WAZIRI MABULA AONYA WANAOTUMIA HISANI YA RAIS
KUVAMIA MAENEO YA HIFADHI
Na Munir Shemweta, WANMM MUSOMA
Waziri wa ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametoa onyo kwa wananchi wanaotumia hisani ya Rais Samia Suluhu Hassan kuvamia maeneo ya hifadhi yaliyomegwa na kurejeshwa kwa wananchi kutokana na kuwa na migogoro ya matumizi ya ardhi.
"Na nitoe tahadhari kumekuwa na tabia leo serikali inakumegea halafu kesho unategemea tena utamegewa, hapatakuwa na kubadilisha mipaka au kumega tena maeneo yaliyotolewa, kilichofanyika ni hisani ya mhe Rais Samia kuweza kuridhia lifafanyike jambo hilo lakini siyo ada kila watu wakihitaji wanamegewa" alisema Dkt Mabula.
Timu ya Mawaziri wa Wizara za kisekta ikiongozwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi iko katika awamu ya pili ya ziara kwenye mikoa mbalimbali nchini kupeleka mrejesho wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975.
Alisema, kinachohitajika kwa maeneo yote yaliyomegwa kwa ajili ya shughuli za wananchi ni kuandaliwa mpango wa matumizi mazuri na jukumu la mikoa ni kuhakikisha mipango ya matumizi bora ya ardhi inaandaliwa kwa maeneo yote yaliyomegwa.
Akizungumza na uongozi wa mkoa wa Mara tarehe 9 April 2022 wilyani Musoma Dkt Mabula ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta alisema, mkoa wa Mara pekee ulikuwa na vijiji 19 na mtaa mmoja vyenye migogoro ya matumizi ya ardhi na kubainisha kuwa vijiji 19 katika mkoa huo vitaendelea kubaki na kufanyiwa marejeo huku mtaa mmoja ukifanyiwa tathmini.
Sehemu kubwa ya migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 ni uvamizi wa maeneo ya hifadhi, mashamba, ranchi, vyombo vya usalama, mapori ya akiba na vyanzo vya maji ambapo uvamizi huo umeleta changamoto kubwa inayofanyiwa kazi na Mawaziri wa Wizara za Kisekta.
Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, kazi inayofanyika katika kutafuta ufumbuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ni pamoja na kubadilisha maeneo ya hifadhi yaliyopoteza sifa, kurekebisha mipaka kati ya hifadhi za misitu, wananchi na wanyama ambako kuna muingiliano ili kuweka alama zitakazoonekana ambazo kila mmoja ataheshimu.
Kwa upande wao, Mawaziri wa Wizara za kisekta walisisitiza umuhimu wa uongozi wa mkoa kuanzia ngazi za chini hadi juu kuhakikisha unasimamia vyema sheria ili maeneo ya hifadhi yasivamiwe tena sambamba na kutilia mkazo uhifadhi wa mazingira na vyanzo vya maji sambamba na kuwepo mipango ya matumizi bora ya ardhi.
‘’ Elimu ya utunzaji vyanzo vya maji itolewe kwa wananchi kwa kuwa wananchi wamekuwa wakifanya shughuli kwenye vyanzo maji na hivyo kuathiri vyanzo hivyo na wakati mwingine kuvikausha hasa nyakati za kiangazi’’ alisema Mhandisi Marypricsa Mahundi.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Khamis Chillo alitaka wananchi kupewa taaluma ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira ili kuepuka uharibifu wa mazingira.
‘’Wananchi waelimishwa namna bora na sahihi ya matumizi ya ardhi kwa kuwa kuna shughuli nyingi za kibinadamu zinazofanywa katika ardhi na inawezekana zinafanyika kutokana na watu kutofahamu matumizi sahihi ya ardhi lengo letu ni kupunguza migogoro ya ardhi’’ alisema Chillo.
Naye Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde alisema, utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi utasababisha baadhi ya maeneo kutengwa kuwekewa mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kusaidia kupunguza changamoto za ardhi.
Mary Masanja aliwaambia viongozi wa mkoa na wilaya wa mkoa wa Mara kuwa, maeneo yanayomegwa kwa ajili ya wananchi yalikuwa sehemu ya maeneo yaliyohifadhiwa na kusema kuwa, wananchi wajiandae kukutana na changamoto za wanyama na kuwataka viongozi kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuishi maeneo hayo.
-----------MWISHO--------------