Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akiweka jiwe la msingi la Tawi la CCM Mombasa kwa Mchina.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Tawi la CCM Mombasa kwa Mchina Nd. Ahmada Yahya Abdulwakil akitoa ufafanuzi wa ujenzi mbele ya Mlezi wa CCM Mkoa wa Magharibi Balozi Seif mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la Tawi hilo.
Wanachama wapya 79 wa CCM na Jumuiya zake wa Tawi la CCM Mombasa kwa Mchina wakila liapo mara baada ya kukabidhiwa kadi na Mlezi wa CCM Mkoa wa Magharibi Balozi Seif Ali Iddi.
Mlezi wa CCM Mkoa wa Maghribi Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika Picha ya pamoja na uongozi mzima wa Tawi la CCM Mmobasa kwa Mchina, Wilaya ya Dimani na Mkoa wa Magharibi mara baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la Tawi hilo.Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM
Balozi Seif Ali Iddi alisema wimbi la vijana wa vyama vya upinzani kuamua
kuvihama vyama hivyo na kujiunga na CCM ni dalili za umadhubuti wa chama hicho unaoonekana kuimarika kila
wakati.
Alisema chama cha Mapinduzi chenye sera na ilani imara inayokiwezesha kushinda kila
baada ya miaka mitano tokea kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa Tanzania
ndio kimbilio la watu wote wenye busara ya kutaka kujiunga na ulingo wa siasa.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Mlezi wa Mkoa wa Magharibi
Kichama alisema hayo mara baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Tawi la
Chama cha Mapinduzi Mombasa kwa Mchina Wilaya ya Dimani Mkoa wa Magharibi.
Alisema makundi ya wafuasi wa vyama vya upinzani wanaoamuwa
wenyewe kuvihama vyama vyao na kujiunga na Chama cha Mapinduzi ni muelekeo wa
ishara kwa CCM kuendelea kuongoza dola katika uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015.
Hata hivyo Balozi Seif aliwatahadharisha Viongozi na
Wanachama wa CCM wasikae na kubweteka na mawazo ya kushinda uchaguzi bila ya
sera na mikakati ya kujipanga vyema kwa ajili ya ushindi huo.
Aliwaomba wana CCM popote pale walipo nchini Tanzania
kuendelea kushikamana na kuacha majungu, fitna na makundi ili ushindi uwe rahisi zaidi ya chaguzi zote
zilizopita za mfumo wa vyama vingi hapa Nchini.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi, wanachama na wapenzi wa chama hicho waliojitolewa kwa
nguvu zao na kuhakikisha kwamba ujenzi wa Tawi la Mombasa kwa Mchina unasimama
imara.
Alisema licha ya kuungwa mkono na wapenzi na watu tofauti
katika ujenzi wa Tawi hilo lakini nguvu za ukamilishaji wa tawi hilo
zitaendelea kubakia mikononi mwa Viongozi pamoja na Wanachama wenyewe wa Tawi
hilo.
Aliutaka uongozi wa Mkoa wa
Magharibi kuwa na tahadhari ya uvamizi wa makaazi unaofanywa na baadhi
ya watu kwa lengo maalum la kuongeza nguvu za
kuimarisha vyama vya kisiasa katika kujiandaa kwa uchaguzi Mkuu ujao.
Balozi Seif akiwa pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliwakumbusha masheha na Wakuu
wa Wilaya nchini kuendelea kufuata
sheria za nchi ipasavyo ili kila mwenye haki yake anapata fursa bila ya vikwazo,ubaguzi wala itikadi za
kisiasa.
Alisema tabia ya baadhi ya watu zaidi wana siasa
kushindikiza masheha kutoa vibali kwa
wafuasi au vijana wao kwa kutaka kupatiwa vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi
wakati muda wa ukaazi wa vijana hao haujatimia ni kuvunja sheria za nchi.
“ Suala hili la kutishwa masheha na kulaumiwa Wakuu wa
Wilaya nililikemea nilipokuwa katika ziara yangu wiki hii Kisiwani Pemba. Na
hapa nalirejea tena kwa kuwakumbusha masheha na wakuu hao wa Wilaya kufanya
kazi zao kwa kujiamini “. Alisema Balozi Seif.
Aliwataka na kuwaasa vijana kujiepusha na ushawishi huo wa
wana siasa wa kutaka kuwalazimisha kufanya mambo yaliyo kinyume na sheria na
utaratibu wa Nchi.
Katika kuunga mkono ujenzi wa Tawi hilo la Mombasa Kwa
mchina Mlezi huyo wa Mkoa wa Magharibi Kichama Balozi Seif aliahidi kukamilisha
ukumbi wa Tawi hilo kwa kutoa mchango wa Jipsam, taa ,mafeni yote ukumbini hapo
pamoja na kusaidia Seti moja ya Jezi kwa
Timu kati ya timu 16 zilizomo ndani ya Tawi hilo .
Mapema akitoa Taarifa fupi ya ujenzi wa Tawi hilo Mwenyekiti
wa Ujenzi ambae pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Nd. Ahmada Yahya Abdulwakil alisema ujenzi huo ulioanza rasmi Tarehe 28
Septemba 2013 umekuja kufuatia wanachama hao kukosa ofisi ya kufanyia kazi zao za Kisiasa.
Nd. Ahmada alisema tawi hilo lenye ofisi zote zinazohitajika
zikiwemo za jumuiya za chama litakuwa na huduma za kisasa zinazokwenda na
wakati pamoja na ukumbi wa Mikutano
ambao utakodishwa kwa shughuli za kijamii ili kuliongezea mapato Tawi hilo.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ujenzi wa Tawi la CCM Mombasa
kwa Mchina aliwashukuru viongozi na wapenzi wote wa chama hicho waliojitolea
kuunga nguvu katika ujenzi wa Tawi hilo lenye hadhi ya chama chenyewe.
Katika hafla hiyo ya uwekaji wa jiwe la msingi la Tawi la
CCM Mombasa Kwa Mchina Balozi Seif alikabidhi kadi kwa wanachama wapya 79 wa chama cha Mapinduzi pamoja na Jumuia
zake wa Tawi hilo.
Ujenzi wa Tawi la
Chama cha Mapinduzi Mombasa kwa Mchina
hadi sasa umeshagharimu zaidi ya shilingi Milioni 45,100,000/- .
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
27/12/2014.