi
Kazi Maalum (Ambassador Special Duties), Balozi James Bwana pamoja na
Mkufunzi Mwelekezi Mwandamizi (Senior Directing Staff - Foreign) wa
Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC) Balozi Noel Kaganda.
Mabalozi wakisikiliza na kufuatilia maelekezo ya Uongozi wa Wizara (hawapo pichani) |
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Joseph Sokoine katika picha ya pamoja na Mabalozi mara baada ya kumaliza kikao |