Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyepo kati kati waliokaa vitini akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa Mapitio ya Sekta ya Afya huko Zanzibar Ocean View Kilimani.
Kulia ya Balozi Seif ni Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Saleh Mohammed Jidawi, Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto Bibi Asha Abdullah na Kwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani hapa Zanzibar Dr. Adymichael Ghirmany.
Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bibi Halima Ali Maulid.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr, Saleh Mohammed Jidawi akitoa taarifa fupi kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Mapitio ya Sekta ya Afya unaofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani Mjini Zanzibar.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mh. Mahoud Thabit Kombo akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Kuufungua Mkutano wa Mapitio ya Sekta ya Afya Zanzibar.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani { WHO } Dr. Adymichael Ghirmany akitoa salamu za Taasisi za Kimataifa zinazotoa huduma Nchini Tanzania kwenye Mkutano wa Siku mbili ya Kimataifa wa Mapitio ya Sekta ya Afya Zanzibar.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Siku mbili wa Mapitio ya Sekta ya Afya Zanzibar unaofanyika Zanzibar Ocean View Kilimani MjiniZanzibar.Picha na – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Miundombinu inayoendelea kuchukuliwana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi wa Mawasiliano ya bara bara na huduma za maji safi na salama licha ya kuimarisha uchumi wa Taifa lakini pia inakwenda sambamba na ustawi wa Jamii.
Alisema Afya za Wananchi zitaendelea kuimarika iwapo upatikanaji wa huduma Bora za maji safi na salama pamoja na ufuatijiaji wa huduma za Afya kwa kutumia bara bara utakuwa wa uhakika.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akiufungua Mkutano wa Kimataifa wa Siku mbili wa Mapitio ya Sekta ya Afya unaofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Ocean View Kilimani mjini Zanzibar na kushirikisha wawakilishi kutoka Taasisi za Kimataifa, Binafsi pamoja na watendaji waandamizi wa Taasisi za Serikali.
Alisema shauku ya Viongozi wa kisiasa ndani ya majimbo mbali mbali nchini kwa kushirikiana na wananchi wao katika kuelekeza nguvu zao kwenye ujenzi wa vituo vya Afya pamoja na Nyumba za Madaktari imeleta faraja kubwa kwa Wizara ya Afya katika utekelezaji wa majukumu yake.
Balozi Seif alifahamisha kwamba udhibiti wa maradhi mbali mbali hapa nchini umechangia kuongezeka kwa umri wa Wananchi kutoka miaka 57 kwa mujibu wa Sensa ya mwaka 2002 hadi miaka 66 kwa sensa ya mwaka 2012.
Alielezea faraja na matumaini yake kwamba hatua hiyo imeifanya Zanzibar kufikia kiwango kinachoridhisha katika mipango iliyojiwekea kwenye malengo ya millennia pamoja na Dira ya Taifa ya 2020.
“ Tunakwenda vyema na Malengo ya Milenia hasa katika kupunguza vifo vya watoto wanaozaliwa ambavyo vimedhibitiwa na kufikia watoto 40 wanaofariki kati ya 1000 wakati sensa ya mwaka 2012 ilionyesha watoto 46 kati ya 1000 walikuwa wakifariki Dunia “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizishukuru Taasisi za Kimataifa na zile za Kitaifa pamoja na Nchi washirika wa Maendeleo zilizojitolea kuunga mkono mipango ya Kiuchumi na Maendeleo ya Zanzibar na kuziomba ziendelee na jitihada hizo.
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar Dr. Saleh Mohammed Jidawi alisema tahadhari madhubuti itaendelea kuchukuliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na washirika wa Maendeleo katika kuona maradhi mbali mbali yanadhibitiwa.
Dr. Jidawi alieleza kwamba tahadhari hiyo imelenga kutoa huduma bora za Afya kwa jamii ili kwenda sambamba na Dira ya Taifa ya 2020 pamoja na Mpango wa malengo ya Milenia.
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Afya amelishukuru shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia Idadi ya Watu { UNFPA } na Shirika la Maendeleo la Denmark { Danida } kwa kudhamini Mkutano huu wa Kimataifa wa Siku mbili wa Mapitio ya Sekta ya Afya hapa Zanzibar.
Alisema hizi ni juhudi zinazoonyesha Mashirika hayo kuunga mkono mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha ustawi wa Wananchi wake kupitia huduma za Afya.
Akitoa salamu kwa Niaba ya Taasisi za Kimataifa zinazotoa huduma Nchini Tanzania Mwakilishi Mkazi wa Shirika na Afya Duniani {WHO } Hapa Zanzibar Dr. Adymichael Ghirmany ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi na nguvu zake kubwa inazochukuwa katika kukabiliana na maradhi tofauti yanayowakumba Wananchi wake.
Dr.Ghirmany alisema juhudi hizo zinazoendelea kushuhudiwa na Taasisi za Kimataifa zimechangia kupungua kuenea kwa maradhi mbali mbali ambao mengi kati yake hupatikana katika nchi za ukanda wa Joto.
“ Tumeshuhudia juhudi za Serikali ya Zanzibar katika kupambana na udhibiti dhidi ya maambukizi kama Ukimwi, Malaria, Homa ya Mapafu, kifua kikuu na kupungua chini ya kiwango kinachokubalika kimataifa “. Alifafanua Dr. Ghirmany.
Mwakilishi Mkazi huyo wa Shirika la Afya Duniani { WHO } aliihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwamba Taasisi za Kimataifa zitaendelea kuiunga mkono katika juhudi hizo ili lengo lililojipangia la kufikisha huduma za Afya kwa wananchi hasa Vijijini lifanikiwe vyema.
Akimkaribisha Mgeni rasmi kuufungua Mkutan o huo Naibu Waziri wa Afya Mh. Mahmoud Thabit Kombo alisema mchango mkubwa uliotolewa na taasisi za Kiataifa na zile za Kitaifa katika kuunga mkono sekta ya Afya zimesaidia kufanya mabadiliko makubwa ya huduma za Afya hapa Nchini.
Mh. Mahmoud aliitaja baadhi ya miradi iliyopata ufadhili wa Taasisi hizo za Kimataifa kuwa ni pamoja na matengenezo ya baadhi ya Vitengo vya huduma za Afya katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja, ujenzi wa Hospitali ya Abdulla Mzee Mkoani Pemba pamoja na huduma za kudhibiti magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi.
Naibu Waziri huyo wa Afya Zanzibar alifahamisha kwamba Mkutano huo mbali ya kuwa na malengo ya mapitio ya afya lakini pia umetoa fursa ya kuimarisha uhusiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya na Washirika wa Maendeleo wa Kimataifa.
Mkutano huo wa Kimataifa wa siku mbili wa Mapitio ya Sekta ya Afya Zanzibar unahudhuriwa na wakurugenzi wa baadhi ya Taasisi za Serikali, wataalamu na watendaji wa sekta ya afya, Mipango pamoja na wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa zinazotoa huduma Nchini Tanzania.