Na. Mwandishi Wetu
Uwepo wa mawakala wa vyama vya siasa wakati wa
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ni kielelezo cha uwazi na ni
muhimu kwa kuwa mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo
kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele leo tarehe 06 Machi, 2025
wakati akifungua mafunzo ya watendaji wa uboreshaji wa Daftari wa mkoa wa Dar
es Salaam.
Jaji Mwambegele amesema licha ya umuhimu huo mawakala
hao wa vyama vya siasa hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa
utekelezaji wa majukumu yao vituoni.
“Wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura. Jambo hili ni muhimu kwani litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa za lazima,” amesema.
Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amesema Tume
imetoa kibali kwa asasi za kiraia 157 kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura na
kibali kwa taasisi na asasi za kiraia 42 kuwa waangalizi watakaoshiriki katika
zoezi la uboreshaji wa Daftari ambapo kati ya hizo, taasisi tisa ni za
kimataifa na 33 ni za ndani ya nchi.
Amewasisitiza watendaji hao kutoa ushirikiano kwa
taasisi, asasi na waangalizi waliopata vibali watakapofika kwenye maeneo yao
kwa kuwa ni wadau muhimu na akaongeza kuwa Tume itawapa vitambulisho kwa
urahisi wa kuwatambua.
Jaji Mwambegele amewataka watendaji hao kutekeleza
majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya
uandikishaji kwa kuwa vifaa hivyo vimenunuliwa kwa gharama kubwa na vinatakiwa
kutumika katika awamu ya pili ya uboreshaji wa Daftari.
“Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu. Aidha, mnapaswa kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza,” amesema.
Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya uboreshaji wa
Daftari mkoani Dar es Salaam ambao utaanza tarehe 17 hadi 23 Machi, 2025 ambapo
vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00
jioni.
Mwisho
--
Mroki Mroki
Online Reporter/Blogger
Mob: +255 755
373999
Email: mrokim@gmail.com.
Blog: https://mrokim.blogspot.
DODOMA, TANZANIA