Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa amesema hayo leo wakati akifungua maadhimisho ya 19 ya siku ya wahandisi nchini ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria ya kuwawezesha wazawa katika ujenzi wa miradi ili kunufaika kiutalaamu, kiuzoefu na kiuchumi.
“Wahandisi ndio nguzo muwe na weledi na umakini katika kusimamia miradi ili iwe bora yenye gharama nafuu na inayokamilika kwa muda uliopangwa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ameaigiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), kuchukua hatua stahiki za kisheria na za haraka kwa makampuni ya kihandisi, Taasisi na wahandisi wasio waadilifu.
Amesema serikali itaendelea kutekeleza miradi mingi ya kimkakati katika kujenga miundombinu na uchumi wa nchi hivyo ni jukumu la wahandisi kuitumia fursa hii muhimu kujenga Taifa lao.
Ameitaja baadhi ya miradi ambayo ujenzi wake unaendelea kuwa ni ujenzi wa reli ya SGR, Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere, Bandari za Dar es salaam,Tanga na Mtwara, miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara, viwanja vya ndege, maji na umeme.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewapongeza na kuwashukuru wahandisi kwa kujenga miundombinu mingi na ya kisasa jijini Dodoma ikiwemo reli, barabara, maji na majengo pia amewataka kuzidi kujenga uaminifu ili waweze kuaminika na kupewa kazi zaidi.
Aidha, amewakaribisha kuangalia fursa za uwekezaji katika mkoa wa Dodoma ili kuuwezesha kuwa na hadhi ya makao makuu ya nchi.
Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Mhandisi Balozi Aisha Amour, amesema maadhimio yote yanayotolewa kwenye maadhimisho hayo yatafanyiwa kazi kwa wakati ili kuendeleza na kuleta tija katika sekta zinazohusu wahandisi nchini.
“Tumejipanga kuhakikisha kazi nzuri zinazofanywa na wahandisi zinaendelezwa na kuhakikiwa ili ziwe kwenye ubora unaokubalika wakati wote”, amesema Balozi Aisha.