Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd.
Abdullah Juma Abdullah akimtembeza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif baadhi ya maeneo yaliyowekwa makontena ndani ya Bandari hiyo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdullah Juma
Abdullah kuchukuwa hatua ya kuyapeleka TRA Makontena yote yaliyoshindwa kufuata
tataribu ambayo yanaleta msongamano ndani ya Bandari hiyo.
Mrundikano mkubwa wa makontena unaoonekana katika Bandari ya
Malindi ambapo baadhi ya wafanyabiashara wanashindwa kutoa makontena yao na
kuleta usumbufu kwa watendaji wa Bandari hiyo.
Balozi Seif alifanya ziara ya ghafla ndani ya Bandari hiyo ili kujionea hali halisi ya utendaji wa bandari hiyo.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Mrundikano Mkubwa wa Makontena uliopo hivi sasa katika
Bandari Kuu ya Malindi Mjini Zanzibar unaonyesha dalili ya kuzitia wasi wasi
baadhi ya meli kubwa za Kimataifa
zinazopanga kuleta mizigo yake katika nchi za Mwambao wa Afrika Mashariki.
Uchelewaji wa baadhi ya wafanyabiashara kuchukuwa makontena
yao Bandarini hapo ndio sababu kubwa inayochangia mrundikano huo usio wa lazima
endapo taratibu za sheria ya kibiashara zitachukuliwa kwa wakati.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
alifanya ziara ya ghafla katika Bandari ya Malindi kuangalia harakati za
Bandari hiyo na kujionea msongamano mkubwa wa Makontena ya wafanyabiashara
ambayo hadi sasa bado hayajachukuliwa wakati muda wa kukaa eneo hilo umepita.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Bandari Zanzibar Nd. Abdulla
Juma Abdulla alimueleza Balozi Seif kwamba baadhi ya wafanyabiashara wanasita
kutoa makontena yao kwa wakati wakilitumia eneo hilo kama sehemu ya kuweka
bidhaa zao wakiendelea kutafuta wateja wa bidhaa hizo.
Alisema tatizo hilo licha ya Uongozi wa Bandari kutoa
matangazo ya kuwataka wafanyabiashara hao wakamilishe taratibu zinazowahusu
lakini bado utekelezaji wake unakuwa wa
kusua sua.
Alisema Uongozi huo umekuwa ukiwasiliana na Mamlaka ya
Mapato Tanzania { TRA } ili
kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo ambalo limekuwa mzigo mkubwa kwa watendaji wa
Bandari hiyo.
“ Zipo taratibu za kisheria zilizowekwa kwa wafanyabaishara wanaochelewa kutoa mizigo yao Bandarini ambayo huipa uwezo Mamlaka ya Mapato Tanzania kupiga mnada kwa biadhaa zilizoshindwa kufuata utaratibu “. Alisema Nd. Abdulla Juma Abdulla.
“ Sisi tunazo kanuni na taratibu zinazotupa Mamlaka ya kuwatoza Dola kumi za Kimarekani kwa wafanyabiashara wanaochelewa kutoa Makontena yao katika muda waliopangiwa “. Alifafanua Nd. Abdulla.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa Bandari Zanzibar alimfahamisha
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba lipo tatizo jengine la uhaba wa vifaa
vya kazi Bandarini hapo kutokana na
ongezeko la mizigo inayoteremshwa pamoja na ufinyu wa nafasi za kuweka Makontena.
Nd. Abdullah alisema ipo nafasi ndani ya eneo la Bandari
ambalo linaweza kusaidia kuweka Makontena yanayoteremshwa kwenye Bandari hiyo
ambalo linaweza kusaidia kupunguza ufinyu wa maeneo ya maegesho ya Makontena.
Alisema tatizo kubwa
ni taratibu za Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar kutoa kibali cha kuruhusu
ujenzi katika eneo hilo ambalo limo ndani ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliomo
katika Hifadhi ya urithi wa Kimataifa kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la
Elimu, Sayansi na Utamaduni { UNESCO }.
Akitoa shukrani zake kwa kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa
na watendaji wa Shirika la Bandari Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Bandari kuyapeleka Mamlaka ya Mapato Tanzania {TRA } Makontena
yote yaliyoshindwa kukamilisha taratibu zilizowekwa.
Balozi Seif alisema Serikali imekuwa ikipokea lawama na malalamiko siku hadi siku kutokana na
harakati zilizopo Bandarini ambazo matatizo mengi husababishwa na watu
wasiopenda kufuata taratibu zilizowekwa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizishauri Mamlaka
zilazohusika na kazi hiyo kuhakikisha kwamba sheria zote za biashara zinafuatwa
na endapo yapo makontena yaliyoshindwa kulipiwa ushuru hatua za kupiga mnada
zichukuliwe ndani ya siku 40 ili kurejesha gharama zinazotumiwa katika kazi
hiyo.