Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier akiweka shada la maua katika kaburi la walilozikwa mashujaa wa Vita vya Maji Maji |
Serikali ya Ujerumani imeahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuboresha Makumbusho ya Majimaji ili kuhifadhi kumbukumbu sahihi kwa ajili ya wakati huu na kwa vizazi vijavyo.
Ahadi hiyo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier alipotembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji Songea Mkoani Ruvuma.
Mhe., Dkt. Steinmeier amesema Ujerumani ipo tayari kufanya uchambuzi na mchakato wa historia ya vita vya Maji Maji kwakuwa kilichotokea zamani hakipaswi kusauhilka na mtu yoyote.
“Ili kuweka kumbukumbu sawa kwa sasa na kwa wakati ujao, Ujerumani tunaahidi kushirikiana na Tanzania kuboresha makumbusho hii,” alisisitiza Mhe. Rais Steinmeier.
Mhe. Dkt. Steinmeier alisema Ujerumani inatamani kufanya uchambuzi na mchakato wa historia ya ‘Vita vya Maji Maji’ na kuongeza kuwa mchakato huo utahusisha vijana, wanafunzi wa shule na vyuo vikuu, wasomi na wataalamu wa hifadhi na sehemu za kumbukumbu.
“Mwaka 2024, Ujerumani ina mpango wa kufanya maonesho kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa ya Tanzania, maonesho hayo yatajulikana kwa jina la “Historia ya Tanzania”, alisema Mheshimiwa Steinmeier.
Awali Waziri wa Sanaa Utamaduni na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro (Mb.) alisema historia ya Tanzania na Ujerumani ina sura mbili tofauti. Alifafanua kuwa sura ya kwanza ni kuhusu vita waliyopigana babu zetu na sura ya pili ni yale mazuri yaliyofanywa na Serikali ya Ujerumani Kama vile kujenga shule, hospitali na kutoa huduma nyingine za kijamii.
“Muhimu zaidi ni kukumbuka na kusahau yaliyopita na kuendelea kudumisha uhusiano mzuri uliopo na kusonga mbele kwa kuleta maendeleo kati ya mataifa yetu mawili, lakini pia katika mji wetu wa Songea ,” alisema Dkt. Ndumbaro
Dkt. Ndumbaro aliongeza kuwa Songea wanatamani kuona makumbusho ya kisasa ya ushirikiano kati ya Ujerumani na Tanzania yakijengwa Songea, “pia tunatamani Ujerumani itusaidie kuboresha chuo cha VETA Songea ili kuwawezesha vijana wetu kupata mafunzo mbalimbali,” alisema Dkt. Ndumbaro.
Waziri Ndumbaro pamoja na mambo mengine, ameiomba Serikali ya Ujerumani kushirikiana na Mji wa Songea kwa kuwawezesha kutembeleana, kushirikiana na kuendeleza utani kati ya Wangoni na Wajerumani.
Mheshimiwa Rais Stenmeier mbali na kutembelea Makumbusho ya Vita vya Maji Maji pia ametembelea Shule ya Msingi ya Majimaji.
Makumbusho ya Vita vya Maji Maji ni makumbusho pekee nchini Tanzania inayoonesha historia kubwa ya Vita vya Maji Maji katika harakati za ukombozi dhidi ya ukoloni wa Wajerumani.
Mheshimiwa Rais Stenmeier amehitimisha ziara yake ya Kikazi ya siku tatu nchini leo tarehe 01 Novemba 2023.
Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier akiwa amekaa na wanafunzi wa Shule ya Msingi Maji Maji wakati alipofanya ziara shuleni hapo |
Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier akiweka ua katika kaburi la Chifu Nduna |