Naibu Waziri Ofisi ya Makamo Muungano na Mazingira Khamis Hamza Chilo (wa tatu kushoto)Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Haji Shaaban Waziri (wa kwanza kulia ) Mdau wa maendeleo ya Jimbo la Uzini Lucia Mwaipopo (wa pili kulia) na Katibu wa App skills Foundation Tinnah Didas Masaburi wakisikiliza maelezo mafupi yanahusu Mazingira, utumiaji wa nishati sahihi ya kupikia na ufahamu wa dhana ya uchumi wa buluu kwa Sister Agnes Paulo (wa pili kushoto)wa parokia ya Kanisa la Katoliki na Chuo cha Utalii cha Machui. |
Na Bahati Habibu
Naibu Waziri Ofisi ya Makamo wa Rais Muungano na Mazingira na Mbunge wa Jimbo la Uzini Khamis Hamza Chilo amesema elimu kubwa inahitajika kwa Wananchi kuacha matumizi ya Mkaa na Kuni kwa matumizi ya kupikia hali itakayopelelekea utunzaji wa Mazingira.
Kauli hiyo ameitoa huko Machui wakati akizungumza na wananchi wa shehia ya machui mara baada ya kukamilika utafiti uliofanywa taasisi isiyo ya serekali ya up skills foundation kutoka Tanzania Bara unaohusisha matumizi ya nishati ya kupikia na ufahamu wa wananchi juu ya dhana ya uchumi wa buluuu.
Amesema wananchi wengi hawana uelewa wa matumizi sahihi ya nishati ya kupikia na dhana ya uchumi wa buluu kwa kuacha matumizi ya kuni na mkaa ambayo hupelekea uchafuzi wa Mazingira na kusababisha maradhi kwa wananchi.
Aidha ameeleza matumizi ya nishati ya gesi kwa kupikia majumbani itasadia kwa kiwango kikubwa utunzaji wa Mazingira kwa nchi kavu na bahari.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la hilo Haji Shaaban Waziri amesema kufanyika kwa utafiti huo katika kijiji cha Machui itasaidia kwa Serekali kufahamu matumizi ya nishati ya kupikia kwa wananchi wanaoishi vijijini pamoja na dhana ya uchumi wa buluu.
Aidha ameeleza Serekali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serekali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kuondosha matumizi ya kuni na mkaa na badala yake wananchi watumie nishati ya gesi kwa matumizi ya kupikia .
Amesema matumizi ya nishati ya gesi ya kupikia ni salama na huepusha maradhi yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa ikiwemo kifua kikuu na homa ya mapafu.
Nae katibu wa app skills foundation Tinnah Didas Masaburi amesema utafiti huo wanaoufanya unalenga kujua ufahamu wa jamii kuhusu dhana ya uchumi wa buluu na matumizi ya nishati ya kupikia.
Pia utafiti huo utaonesha ni kwa namna gani jamii inatambua njia ya utunzaji wa Mazingira na kutoa Elimu ya matumizi sahihi ya nishati isiyo na madhara kwa binaadamu.
Nao wananchi wa Shehia ya Machui wameushukuru uongozi wa Jimbo la Uzini kwa kuiteua Shehia yao kuwa sehemu ya utafiti huo ambao umewasaidia kufahamu njia sahihi ya utunzaji wa Mazingira na dhana nzima ya Uchumi wa buluu.
Utafiti huo umefanyika katika Shehia ua Machui kwa Mkoa wa Kusini Unguja, Shehia ya Matemwe Kigomani, Shehia ya Mkokotoni kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja na Shehia ya Mndo kwa Mkoa wa Mjini Magharibi.
Ujumbe wa App Skills foundation ukiongozwa na Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Haji Shaaban Waziri akisalimiana na Mwakilishi wa Jimbo la Matemwe na Mwenyekiti wa Kiwanda Mungu ndie hakimu cha kuchakata takataka na kuwa mbolea Sulubu Kidogo Amour huko Matemwe ujumbe huo ulifika hapo kwa lengo la kufanya utafiti wa utunzaji wa Mazingira, matumizi sahihi ya nishati ya kupikia na ufahamu wa wananchi juu ya dhana ya uchumi wa buluu.