Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi
akimkabidhi Tanuri la kuhifadhia taka taka Mkuu wa Kituo cha Afya Cha Kitope
Dr. Ameir Yunus Makame.
Mama
Asha Suleima akizungumza na baadhi ya watendaji wa Kituo cha Afya cha Kitope
mara baada ya kukabidhi Tanuri la kuhifadhia taka taka zinazokusanywa ndani ya
Kituo hicho.
Tanuri la kuhifadhi taka taka zinazozalishwa katika Kituo
cha Afya cha Kitope lililojengwa na kugharamiwa na Mbunge wa Jimbo la Kitope
Balozi Seif Ali ili na kuungwa Mkono na Halmashauri ya Wilaya ya Kaskazini “
B”.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Mama Asha Suleiman Iddi
amewakumbusha Wafanyabiashara na Wananchi kuendelea kuwa na utamaduni wa kulipa
kodi kwa wakati ili fedha zinazokusanywa na Halmashauri za Wilaya zao ziweze
kuongeza nguvu katika kusaidia kuiendeleza miradi yao ya maendeleo.
Alisema nguvu za baadhi ya Halmashauri hapa Nchini zinakuwa
ndogo kuunga mkono miradi ya Wananchi kutokana na baadhi ya wananchi hasa
wafanyabiashara kukweka kulipa kodi kitendo ambacho pia kinakosesha mapato
Serikali Kuu.
Mama Asha Suleiman Iddi alitoa kumbusho hilo wakati
akikabidhi tanuri la kuchomea taka taka { Placentar Pits } katika Kituo cha
Afya cha Kitope Kiliomo ndani ya Jimbo la Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Ujenzi wa Tanuri hilo uliogharamiwa na Mbunge wa Jimbo la
Kitope Balozi Seif Ali Iddi na kuungwa mkono wa Halmashauri ya Wilaya ya
Kaskazini “ B “ulifuatia ziara aliyoifanya Kituoni hapo Tarehe 3 Machi Mwaka
2013 na kuelezwa changamoto zinazokikabili Kituo hicho.
Mama Asha alisema uwepo wa Tanuri hilo ambalo ilikuwa kilio
cha muda mrefu kwa wafanyakazi wa Kituo hicho umelenga kuhifadhi mabaki ya taka
taka zinazozalishwa kituoni hapo ambazo kuachiwa kwake zingeweza kusababisha
maambukizo ya maradhi mbali mbali.
Alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwa juhudi anazoendelea kuchukuwa katika
kusaidia kuunga mkono miradi inayoanzishwa na Wananchi ndani ya Jimbo hilo.
Aliwatahadharisha Wananchi wa Jimbo hilo kujiepusha na choko
choko zinazoendelea kupenyezwa na baadhi ya watu ndani ya Jimbo hilo
zikielezkezwa zaidi kwa vijana kwani kuachiwa kwake zinaweza kuviza maendeleo
yaliyopatikana Jimboni humo.
Akitoa shukrani Mkuu wa Kituo hicho Dr. Ameir Yunus alisema
changamoto ya ukosefu wa Tanuri hilo ilikuwa ikiwapa wakati mgumu wafanyakazi
wa kituo hicho katika kukabiliana na taka taka zilizokuwa zikikusanywa ndani ya
Kituo hicho.
Dr. Yunus alisema changamoto ya ukosefu wa Tanuri hilo
ilikuwa ikiwapa wakati mgumu wafanyakazi wa Kituo hicho katika kukabiliana na
taka taka zilizokuwa zikikusanywa ndani ya Kituo hicho.
Mkuu huyo wa Kituo cha Afya cha Kitope aliwaomba akina mama
waja wazito wa Jimbo hilo na vitongoji vyake kukitumia kituo hicho katika
kupata huduma za afya pamoja na zile za waja wazito ili wawe na uhakika wa kujifungua
salama.
Dr. Yunus alifahamisha kwamba ule wakati wa akina mama
kwenda kituoni hapo na Majembe kwa ajili ya kupata huduma za uzazi umekwisha
kabisa baada ya kupatikana kwa Tanuri hilo.
Tarehe 3 Machi Mwaka 2013 Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi
Seif Ali Iddi alifanya ziara ya kukikagua Kituo cha Afya cha Kitope na
kutoridhika na mazingira aliyoyakuta ya Kituo hicho.
Aliwakumbusha wafanyakazi wa Kituo hicho kuzingatia usafi wa
mazingira yanayokizunguuka kituo hicho ili kuepuka maradhi yanayoweza kuwakumba
wagonjwa wanaofika kituoni hapo ambapo aliahidi kuwajengea Tanuri la kuhifadhia
taka taka.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
29/1/2015.