Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba akizungumza.
Na Mwandishi Wetu
NAIBU Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuongoza Tamasha Maalumu la 'Upendo wa Mama' linalotarajiwa kufanyika katika Kanisa la Rutheran Mabibo Extenal jijini Dar es Salaam na kushirikisha waimbaji wengi kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumzia tamasha hilo leo jijini Dar es Salaam, Rais wa taasisi ya Upendo kwa Mama Foundation yenye makao makuu yake mkoani Arusha, Injinia Carlos Mkundi alisema Naibu Waziri Nchemba ndiye mgeni rasmi wa Tamasha hilo maalumu ambalo pamoja na mambo mengine linafanyika kutambua mchango mkubwa wa mama kuanzia katika ngazi ya familia na jamii nzima.
Injinia Mkundi alisema tamasha hilo litakalofanyika Januari Mosi, 2015 chini ya uratibu wa Taasisi ya Upendo kwa Mama Faundation, litashirikisha waimbaji wa injili akiwemo Faraja Ntaboba kutoka Congo, Stella Joel, Ado Novemba, Jane Misso, Edson Mwasabwite wote kutoka jijini Dar es Salaam. Na Rose Molel, Helen Kigazi wote kutoka mkoani Arusha.
Injinia Carlos Mkundi na mwimbaji wa muziki wa injili ambaye naye atatumbuiza katika tamasha hilo, aliwataja waimbaji wengine ambao watashiriki katika tamasha ni pamoja na Mbunge, Matha Mlatta, Kwaya ya Mamajusi kutoka Moshi, mwimbaji Tumaini Njole, Messi Chengula na waimbaji wengine wengi.
"...Washiriki kila mmoja anaweza kuja na mamayake anayempenda pamoja na zawadi yake maalum, ambayo atamkabidhi wakati itakapotangazwa...kutakuwa na waimbaji wa muziki wa injili kutoka nje na ndani ya nchi ili kuleta mvuto zaidi tunawaomba wananchi wajitokeze zaidi kuja kutambua mchango wa mama na kuonesha upendo kwa mama zao," alisema Injinia Mkundi.
Akifafanua zaidi alisema Tamasha la Upendo kwa Mama litakuwa la bure na litaanza majira ya saa saba mchana siku hiyo na kuendelea hadi jioni litakapofungwa.
Aisema siku hiyo washiriki wanaombwa kuja na zawadi maalumu ambayo kila mmoja atamkabidhi mamayake anayempenda katika familia zao.
Rais wa Taasisi ya Upendo kwa Mama Faundation, Injinia Caros aliongeza kuwa lengo lingine ni pamoja na kuwatia moyo akinamama na kuwaonesha upendo juu ya kazi kubwa wanayoifanya katika familia zao na jamii kwa ujumla.
Alisema baada ya uzinduzi wa tamasha hilo kanisani hapo yataandaliwa matamasha mengine makubwa na kufanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaa pamoja na mengine katika mikoa mbalimbali.
Aidha aliongeza tamasha kama hilo pia lilifanyika mkoani Arusha Novemba 16, 2014 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeib na kuwashirikisha akinamama zaidi ya 40,000.