Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akizindua rasmi Bara bara ya pili ya Amani hadi Mtoni baada ya kukamilika awamu
ya mwisho ikiwa ni shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 51 ya
Mapinduzi ya Zanzibar.
Kulia ya Balozi Seif ni Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano
Zanzibar Mh. Juma Duni Haji na Naibu Wake Mh. Issa Ussi Gavu.
Balozi Seif akikata utepe kuashiria
uzinduzi rasmi wa bara bara ya amani – Mtoni akishindikizwa na Waziri wa
Miundombinu na Mawasiliano Mh. Juma Duni Haji kuilia yake na Naibu Waziri wa
Wizara Hiyo Mh. Issa Ussi. Na kushoto ya Balozi ni Afisa Uhusiano wa Wizara
hiyo Nafisa Madai.
Balozi Seif na Uongozi wa Wizara ya Maiundo mbinu na Mawasiliano wakikagua kwa miguu na baadaye magari bara bara ya Mtoni hadi amani.
Baadhi ya watendaji wa Wizara ya
Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa bara ara ya Mtoni Amani hapo uwanja wa Gara gara
Mtoni Kidatu.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alisema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar imefanikiwa vyema katika
uimarishaji wa mtandao wa Bara bara
Mjini na Vijijini na kufikia kilomita elfu 1,235.52 Unguja na Pemba tokea
kubadilisha mfumo wa ujenzi wa Bara bara hizo katika miaka ya 90.
Alisema mfumo huo wa ujenzi kwa upangaji mawe na kushindilia
kwa mkono umebadilika na kuingia mfumo wa kisasa unaotumia kifusi na kumalizia
kwa lami ya moto na baridi.
Balozi Seif alieleza hayo wakati wa hafla ya uzinduzi wa
Bara bara ya Pili ya Amani hadi Mtoni { Mkapa Road } ikiwa ni mwanzoni mwa
shamra shamra za maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 51 ya Mapinduzi
matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 zilizoanza rasmi Tarehe 2 Januari 2015.
Alisema Serikali ilichukuwa jitihada za makusudi katika
kuzijenga upya bara bara zake Mijini na Vijijini ambazo tayari zilikuwa
zimeharibika vibaya licha ya kazi hiyo kukumbwa na vikwazo tofauti ikiwemo
ufinyu wa upatikanaji wa fedha za ununuzi wa zana, vifaa pamoja na ulipaji
fidia.
Balozi Seif alisema kukamilika kwa ujenzi wa bara bara ya
Amani – Mtoni ni miongoni mwa hatua
muhimu za kuimarisha miundombinu itayowarahisishia wananchi usafiri kwa
kuzingatia kuwa bara bara ni kiunganishi kikubwa kinachotumiwa katika
kusafirisha huduma muhimu za Kiuchumi na Kijamii.
“ Hizi zote ni juhudi zinazochukuliwa na Chama cha Mapinduzi katika kutekeleza Ilani yake ya Uchaguzi kwa vitendo katika kuhakikisha Nchi ina bara bara bora na za kisasa, hii yote ni katika kuwaletea maendeleo wananchi wetu “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza watendaji wa
Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano katika kusimamia ujenzi wa Bara bara mbali
mbali hapa nchini ambapo wameweza kutekeleza vyema majukumu waliyopangiwa na
Taifa.
Balozi Seif alieleza kwamba haiba na uzuri wa Bara bara unategemea hali ya matunzo ya bara bara
husika. Hivyo aliwaomba wananchi na watumiaji wote kuzitunza bara bara wanazozitumia ili
zidumu na kuendelea kutumika kwa kipindi kirefu.
Alitoa wito kwa
madereva wote wa vyombo vya moto kutumia bara bara kwa uangalifu zaidi pamoja
na kufuata alama za bara barani zilizowekwa wakati wakiendesha vyombo vyao ili
kuepuka ajali za mara kwa mara ambazo zinaweza kuepukika.
Aliwaomba madereva hao kuachana na mtindo wa kuegesha gari
mbovu zinazodondosha mafuta na kuharibu bara bara sambamba na kuwa waangalifu
kwa gari hasa zile zinazobeba makontena zinazotumia mipira ya magongo
yanayopelekea uharibifu mkubwa wa bara bara.
Balozi Seif pia aliwakumbusha madereva kwenda mwendo mzuri
kama alama za bara bara zinavyoainisha ya mwendo wa kilomita 40 kwa saa na
kuepuka bara bara hiyo kufanywamakaburi ya watu wanaotembea kwa miguu na wale
wanaotumia vyombo vodogo vya ringi mbili.
Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano
Zanzibar Dr. Juma Malik Akil alisema ramani ya ujenzi wa bara bara ya Mtoni
hadi Kiembe Samaki ilikuwepo tokea awamu ya kwanza.
Dr. Malik alisema hatua za ujenzi wa bara bara hiyo zilianza
mapemba katika miaka ya 90 lakini zilikwama baada ya daraja lililojengwa
kuunganisha bara bara hiyo ambalo tayari lilikuwa limeshamikika kuvunjika.
Alisema ujenzi wa bara bara ya Amani hadi Mtoni yenye urefu
wa kilo mita 4 na upana wa mita nane kila njia mbili zilizokuwepo umekamilika
kwa awamu zote mbili na utasaidia kuondoa kiu ya wakaazi wa maeneo hayo
waliopata usumbufu wa usafiri kwa kipindi kirefu.
Alifahamisha kwamba
wahandisi wa ujenzi wa bara bara hiyo kutoka Idara ya ujenzi na Utunzaji
Bara bara { UUB } iliyopata ufadhili wa
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mfuko wa Bara
bara Zanzibar kwa gharama ya zaidi ya Shilingi Bilioni Nne imetenga njia maalum
ya watembeao kwa miguu.
Katibu mkuu huyo wa
Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar alieleza kwamba Serikali tayari
imeshajenga Bara bara zenye urefu wa Kilomita 704 kwa Unguja na Kilomita 531
kwa Pemba.
Dr. Malik alifafanua
kwamba hadi sasa tayari Mkoa wa Mjini Magharibi umeshawekewa miundombinu mizuri
ya bara bara kwa zaidi ya Kilomita 206 kati ya hizo Manispaa ya Mji pekee ina
kilomita 68, wakati bara bara kuu zina urefu wa kilomita 332, Vijijini Kilomita
544 na zile za mashambani zimefikia kilomita 270.2.
Akimkaribisha mgeni
rasmi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa
Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar Mh. Juma Duni Haji alisema licha ya bara
bara ya Mtoni Amani kusaidia kupunguza msongamano wa Bara bara kuu inayoingia
Mjini lakini matumizi yake yameongezeka na kuifanya kuwa na harakati zaidi.
Waziri Juma Duni
alieleza kwamba hatua za kulinda usalama wa wananchi itaimarishwa kufuatia
msongamano huo uliobeba magari makubwa hasa yale ya mchanga na mizigo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
3/1/2015.