Home » » Bongo Movie wanatamba kimuziki pia

Bongo Movie wanatamba kimuziki pia

Written By CCMdijitali on Tuesday, July 30, 2013 | July 30, 2013

Baby Madaha msanii aliyeibukia kutoka mashindano ya BSS na kuwa moja kati ya waigizaji wanaofanya vizuri katika fani zote mbili yaani muziki na filamu, kaigiza filamu za ‘Ray Of Hope’, ‘Nani’, ‘Desperado’ na nyinginezo.


 Masanja

KATIKA kujiongezea kipato zaidi au kulinda umaarufu wao usipotee katika jamii, baadhi ya wasanii wa filamu hapa  Bongo  wamejikita katika fani nyingine ya muziki.

Wasanii waliofanya hivyo ni wengi, japo si wote walioweza kushika chati ya muziki kwa umahiri.
Lakini wasanii wa filamu ambao wameingia katika uimbaji wamefanikiwa tofauti na wasanii wa muziki walioingia katika filamu. Jambo hilo linatoa mwanya kwa waigizaji kuamini kuwa wanaweza kuteka soko la muziki pia.

Wasanii wa filamu wanaoimba wameanza muda kidogo, wa kwanza kuingia katika muziki alikuwa Jackson Makwaya ‘Bambo’ ambaye alivuma na wimbo ‘Kitambi’.

Bambo alifanya hivyo baada ya kuwa nyota katika uigizaji kupitia kundi la Kaole Sanaa. Baadaye swahiba wake, Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’ naye akafuata nyayo.

Ukifuatilia kwa undani utagundua kuwa wasanii wengine wa filamu ambao wamekuwa wakifanya muziki, wanafanya hivyo kama kwa ‘kubipu’ kwani bado wanang’ang’ania filamu zao.

Tena wanaofanya hivyo ni Wachekeshaji (makomedi) ambao ni Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’, Hamis Mshangani ‘Mtanga’, Lucas Mhuvile ‘Joti’, Asha Boko, Gilliady Kahena ‘Masai Nyota Mbofu’, Makwaya ‘Bambo’, Martin Tin White, Maulid Ali ‘Mau Maufundi,’Alex Machejo ‘Bingwa wa Rivasi’ na Mwinshehe ‘Kingwendu’.

Wengine ni Isaya Mwakilasa ‘Wakuvanga’, Mohamed Abdalah James ‘Kinyambe’ na Silvester Mjuni ‘Mpoki’ ambaye wimbo wake ‘Sangazi’ umeshinda tuzo za Kilimanjaro.

Baby Madaha msanii aliyeibukia kutoka mashindano ya BSS na kuwa moja kati ya waigizaji wanaofanya vizuri katika fani zote mbili yaani muziki na filamu, kaigiza filamu za ‘Ray Of Hope’, ‘Nani’, ‘Desperado’ na nyinginezo.

Kati yao, wasanii ambao nyimbo zao zilishika chati ni Sharo Milionea (marehemu sasa). Aling’ara na nyimbo zake kama vile ‘Changanya Changanya’ na ‘Chuki Bure’.

Pia mchekeshaji Masanja Mkandamizaji naye anatamba kwa kuimba nyimbo za Injili na kuendelea kutesa katika fani ya uimbaji.

Albamu ya Isiah Mwakilasa ‘Wakuvanga’ inaitwa Kato na ina nyimbo nane, msanii huyo ni mmoja kati ya wanaounda kundi la Orijino Komedi.

Yeye pamoja na kutoa albamu, pia ameweza kutoa ajira kwa vijana wanaotembeza kuuza albamu hiyo kwa wananchi.

Marehemu Sharo Milionea baada ya kufanya vema katika uchekeshaji na kushiriki katika filamu ya Safari za Adili,  aliibuka na kutesa katika muziki hadi mauti yalipomkuta.

Wasanii wengine wa filamu wanaoimba ni pamoja na Simon Mwakipagata ‘Rado’, Rose Ndauka, Aunty Ezekiel, Dokii na  Mzee Mgari ambaye kaibuka hivi karibuni na wimbo ‘Dar Raha’.

Masanja Mkandamizaji yeye alitoa albamu ya Hakuna Jipya akiimba Injili na kufanikiwa kuwateka wapenzi wa muziki huo.

Mwigizaji mwingine anayeimba akitokea katika kundi la Scopion Girl ni Miliam Jolwa ‘Jini Kabula’. Msanii huyu akiwa na kundi hilo, alifanikiwa kurekodi wimbo wa ‘Mapenzi Nini’.

Dokii ambaye ni mwigizaji na mtayarishaji, ameigiza filamu nyingi kama vile ‘My Nephew’, ‘Money Transfer’ na ‘Sister wa Bush’, yeye alitumia ziara ya Rais wa Marekeni, Barrack Obama, nchini Tanzania kutoa kibao.

Wimbo huo ‘Welcome Obama’ ulipata chati kubwa wakati wa ziara hiyo hivi karibuni.

Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ameshiriki filamu kama ‘Tifu la Mwaka’, ‘Zawadi’ na nyinginezo na hakuna aliyeamini kama anaweza kutamba katika muziki pia.

Lakini majibu yamepatikana baada ya kuimba nyimbo za ‘Lawama’, ‘Dume Dada’, ‘Paka La Bar’ na ule wa ‘Nakomaa na Jiji’.

Msanii Snura Anton Mushi kaigiza filamu za ‘Hitimisho’, ‘Mfalme Seuta’, ‘Zinduna’ na nyinginezo, katika muziki pia ametamba na kibao cha ‘Shoga Yake Mama’ na sasa anatamba na wimbo ‘Majanga’.

Lakini hali ni tofauti kwa wasanii wa muziki walioingia katika filamu. Ni Hemed Suleiman pekee tu ndiye angalau ameweza kufanya vizuri. Hemed ameshiriki filamu nyingi na kuwa pacha wa msanii Yusuf Mlela.

Wasanii wa muziki waliowahi kuigiza ni Chege na Mh.Temba ambao wameshiriki katika filamu za ‘Dar Moro’ na ‘Papaa’.

Akina GK, AY, Juma Mchopa ‘Jay Mo’ waliwahi kuigiza katika filamu ya Girlfriend, marehemu Albert Mangwea na Dark Master nao walishiriki filamu ya Copy.

Pia kuna akina Izzo Business, Dully Skyes, Queen Darlin, Linah nao wameshiriki katika uigizaji, lakini bado hawajateka tasnia hiyo ya filamu.

By MYOVELA MFWAISA
Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link