Home » » Atimuliwa Big Brother

Atimuliwa Big Brother

Written By CCMdijitali on Tuesday, July 30, 2013 | July 30, 2013

Kabla ya kugombana na Elikem, Ijumaa iliyopita, Nando amekuwa na tabia ya kubeba vitu vya hatari mfukoni akiwa kwenye sherehe mbalimbali zilizokuwa zikifanyika ndani ya jumba hilo

 Nando

MSHIRIKI machachari katika mashindano ya Big Brother The Chase, Amil Khan maarufu kama Nando, juzi Jumapili usiku alitimuliwa kwenye jumba hilo baada ya kuingia na mkasi chumbani alipogombana na Elikem wa Ghana hali iliyowafanya waandaaji kuingiwa hofu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja Uhusiano wa Multichoice Tanzania, Barbara Kambogi alisema ofisi yake imepokea taarifa hizo na kwamba mwakilishi huyo wa Tanzania alivunja masharti ya mchezo huo kwa kuhatarisha uhai wa mshiriki mwenzake Elikem.

“Nando amekuwa na tabia ya kubeba vitu hatarishi mara kwa mara, waandaaji wa mashindano walituvumilia kwa mara ya kwanza alipokutwa na kisu kwenye sherehe ya Channel O mwezi uliopita, lakini baadaye amegombana na mwenzake anaahidi kumuua, ule mkasi aliobeba kwenda nao chumbani ni kithibitisho,” alisema Kambogi.

Kambogi alisema bado haijafahamika rasmi ni lini Nando atarejea nchini kwani kwa sasa lazima atafutiwe mwanasaikolojia ili aweze kurudishwa katika hali yake ya kawaida.

Kabla ya kugombana na Elikem, Ijumaa iliyopita, Nando amekuwa na tabia ya kubeba vitu vya hatari mfukoni akiwa kwenye sherehe mbalimbali zilizokuwa zikifanyika ndani ya jumba hilo.

Baada ya kukutwa na kisu mwezi uliopita kwenye sherehe ya Channel O, Biggie(kiongozi wa jumba) alimwita na kumpa onyo la kwanza, lililohusu ukiukwaji wa sheria za mashindano kwa kutembea na silaha.
Ijumaa iliyopita, Nando aligombana na Elikem na kupeana maneno makali. Hilo lilikuwa kosa la pili kwa Nando.

Kama haitoshi Nando alisema “  Najisikia kama nimchome kisu, mtu kama huyu anastahili kufa,” baadaye kamera zilimnasa Nando akichukua mkasi na kwenda nao chumbani kisha aliuweka chini ya mto wake, tukio hilo lilihatarisha usalama kwa Elikem.

Aliitwa katika chumba cha maulizo na kusomewa mashtaka yake matatu na kisha aliambiwa afungashe virago kwa ajili ya kutoka katika jumba hilo mara moja. Elikem naye alipewa onyo la kwanza na endapo atavunja kanuni na masharti ya mchezo huo atatolewa mara moja.

Big Brother alisema kuwa kitendo cha Nando hakistahili kuvumiliwa kwani kuendelea kubaki na mshiriki kama huyo ni kuhatarisha maisha ya washiriki wengine ndani ya jumba hilo.

Annabel kutoka Kenya na Sulu wa Zambia waliaga mashindano Jumapili usiku.

Mwaka 2011, Mtanzania Lotus Kyamba pia aliondolewa Big Brother kwa kumpiga mtu.

By HERIETH MAKWETTA
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link